“HAKIKISHENI WATOTO WOTE WANASAJILIWA NA KUPATIWA VYETI VYA KUZALIWA” DOKTA. MWINYI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Ofisi ya Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar kushirikiana na Masheha kuhakikisha watoto wote wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa ili kuisaidia serikali kupata takwimu sahihi pindi zinapohitajika.

Ametoa agizo hilo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya usajili Barani Africa kilichofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil, Kikwajuni Mkoa wa Mjini Magharib.

Rais Dkt. Mwinyi amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usajili wa matukio ya kijamii ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa haraka wa kumbukumbu na nyaraka muhimu za matukio ya kijamii ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho.

Aidha, Dkt. Mwinyi amefahamisha kua suala la utambuzi wa kisheria wa kidigitali ni jambo lisiloepukika hivyo amewataka wananchi kufika katika vituo vya usajili ili kusajili matukio ya kijamii mara tu yanapo jitokeza katika maeneo yao.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Mohamed amewataka watendaji wa ofisi ya usajili wa matukio ya Kijamii kufanya kazi kwa bidii huku wakitambua kua juhudi zao zitakua alama nzuri kwa vizazi vijavyo.

Akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya usajili Barani afrika Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Usajili wa Matukio ya kijamii Zanzibar Muhamedi Ame Makame amesema hadi kufikia sasa aslimia 98 ya vizazi vyote vinavyotokea ndani ya Zanzibar vinasajiliwa.Amesema hali hiyo imetokana na utowaji wa humuda za usajili wa matukio ya kijamii kwa njia ya mifumo ya Kielektroniki na kupelekea taasisi mbali mbali kuomba kuunganishwa na mifumo ya usajili ili ziweze kutoa huduma kwa ufanisi.

Siku ya usajili Barani Africa huadhimishwa kila mwaka ikifikapo tarehe 10 Agusti ambapo kwa upande wa Zanzibar huadhimishwa na Wakala wa usajili wa Matukio ya kijamii Zanzibar yenye Kauli mbiu isemayo “usajili wa Matukio ya kijamii ni msingi wa miundombinu ya kidigitali na utambulisho wa kisheria Zanzibar”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *