
Jumla ya wageni 98,370 wameingia nchini kwa mwezi wa Julai 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 45.2 ikilinganishwa na wageni 68,223 waliowasili mwezi kama huo mwaka 2024.
Takwimu hizo zilitolewa jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mazizini, ambapo Mtakwimu kutoka Seksheni ya Takwimu za Utalii, Fatma Hilali Moh’d, alieleza kuwa idadi hiyo inaonesha mafanikio makubwa katika sekta ya utalii nchini.
Kwa mujibu wa Fatma, Italia imeongoza kwa kuleta idadi kubwa ya wageni, ambapo jumla ya wageni 10,403 kutoka nchi hiyo waliwasili, sawa na asilimia 10.6 ya wageni wote huku Ufaransa ikishika nafasi ya pili kwa wageni 7,593, sawa na asilimia 7.7.
Aidha, alifafanua kuwa asilimia 90.8 ya wageni wote (89,325) waliingia Zanzibar kupitia viwanja vya ndege, huku 9,045 wakiwasili kupitia bandarini.

Kwa upande wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, ofisa Uhusiano Shariff Bakari Shariff alieleza kuwa kati ya wageni walioingia nchini, 2,947 walikuwa ni Watanzania, ambapo 2,143 kati yao walitoka nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali,Hata hivyo, alieleza kuwa mtu mmoja kati yao alizuiliwa kuingia nchini kwa sababu mbalimbali.
Shariff aliongeza kuwa wageni 213 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuishi nchini kinyume cha sheria na kuzidisha muda wa ukaaji. Kati yao, 164 walipewa adhabu ya kulipia vibali maalumu ili kuhalalisha ukaazi wao.Katika hatua zaidi za kisheria, wageni watatu wamepelekwa mahakamani, sita wakitakiwa kuondoka nchini, na ishirini wanaendelea kuhojiwa na vyombo husika.

Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kuhusu watu wasiowafahamu wanaoishi nchini kinyume cha sheria.Kwa upande wake, Maabad Jaffar Muhidini kutoka Kamisheni ya Utalii alitaja sababu zilizopelekea ongezeko hilo la wageni, zikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya usafiri angani na baharini pamoja na mabadiliko ya sera ya utalii.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuimarisha miundombinu hiyo kwa lengo la kuvutia wageni zaidi kufika visiwani Zanzibar.
