Na Abdul Sakaza
follow up story
Imeboresha saa 9 zilizopita
Wananchi Mkoa wa Kaskazini Unguja wamepongeza uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo, Cassian Gallos Nyimbo, kwa kuwateua Masheha wapya katika shehia mbalimbali, huku wakiwataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki, uwajibikaji na usawa bila kuathiriwa na tofauti za kisiasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Sakaza Digital, baadhi ya wananchi walisema uteuzi huo umefanyika wakati ambao jamii inahitaji viongozi wa ngazi ya shehia watakaoweka mbele maslahi ya wananchi wote, bila kujali itikadi za vyama vya siasa, dini au makundi ya kijamii.
Mkazi wa Shehia ya pitanazako, Asha Ali Juma, alisema masheha ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma kwa usawa na kwa mujibu wa sheria
“Tunawapongeza viongozi walioteuliwa, lakini tunawaomba watambue kuwa wao ni viongozi wa wananchi wote. Wajiepushe na upendeleo wa kisiasa na wahakikishe haki inatendeka kwa kila mmoja,” alisema Asha
Ali Suleiman ni mkazi wa Shehia ya Kiwengwa, alisema wananchi wanatarajia kuona masheha wapya wakisimamia maendeleo ya shehia zao kwa kushirikiana na wananchi badala ya kujikita katika migawanyiko ya kisiasa.
“Tunataka viongozi watakaotusikiliza, watakaokuwa karibu na wananchi na kutatua changamoto zetu kwa kuzingatia sheria na maslahi ya umma, siyo itikadi za vyama vya siasa,” alisema.
Kwa mujibu wa wananchi hao, mafanikio ya uongozi wa shehia yatategemea uwezo wa masheha kushirikisha wananchi katika maamuzi ya maendeleo, kusimamia amani na utulivu pamoja na kuimarisha uwajibikaji katika maeneo yao.

Haya yanajiri baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo mapema jana kutangaza uteuzi wa Masheha wapya katika Wilaya za Kaskazini ‘A’ na Kaskazini ‘B’ ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi na masheha waliostaafu na kuimarisha utendaji wa Serikali katika ngazi ya shehia.
Katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ walioteuliwa ni Hussein Haji Bilali (Moga), Mcha Silima Juma (Muwange), Faidini Vuai Fumu (Matemwe), Juma Mossi Baya (Kigomani), Haji Pili Faki (Jugakuu), Ali Abass Hamad (Potoa), Hassan Haji Sheha (Gomani) na Muhammed Khamis Muhammed (Pitanazako).
Kwa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ walioteuliwa ni Maulid Masoud Ame (Kiwengwa), Shabani Sarboko Makarani (Mangapwani), Mossi Ame Mossi (Mahonda), Kijakazi Muhammedi Machano (Upenja), Khamis Makame Mzee (Gube) pamoja na Masoud Kassim Ali (Zingwezingwe).
Mkoa wa Kaskazini Unguja una jumla ya shehia 75, ambapo 44 zipo Wilaya ya Kaskazini A na 31 zipo Wilaya ya Kaskazini B. Hivyo, wananchi wanasema uteuzi wa masheha wapya ni hatua muhimu ya kuimarisha utawala wa ngazi ya msingi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa jamii
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo , shughuli ya kuwaapisha masheha hao wapya inatarajiwa kufanyika Alhamisi, tarehe 2 Julai 2026.
