SERIKALI YA ZANZIBAR KUHAKIKISHA VIJANA WANAPATIWA FURSA,MAFUNZO,MITAJI KUONDOKANA NA UTEGEMEZI

NA FAUZIA MUSSA

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Salama Mbarouk Khatib, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na mashirika na taasisi binafsi katika kuhakikisha vijana wanapatiwa fursa za mafunzo na mitaji itakayowawezesha kujiendeleza na kuondokana na utegemezi.

Akifungua mafunzo ya siku tatu ya ujasiriamali kwa vijana 75 yaliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Watoto la SOS Children’s Villages Zanzibar, yaliyofanyika katika Kituo cha Walimu Bububu (Bububu TC), Katibu Mkuu huyo alisema kuanzishwa kwa wizara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha vijana wananufaika na fursa zilizopo Nchini Katika kuendeleza mawazo Yao ya kibiashara na ujasiriamali kwa ujumla.

Alieleza kuwa uwepo wa mashirika kama SOS unasaidia kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwainua vijana kiuchumi kupitia elimu ya ujuzi, maarifa na kazi za mikono.“Serikali imejipanga kuhakikisha kila kijana anakuwa na shughuli halali ya kumuingizia kipato.Kupitia elimu ya ujuzi na mafunzo ya ujasiriamali tunaenda kuwasaidia vijana kujiajiri, kuajirika na hata kuajiri wengine,” alisema Salama.

Aliwataka vijana kutumia ipasavyo fursa ya mafunzo hayo wanayopatiwa bila malipo, akisisitiza kuwa ujasiriamali hauhitaji mtaji mkubwa bali unahitaji malengo madhubuti, nidhamu na tathmini sahihi ya biashara wanazotaka kuanzisha au kuziendeleza.

Aidha, aliishukuru SOS kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwawezesha vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa, akieleza kuwa vijana wengi wangetumia gharama kubwa kupata mafunzo kama hayo endapo yasingetolewa bure.Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Vijana na Jinsia Taifa kutoka SOS Zanzibar, Evelyne Baruti, alisema mafunzo hayo yamewashirikisha vijana kutoka mabaraza ya vijana na shehia mbalimbali zilizonufaika na mradi wa uwezeshaji vijana unaotekelezwa na shirika hilo.

Alisema lengo la mradi huo ni kuhakikisha vijana wanajitambua, wanakuza vipaji vyao na kupunguza idadi ya vijana wasiojishughulisha mitaani.“Tumezingatia maelekezo yaliyomo katika Sera ya Vijana ya kuimarisha malezi mema, ajira na ujasiriamali. Vijana hawa ndio watakaounda familia na kuisimamia jamii ya kesho, hivyo ni lazima tuwawezeshe leo,” alisema Baruti.

Aliongeza kuwa SOS imewekeza katika kuwajengea vijana uwezo wa kuanzisha na kuendesha vikundi vya kuweka na kukopa, ili kuwapa elimu ya fedha, nidhamu ya matumizi na mbinu za kukuza mitaji yao.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaibu Mohammed Ibrahim alisema SOS ni mshirika muhimu wa Serikali katika mapambano dhidi ya umaskini kwa vijana, akibainisha kuwa tayari baadhi ya washiriki wameshapatiwa mitaji midogo ya kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali, ikiwemo biashara za ushonaji na kazi nyingine za amali.

Alisisitiza kuwa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana ni funguo ya milango ya ajira binafsi na rasmi, na kwamba vijana wanapaswa kujiunga na mabaraza ya vijana na kuanzisha vikundi ili kurahisisha upatikanaji wa msaada na rasilimali.“Maeneo haya yanawaunganisha vijana bila kujali dini, rangi au kabila. Tukitaka kumwezesha kijana mmoja mmoja itakuwa ngumu, lakini kupitia vikundi tunaweza kuwafikia wengi kwa wakati mmoja,” alisema.

Mapema aliekeza matumaini ya Idara ya Vijana kupitia Mafunzo hayo ni kuwa vijana watanufaika na elimu ya vitendo, kubuni miradi bunifu na kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.Kauli mbiu ya mafunzo hayo ni “Mafunzo ya Ujasiriamali kwa Vijana ni Funguo ya Fursa za Ajira na Kujitegemea.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *