TAMWA ZNZ YAWAFIKIA WATU 2,791 KUWAPA ELIMU YA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WASICHANA

Na Abdul Sakaza

Jumla ya watu 2,791 kutoka Unguja na Pemba wamefikiwa na elimu ya uhamasishaji wa jamii kuhusu kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kupitia shughuli mbalimbali za uelimishaji zilizotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA Zanzibar).

Taarifa hiyo ilitolewa jana katika ukumbi wa mikutano wa TAMWA Zanzibar ,Tunguu Mkoa Kusini Unguja na Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA Zanzibar, Mohammed Khatib Mohammed, wakati akiwasilisha matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa “Tunaweza Pamoja”, unaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) kwa kushirikiana na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa unaolenga kujenga jamii salama na yenye usawa wa kijinsia.

Akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha wadau mbalimbali wanaopambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na wasichana, Mohammed alisema kuwa katika kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu, watu 2,791 walifikiwa na elimu hiyo kupitia mikutano na kampeni za uhamasishaji zilizowahusisha madereva wa boda boda, bajaji, dala dala, wakulima pamoja na makundi mengine maalumu ya kijamii.

Alisema elimu hiyo imelenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia, umuhimu wa kuripoti matukio ya ukatili pamoja na kushiriki katika juhudi za kulinda haki za wanawake na wasichana.

Aidha, aliwataka wadau waliofikiwa na mafunzo hayo kuendelea kuwa mabalozi wa mabadiliko katika maeneo yao kwa kutoa elimu waliyoipata kwa wananchi wengine ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake, Afisa Programu wa TAMWA Zanzibar ambaye pia ni Afisa wa Mradi wa “Tunaweza Pamoja”, Asia Hakim, alisema tathmini zilizofanyika katika kipindi cha Machi hadi Mei zinaonyesha kuwa bado kuna haja ya kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii ili kubadili mitazamo inayochochea ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Alieleza kuwa ushiriki wa wadau mbalimbali katika shughuli za mradi huo umechangia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya haki za wanawake na watoto wa kike, huku akiwahimiza washiriki kuwa sehemu ya kutetea haki hizo na kushiriki kikamilifu katika kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.

Nao washiriki wa mkutano huo waliishukuru TAMWA Zanzibar kwa kuendelea kuwajengea uwezo na kuwapatia elimu inayowasaidia kutekeleza majukumu yao katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na wasichana katika jamii.

Kwa mujibu wa takwimu za Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia zilizotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Takwimu Zanzibar (OCGS) mwaka 2025, jumla ya matukio 1,228 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa Zanzibar, huku waathirika wakifikia 1,230. Kati ya waathirika hao, watoto walikuwa 1,050 sawa na asilimia 85.4, wanawake 162 sawa na asilimia 13.2 na wanaume 18 sawa na asilimia 1.5.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa wanawake na watoto wa kike bado ni miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi na vitendo vya ukatili wa kijinsia, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha juhudi za uelimishaji, uhamasishaji na ulinzi wa haki za makundi hayo katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *