Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza thamani ya zao la mwani kupitia uanzishaji wa viwanda vya usindikaji, ili kuongeza kipato cha wakulima, kupanua masoko na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Zanzibar kimataifa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 01 Julai 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Mhe. Susan Ngongi Namondo.
Amesema Serikali iko tayari kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa katika kuendeleza kilimo cha mwani kupitia mafunzo, teknolojia, mitaji na huduma za kifedha, huku akiushukuru Umoja huo kwa mchango wake katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Kwa upande wake, Mhe. Susan Ngongi Namondo amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza sekta ya mwani na kuongeza thamani ya zao hilo, pamoja na kuandaa filamu maalum ya kuitangaza Zanzibar na fursa za uwekezaji katika kilimo cha mwani duniani
