CFP YANUNUA VIFAA VYA MIUNDOMBINU YA MAJI YENYE THAMANI YA MILIONI 150,000 KWA WAKULIMA WA KILIMO MSETO BUNGI

Na Abdul Sakaza

Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa kwa wakulima wa kilimo mseto katika kijiji cha Bungi,wilaya ya kati mkoa wa Kusini Unguja,Kupungua kwa mvua za msimu, kuongezeka kwa joto, na mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa yameathiri uzalishaji wa mazao mbalimbali, hivyo kuhatarisha ustawi wa wakulima pamoja na matatizo ya ardhi kukauka, hali inayosababisha kupungua kwa rutuba na kushindwa kuzalisha kwa kiwango cha kuridhisha.

Athari hizi zimepelekea kupungua kwa mavuno, hali inayosababisha uhaba wa chakula na kupanda kwa bei ya mazao sokoni kwa mfano kwasasa mazo ya mboga mboga kama vile mchicha, nyanya, bilingani, karoti, pilipili hoho, kitunguu, bamia, na spinachi yamepanda bei katika masoko mbali mbali kama vile soko la mwanakwereke na jumbi.

Kwa mujibu wa Utafiti na Ripoti ya hali ya mazingira ya Zanzibar ya mwaka 2021 iliyofanya na ofisi ya makamo wa kwaza wa rais Zanzibar kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa uchumi wa Zanzibar umebaini kuwa Zanzibar inakabiliwa na ongezeko la kiwango cha joto, kubadilika kwa majira ya mvua, kuongezeka upepo mkali wakati wa kusi na kaskazi, ongezeko la kina cha bahari, mawimbi yake  na kuongezeka kwa matukio ya maafa, yote yakihusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa

Fatma Haji, mkulima wa kilimo mseto kwa miaka 15 Bungi, anasema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, mvua zimekuwa chache na zisizotabirika.

“Zamani mvua zilikuwa zinanyesha kwa msimu wake, lakini sasa hatujui lini italeta mafuriko na lini itakosekana kabisa,Migomba yangu mwaka jana mwazoni ilishindwa kuzaa vizuri kwa sababu mvua ilianza kuchelewa na ilipokuja ilikuwa nyingi kupita kiasi,” anasema Fatma.

Mbali na athari hizo, magonjwa ya mazao yameongezeka kutokana na joto kali na unyevunyevu usiotabirika hali inayo sababisha Wakulima wengi wanakumbana na changamoto ya kuongezeka kwa wadudu waharibifu kama vile viwavijeshi na vidukari ambavyo vinaharibu mazao kabla ya kuvunwa.

Wakulima hawa wanasema ili kukabiliana na hali hii, baadhi yao wameanza kutumia mbegu zinazostahimili ukame, mbinu za kilimo cha mzunguko, na upandaji wa miti ili kuboresha mazingira na kuhifadhi unyevunyevu ardhini.

Kurwa Daniel ni mkulima kutoka Bungi, ambaye kwa sasa anatumia mbinu za kilimo mseto ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,anasema ameanza kutumia mbegu zinazostahimili ukame pamoja na mbinu za kilimo cha mzunguko ili kuongeza uzalishaji wa mazao yake na kuimarisha rutuba ya ardhi pia anapanda miti kwa lengo la kuhifadhi unyevunyevu ardhini, kupunguza athari za upepo mkali na kuboresha mazingira kwa ujumla. Kwa kutumia mbinu hizi, Daniel anajitahidi sio tu kuongeza mazao yake, bali pia kulinda mazingira yake dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Juma Ali, mkulima wa mazao na mfugaji wa kuku kutoka Bungi, yeye anasema kuwa mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kuongezeka kwa magonjwa ya mazao na mifugo, hali inayozidisha changamoto kwa wakulima na wafugaji ,Ali anasema kuwa vipindi vya mvua zisizo na utabiri na jua kali vinavyoshuhudiwa sasa vinachangia kuenea kwa magonjwa ya mazao kama vile madoa meusi na kuoza kwa mazao, pamoja na magonjwa ya mifugo kama vile homa ya mapafu na Hali hii imeongeza mzigo kwa wakulima na wafugaji.

“Joto linapoongezeka,wadudu waharibifu wanaongezeka pia,Tumekuwa tukitumia gharama kubwa kununua madawa ili kuokoa mazao yetu,Pia kuku wangu wanapata magonjwa mara kwa mara, hali ambayo haikuwepo sana miaka ya nyuma,” anasema Juma.

Mabadiliko ya tabianchi yameathiri sio tu kilimo bali pia maisha ya kijamii katika maeneo ya wakulima wa kilimo mseto,Wakulima wengi wanashindwa kupata kipato cha kutosha kutokana na upungufu wa uzalishaji, ambapo mabadiliko ya hali ya hewa yamepunguza mazao na kuongeza gharama za kilimo,Hali hii imewafanya wakulima wengi kutafuta fursa nyengine za kiuchumi mijini,ambapo wanajaribu kutafuta ajira mbadala ili kuendeleza maisha yao.

Aidha, changamoto hizi pia zimewalazimu baadhi ya wakulima kupunguza idadi ya mazao wanayolima ili kupunguza hasara kutokana na uhaba wa maji na magonjwa ya mazao,Ingawa wanajitahidi kuboresha kilimo chao, wengi wamejikuta wakiishi katika mazingira magumu, na hivyo kuathiri si tu uchumi wao bali pia ustawi wa familia zao.

Kwa mujibu wa Mzee Hassan Mabula, mkulima mkongwe wa Bungi, anasema wakazi wa kijiji wanakabiliana na changamoto kubwa ya chakula na kipato. “Zamani tulikuwa tunazalisha chakula cha kutosha na kuuza ziada,Siku hizi tunalima kwa shida na hata hatuwezi kuhifadhi mazao yetu kwa muda mrefu kwa sababu ya ukame na wadudu waharibifu,” anasema Mzee Hassan.

Mbali na mabadilko ya tabia nchi kusababisha athari kwa wakulima wa kilimo mseto ,ikiwemo changamoto za magonjwa ya mazao na mifugo, upatikanaji wa maji pia ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayowakumba wakulima katika maeneo ya Bungi.

Mariam Nkakuba anasema kuwa maji wanayoyategemea hutoka kwa msimu mmoja tu kwa kipindi cha siku moja, na mara nyingi huwa hayatoshi kwa matumizi ya kila siku,Hali hii inazidisha ugumu wa kilimo kwani maji ni rasilimali muhimu katika ustawi wa mazao na mifugoHatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya TabianchiLicha ya changamoto hizi, wakulima wa Bungi wameanza kuchukua hatua za kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi,Fatma ngole ni mkulima wa kilimo mseto anasema kuwa sasa wanapanda miti ya kivuli na kutumia mbinu za kuhifadhi unyevunyevu kwenye udongo kama vile kutumia majani makavu kufunika ardhi.

kuwepo kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi katka kilimo mseto katika kijiji cha bungi taasisi mbali mbali zimewapa mafuzo ya kulima kilimo mseto ili kukabiliana na changamoto hizo kwamfano community forest pemba (CFP) imewawezesha wakulima kuwapa mafunzo na mbinu bora za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula unaendelea kwa ufanisi.

Mbarouk Mussa Omar ni Mkurugenzi wa Jumuiya ya Misitu Pemba (Community Forest Pemba, CFP) anasema kupitia mradi wa Zanzibar Women Leadership in Adaptation (Zan Adapt) Jumla ya shilingi million 150,000 za kitanzania zimetumika kununua vifaa vya mindombinu ya maji, Kwa wanufaika wa kilimo mseto, ili kulima na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nakusema kua lengo la mradi wa ZanzAdapt ni kuwawezesha wanawake  Kwa kuwapa mafunzo na Miche ya miti mbali mbali, ili kulima na kuinua vpiato vyao kiuchumi

Shabani Peter, ni Ofisa wa teknolojia  ya Uzalishaji wa mradi wa ZanzAdapt, amesema mradi huo umefadhiliwa na Global Affair Canada, na umetoa elimu  na  mafunzo ya kilimo ,Kwa wanawake  zaidi ya asilimia  80, wa Unguja na Pemba, kuhusu kilimo mseto , mabadiliko ya tabianchi na kumfanya mwanamke awe kiongozi katika kukabiliana nayo.

Pia shabani anasema kupitia mradi huo wanalenga kuwafikia wakulima 4,000 wakiwemo wa bungi na kati ya hao asilimia 80 ni wanawake ili kuwapa elimu na mbinu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwamo kupanda miti.Mradi huo, unatekelezwa Kwa kushirikiana na Shirika la Misitu Duniani (C F I), Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar, (TAMWA ZNZ)  na Taasisi ya Community Forest Pemba,(CFP).

Mwatima Abdallah Khamis, Ofisa Misitu kwa Jamii kutoka Idara ya Misitu Zanzibar , anasema kuwa shughuli za kibinadamu ni miongoni mwa sababu kuu za uharibifu wa mazingira, ambapo matokeo yake ni pamoja na kuongezeka kwa uharibifu wa maeneo ya kilimo na makazi kutokana na mabadiliko ya uharibifu huo .

Anasisitiza kuwa juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa mazingira, kama vile kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira, ni muhimu katika kupunguza madhara haya Hasa upandaji wa miti unachukuliwa kama suluhisho muhimu kwa sababu miti husaidia kuleta mvua na kupunguza ukame. Hata hivyo, ili kudhibiti hali hii, juhudi za pamoja na ushirikiano wa wananchi ni muhimu, kwani athari za mabadiliko ya mazingira zinakwamisha mipango ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu.

Serikali ya Zanzibar kupitia Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo mheshimiwa Shamata Shaame Khamis amesema wizara inaendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya mbinu za kisasa za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Programu za umwagiliaji mdogo, upatikanaji wa mbegu bora, na matumizi ya teknolojia za kisasa kama kilimo cha kisasa cha umwagiliaji (drip irrigation) ni miongoni mwa mikakati inayopendekezwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *