UFUGAJI WA NYUKI WATAJWA KUWA NGUZO YA CHAKULA NA MAZINGIRA

NA FAUZIA MUSSA
WAKATI dunia ikiendelea kuadhimisha siku ya nyuki Duniani, jamii imetakiwa kuongeza juhudi za kuwahifadhi nyuki kutokana na mchango wao mkubwa katika uzalishaji wa chakula, uhifadhi wa mazingira pamoja na maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Wito huo umetolewa na wanachama wa Kikundi cha Ustawi wa Jamii Chuini kinachojishughulisha na ufugaji wa nyuki, walipozungumza na mwandishi wa habari hii kuelekea maadhimisho hayo.
Mmoja wa wanachama wa kikundi hicho, Suleiman Mwalimu Iddi, alisema nyuki ni viumbe muhimu sana katika maisha ya binadamu kutokana na mchango wao katika uzalishaji wa asali pamoja na kusaidia uchavushaji wa mimea mbalimbali ya chakula na misituni.

Alisema zipo aina tofauti za nyuki wakiwemo wa pwani, milimani na tambarare ambapo baadhi yao huuma na wengine hawana tabia ya kuuma, lakini wote wana nafasi kubwa katika kulinda mazingira na kuongeza uzalishaji wa mazao.
“Nyuki wana faida kubwa kwa binadamu na mazingira. Mbali na kutupatia asali, wanasaidia uchavushaji wa mimea jambo linaloongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na miti ya asili,” alisema Suleiman.
Wanachama hao walieleza kuwa hapo awali hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa nyuki, lakini kupitia mafunzo waliyopewa na Taasisi ya Can Tanzania inayojishughulisha na masuala ya mabadiliko ya tabianchi, wameweza kutambua thamani ya viumbe hao katika afya, mazingira na uchumi wa jamii.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Hussein Ali Kombo, alisema elimu waliyoipata imewasaidia kuachana na ufugaji wa mazoea na kuanza kutumia njia za kisasa za ufugaji wa nyuki kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kipato cha familia zao.

Alisema kupitia mafunzo hayo wamegundua kuwa nyuki ni rasilimali muhimu inayoweza kuchangia maendeleo ya jamii ikiwa watahifadhiwa na kutunzwa vizuri.

Naye Katibu Msaidizi wa kikundi hicho, Haji Khamis Hassan, alisema ufugaji wa nyuki umeanza kuwanufaisha kiuchumi wanachama wa kikundi hicho huku ukiwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na viumbe hai.
Alisema zamani walikuwa wanawaogopa nyuki na kuwaona kama wadudu hatari, lakini sasa wamebaini kuwa ni chanzo muhimu cha kipato na maendeleo ya familia zao.
“Awali tulikuwa tunawaona nyuki kama maadui, lakini sasa tumegundua kuwa ni marafiki wa binadamu. Kupitia ufugaji huu tunapata asali halisi inayotusaidia kuongeza kipato na kuhudumia familia zetu,” alisema Haji.

Aliongeza kuwa kwa sasa mzinga mmoja unaweza kutoa hadi chupa 40 za asali zenye ujazo wa lita moja na nusu ambapo kila chupa huuzwa kwa shilingi 45,000 hali inayowasaidia wanachama kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake, mwanachama mwingine wa kikundi hicho, Mwamke Juma Silima, alisema mwanzoni walikumbwa na changamoto ya ukosefu wa elimu ya ufugaji wa kisasa jambo lililosababisha kuchelewa kuvuna asali kutokana na kutofahamu tabia za nyuki hasa kipindi cha mvua.

Alisema katika msimu uliopita walikosa mavuno baada ya nyuki kutumia asali yote kama chakula wakati wa mvua kutokana na wao kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mzunguko wa maisha ya nyuki.
“Hatukujua kuwa wakati wa mvua nyuki hutumia asali yao kama chakula. Tulipofika kuvuna tulikuta tayari wameshatumia asali yote,” alisema.

Siku ya Nyuki Duniani huadhimishwa Mei 20 kila mwaka, huku maadhimisho ya mwaka huu yakibebwa na kauli mbiu isemayo, “Uhifadhi wa Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Taifa Letu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *