Na. Muandishi wetu
Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), imesema itawachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wasiotumia ipasavyo mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki wakati wa mauzo.
Kauli hiyo imetolewa leo Kamishna Mkuu wa ZRA ndugu Said Athumani Kiondo baada ya kufanya ziara ya kukagua uwajibikaji wa Walipakodi ikiwemo matumizi sahihi ya mashine za kutolea Risiti za kieletroniki katika eneo la Mlandege, Mjini Unguja.
Kamishna Kiondo alisema katika ziara hiyo ZRA imebaini kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao mauzo yao hayaendani na ukubwa wa biashara zao hivyo aliwataka kutumia vyema mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki ili kutimiza wajibu wao wa kisheria.
Alibainisha kuwa, ZRA itaendelea kutumia kila mbinu katika kuwahamasisha Walipakodi kwa kuwa ni jukumu mama la taasisi hiyo na akabainisha kwamba Walipakodi wanapaswa kukumbushwa mara kwa mara ili kuwasaidia kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi inayostahiki.
Sambamba na hayo, Kamishna Mkuu Kiondo, aliwatanabahisha wafanyabiashara wenye tabia ya kutotoa Risiti kwa usahihi ili wakwepe kulipa kodi kuwa nchi haijengwi na mtu mmoja badala yake kila mmoja anapaswa kuchangia maendeleo ya nchi yake.

Naye, Mfanyabiashara wa eneo la Mlandege, ndugu Ahmed Massoud Khamis alisema amefurahishwa na ziara ya Kamishna mkuu iliyofanywa katika eneo la Mlandege na akadokeza kuwa itampa mazingira halisi ya kutambua namna ya biashara inavyokwenda.
Alisema ni matarajio ya Wafanyabiashara wa eneo hilo kuwa ziara hiyo itapunguza dhana au malalamiko kutoka kwa ZRA ya kuwa mapato wanayoyalipa kidogo huku akidai kuwa sababu hayo ni biashara kutotengemaa.
Sambamba na hayo alipongeza ziara hiyo ya Kamishna Mkuu na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wake kwa kutembelea mazingira halisi ya wafanyabiashara badala ya kujifungia ofisini pasi na kuyafahamu mwenendo wa biashara ulivyo.

Ziara hii ya Kamishna Mkuu wa ZRA kwa wafanyabiashara wa Mlandege inaashiria ufunguzi rasmi wa zoezi la ukaguzi wa uwajibikaji wa wafanyabiashara nchi nzima.
Ukaguzi ambao unatarajiwa kutamatika mwishoni mwa Mwezi wa sita 2026 na kwamba utawagusa wafanyabiashara wa makundi mbali mbali Unguja na Pemba.
