ZRA YAAHIDI KUSAIDIA UTATUZI CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA

Na. Muandishi Wetu.

Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imesema imeahidi kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara ili kuleta ustawi wa biashara na ulipaji Kodi Nchini.

Hayo yamesemwa leo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ndugu Said Kiondo Athumani kwa wakati tofauti alipofanya ziara ya kuwatembelea Walipakodi Wakubwa nchini.

Kamishna Kiondo alisema taasisi yake inafahamu kuwa ustawi mzuri wa biashara ndio chachu kuimarika ukusanyaji wa mapato nchini na kwamba ZRA itahakikisha inashirikiana na wadau na Serikali kwa ujumla ili kuwasaidia walipakodi kuondokana na changamoto hizo.

Alifafanua kuwa, kwa kufahamu nafasi ya Wafanyabiashara katika ukuaji wa Uchumi wa nchi pamoja na maendeleo yake yanayosababishwa na Kodi wanazozilipa, ZRA inathamini mchango huo na itaendelea kuwaunga mkono katika kila hatua ili kuwawezesha kufanya biashara zao katika mazingira bora.

Kwa upande mwengine, Kamishna Mkuu alisisitiza kuwa kiasi cha kodi kinacholipwa na wafanyabiashara kinapaswa kuendana na ukubwa wa biashara zinazofanywa huku akionesha dukuduku kuwa baadhi ya biadhara zimekuwa zikilipa Kodi kidogo tofauti na ukubwa halisi wa biashara zao.

Alisema Mamlaka itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wafanyabiashara lakini walipakodi wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zote za Kodi nchini ili kuhakikisha kodi sahihi ya Serikali inalipwa na Walipakodi wanabaki upande salama.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika ofisini kwao Mlandege, Mkurugenzi mtendaji wa Kampouni ya Premier Enterprise Limited ndugu Humoud Nassor Al-Rawahy alielezea kufurahishwa kwake na ziara hiyo ya Kamishna Mkuu na kusema kuwa inaonesha namna anavyowajali na kuwathamini Walipakodi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Muendeshaji waa Kampuni ya Yassir Provision ndugu Walid Yakoub Abdulkarim alimpongeza Kamishna Mkuu wa utaratibu wake aliouanzisha wa kuwatembelea Walipakodi na akabainisha kuwa unalenga kujenga mahusiano mema baina ya ZRA na wadau wake.

Katika ziara zilizofanyika leo, Kamishna Mkuu Kiondo alipata nafasi ya kuzitembelea Kampuni mbili ambazo zinajihusisha na uingizaji wa bidhaa mbali mbali nchini.

Huu ni mfululizo wa ziara za Kamishna Mkuu wa ZRA kwa Walipakodi zinazolenga kuhimiza ulipaji kodi wa hiari, matumizi ya Mashine za Risiti, na kusikiliza changamoto zao za kikodi ambazo ZRA imeahidi kuzishughulikia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *