Na Abdul Sakaza
Imeboreshwa saa 9 zilizopita ,
Ni saa tisa za usiku katika eneo la Fungurefu, lililopo Shehia ya Mtowapwani, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja lenye Wakaazi 3,503, Wanaume 2,041 Nawanawake 1462 kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022. Giza nene limetanda huku upepo mkali wa bahari ukivuma kwa kasi na kuongeza ukali wa baridi katika eneo hilo la pwani. Pembeni mwa ufukwe, kundi la wanawake na wasichana limekusanyika wakinong’ona maneno ya hapa na pale huku wakisubiri kwa hamu boti za wavuvi zirejee kutoka baharini zikiwa na mzigo wa dagaa.
Baadhi yao wamejifunika vitenge kujikinga na baridi kali ya usiku, huku wengine wakitumia mwanga hafifu wa tochi za simu zao kuangaza njia na kuendelea na shughuli zao katika mazingira yenye changamoto nyingi.
Kila mmoja anaonekana kuwa na haraka ya kuwahi mzigo wa dagaa kabla haujaisha. Katika mazingira hayo ya usiku, wanawake hao hulazimika kuvumilia uchovu, hofu na wakati mwingine vitendo vya udhalilishaji ili tu wapate kipato cha kuendesha maisha yao.
“Mtu usipowahi mapema hupati kazi. Tukichelewa tunarudi mikono mitupu,” anasema mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 19 aliyekubali kuzungumza na mwandishi kwa sharti la kutotajwa jina lake kwa kuhofia usalama wake.
Katika ukanda wa pwani wa Kaskazini Unguja, harufu ya dagaa waliokaushwa juani imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa wakazi wa Mangapwani na Fungurefu. Kila alfajiri wanawake na wasichana huonekana wakikimbilia madikoni wakiwa na ndoo, mabeseni na vifaa vya kuanikia dagaa kwa matumaini ya kupata kipato kidogo cha kusaidia familia zao.
Kwa nje shughuli hizi huonekana kuwa sehemu ya kawaida ya uchumi wa pwani, lakini nyuma ya pazia kuna simulizi nzito za unyonyaji wa kijinsia, matusi, mazingira magumu ya kazi na ukosefu wa ulinzi kwa wanawake na wasichana wanaojihusisha na biashara hiyo.

WAHANGA WAANIKA MASAIBU YAO
Baadhi ya wanawake na wasichana wanaofanya kazi ya kuanika na kubeba dagaa katika maeneo ya Mangapwani na Fungurefu wanasema matukio ya matusi na unyanyasaji wa kingono yamekuwa yakivunja utu wao na kuwafanya wajisikie kutokuwa salama katika mazingira yao ya kazi.
Halima Iddi Juma (si jina lake halisi), anasema Aprili 17, 2025 alifanyiwa udhalilishaji wa kimwili na mmoja wa wavuvi wakati akisubiri kupokea ndoo ya dagaa karibu na boti aina ya Ngwanda.
“Aliniingizia mkono sehemu za siri mbele ya watu. Nilihisi fedheha kubwa sana lakini sikuweza kuripoti kwa sababu ya aibu na hofu ya namna jamii ingenichukulia,” anasimulia kwa huzuni.
Mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 27 kutoka Mangapwani alisema baadhi ya mabaharia hutumia lugha za matusi na vitisho dhidi ya wanawake wanaokataa mahusiano ya kingono.
“Ukikataa wanakwambia hutapata dagaa wa kununua au watakufukuza katika eneo la kazi. Wengine hutumia nafasi zao kututisha kwa sababu wanajua tunategemea kazi hii kwa maisha yetu,” alisema.

Katika maeneo hayo pia wapo wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 wanaoshiriki shughuli ndogo ndogo za kuanika na kuchambua dagaa. Baadhi yao wanasema hukumbana na vitendo vya kushikwa isivyofaa na kutukanwa mara kwa mara, lakini huendelea kuvumilia kutokana na hali ngumu za kiuchumi na ukosefu wa ajira mbadala.
Nachia (si jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 16, anasema baada ya kuanza kazi alipokelewa vizuri, lakini hali ilibadilika baada ya mwajiri wake kuanza kumtaka kufanya naye ngono.
“Nilifanya kazi kwa wiki tatu tu. Baadaye mwajiri wangu alianza kunitaka kufanya ngono. Nilipomkatalia aliniambia niondoke au hatanilipa mshahara wangu. Nililia na kuwapigia simu watu wa nyumbani. Mwishowe alinilipa na nikatafuta kazi kwa mwajiri mwingine,” alisema.

Uchunguzi wa mwandishi umebaini kuwa wanawake wengi wanaofanya kazi katika madiko ya Mangapwani na Fungurefu hawana mikataba rasmi ya ajira wala mifumo madhubuti ya ulinzi wa haki zao, jambo linalowafanya kuwa katika mazingira yanayoweza kuchochea unyanyasaji na ukosefu wa haki.
“Tunafanya kazi kwa hofu kila siku lakini hatuna njia nyingine ya kujipatia kipato. Hii ndiyo kazi inayotusaidia kuhudumia familia zetu,” alisema mmoja wa wanawake aliyekutwa akianika dagaa katika eneo la Fungurefu.
Kwa upande wao, baadhi ya mabaharia, wanunuzi wa dagaa na viongozi wa madiko waliokubali kuzungumza na mwandishi walikiri kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na baadhi ya watu katika maeneo hayo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika na kuimarishwa kwa mifumo ya kuripoti matukio hayo.
Nahodha wa boti, Ibrahim Haji, alisema kuwa wanawake wanaofanya kazi za kuanika na kusindika dagaa wanapaswa kuheshimiwa na kulindwa dhidi ya aina yoyote ya unyanyasaji.
“Sisi tunafanya kazi pamoja kila siku na wanawake hawa. Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha wanapata mazingira salama ya kufanya kazi. Wale wanaowadhalilisha wanapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Ibrahim Haji.
Naye baharia wa boti, Juma Haji Jecha, alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya nafasi zao kwa kuwafanyia wanawake vitendo vya matusi na unyanyasaji jambo ambalo linapaswa kukemewa na jamii nzima.
“Wanawake ni sehemu muhimu ya shughuli za dagaa. Hatupaswi kuwanyanyasa wala kuwavunjia heshima. Tunahitaji kushirikiana kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa kabisa,” alisema Juma Haji Jecha.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa dagaa Ibrahim Sheha, maarufu kama Kima, alisema kuwa usalama wa wanawake katika maeneo ya kazi ni muhimu kwa maendeleo ya biashara na ustawi wa jamii.
“Wanawake wana mchango mkubwa katika biashara ya dagaa. Wanahitaji kufanya kazi katika mazingira yenye heshima, usalama na haki bila kuogopa matusi, vitisho au unyanyasaji wa aina yoyote,” alisema Kima.

VIONGOZI WA MADIKO WAANIKA UKWELI WA MATUKIO
Wasimamizi wa madiko ya Mangapwani na Fungurefu wanasema matukio ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na wasichana yamekuwa yakiongezeka katika maeneo hayo, hasa wakati wa usiku ambapo shughuli za upakuaji wa dagaa na uchukuaji hufanyika kwa wingi.
Kwa mujibu wa viongozi hao, katika mwaka 2025 madiko ya mangapwani na fungurefu yamenakili kesi 827 sawa na aslilimia 100% ambapo kwa Mangapwani yamenakili jumla ya kesi 240 zinazohusisha wanawake na wasichana sawa na asilimia 29.0 % ambapo kesi 80 ni za shambulio la matusi sawa sawa na asilimia 33.3 %. huku kesi 160 zikihusiana na unyanyasaji wa kingono sawa na asilimia 66.7.
Katika eneo la Fungurefu, jumla ya kesi 587 sawa na asilimia 71.0 % zimeripotiwa, ambapo kesi 230 ni za shambulio la matusi , sawa na asilimia 39.2 % na kesi 357 ni za unyanyasaji wa kingono sawa na asilimia 60.8. %

Aliy Abrahmani Khamisi, ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa diko la Fungurefu, amesema baadhi ya mabaharia, mapapasi na wafanyabiashara wenye uwezo wa kununua dagaa wanatajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa katika vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto wanaojishughulisha na shughuli za uanikaji na biashara ya dagaa.
“Matukio mengi hufanywa na baadhi ya mabaharia, mapapasi pamoja na watu wenye uwezo wa kununua dagaa. Wanawake wengi wanategemea kazi hii kwa ajili ya kujipatia kipato na kuendesha maisha yao, hivyo mara nyingi hushindwa kujitetea wanapokumbana na vitendo hivyo,” alisema Khamisi.
Kwa upande wake, Nahodha Haji Meja, kiongozi wa diko la Mangapwani, amesema licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya matukio ya udhalilishaji, bado kesi nyingi hazifiki katika vyombo vya sheria kutokana na waathirika kuogopa aibu, vitisho au kupoteza fursa za kujipatia kipato.
“Wapo wanawake wanaonyamaza kwa sababu wanaamini wakiripoti wataonekana wasumbufu na hatimaye kunyimwa nafasi za kufanya kazi katika eneo hili,” alisema Meja.
Kwa pamoja, viongozi hao wamezitaka mamlaka husika, wadau wa haki za wanawake na jamii kwa ujumla kuongeza juhudi za kutoa elimu kuhusu haki za binadamu, kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa za matukio ya ukatili na kuhakikisha wahusika wa vitendo vya udhalilishaji wanachukuliwa hatua za kisheria ili kulinda usalama na ustawi wa wanawake na watoto wanaofanya kazi katika sekta ya dagaa.
| Eneo | Jumla ya Kesi | % ya Kesi Zote |
| Mangapwani | 240 | 29.0% |
| Fungurefu | 587 | 71.0% |
| Jumla | 827 | 100% |

RIPOTI ZA OCGS ZINASEMAJE?
Kwa mujibu wa takuwimu za Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Takwimu Zanzibar (OCGS ya mwaka 2025, jumla ya matukio 1,228 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa Zanzibar, huku waathirika wakifikia 1,230. Kati ya waathirika hao, watoto walikuwa 1,050 sawa na asilimia 85.4, wanawake 162 sawa na asilimia 13.2 na wanaume 18 sawa na asilimia 1.5. Hali hii inaonesha kuwa wanawake na watoto wa kike wanaendelea kuwa miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa makosa ya kubaka yaliongoza kwa kuripotiwa mara 660, yakifuatiwa na matukio ya shambulio la aibu na kukashifu 166, kutorosha 146 pamoja na kulawiti au kunajisi 95. Takwimu hizi zinaashiria kuendelea kuwepo kwa changamoto kubwa za usalama wa wanawake na watoto katika jamii pamoja na mazingira mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, matukio mengi ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yalitokea nyumbani kwa mtuhumiwa ambapo yalifikia matukio 574 sawa na asilimia 46.7 ya matukio yote yaliyoripotiwa. Majumba mabovu yalifuatia kwa matukio 164 sawa na asilimia 13.4. Hali hii inaonesha kuwa maeneo yenye uangalizi mdogo yanaendelea kuwa sehemu hatarishi kwa wanawake na watoto.
Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, ripoti imeonesha kuwepo kwa matukio mbalimbali ya udhalilishaji wa kijinsia katika wilaya za Kaskazini A na Kaskazini B, jambo linalodhihirisha kuwa changamoto hiyo bado ipo katika jamii za mkoa huo na inahitaji juhudi za pamoja za kuzuia na kukabiliana nayo.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa matukio 540 sawa na asilimia 44.0 bado yalikuwa chini ya upelelezi wa Jeshi la Polisi mwishoni mwa mwaka 2025, huku matukio 396 sawa na asilimia 32.2 yakiwa mahakamani. Hali hii inaashiria umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa, uchunguzi na upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kutoka Dawati la Jinsia la wanawake na Watoto Mkoa wa Kaskazini Unguja lenye makao yake Mahonda, baadhi ya matukio ya udhalilishaji yanayotokea katika maeneo ya Mangapwani na Fungurefu yamekuwa yakiripotiwa lakini sio rasmi, ingawa idadi kubwa ya waathirika bado hawajitokezi kutoa taarifa na ushahidi kwa vyombo husika.

Akizungumza na Sakaza Digital Blog Afisa Wa Dawati La Jinsia La Wanawake Na Watoto Mkoa Wa Kaskazini Unguja Chum Makame Hemed amesema kwasasa hawana takuwimu kamili juu ya matokeo yanayotokea kutokana baadhi ya wahanga kutokua na mwamko wa kuripoti taarifa hizo .
Ameweka bayana kua wanawake na wasichana ndio wanaoongoza kuathirika na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia katika maeneo hayo, hali inayohitaji hatua za haraka za kuwakinga ili kuhakikisha usalama wao wanapotekeleza shughuli za kujitafutia kipato.
Aidha, Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kaskazini Unguja limewataka wananchi wa Mangapwani na Fungurefu kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema pindi wanaposhuhudia au kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, ili kurahisisha uchunguzi na kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

Afisa Programu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA Zanzibar), Asia Hakim, amesema wanawake wanaofanya kazi katika maeneo ya mwambao, ikiwemo shughuli za uvuvi na uanikaji wa dagaa, wanahitaji ulinzi maalumu kutokana na mazingira wanayofanyia kazi kuwa na vihatarishi vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Akizungumza kupitia Mradi wa “Tunaweza Pamoja”, unaotekelezwa na UN Women kwa kushirikiana na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa unaolenga kujenga jamii salama, yenye usawa na isiyovumilia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, Asia alisema bado kuna changamoto ya wanawake kukosa mifumo salama ya kuripoti matukio ya ukatili.
“Wanawake hawa mara nyingi hukosa sehemu salama za kutoa malalamiko na wengi wao hufanya kazi katika mazingira yenye uangalizi mdogo, jambo linalowaweka katika hatari ya kukumbana na vitendo vya udhalilishaji,” alisema Asia.
Aidha, amezitaka taasisi za serikali, viongozi wa jamii, waajiri pamoja na wadau wa sekta ya uvuvi kushirikiana kuweka mazingira salama ya kazi kwa wanawake, kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu haki za wanawake na kuhakikisha waathirika wa ukatili wanapata msaada wa kisheria na kisaikolojia kwa wakati.

Kwa upande mwingine, baadhi ya taasisi zinazojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto ikiwemo JUVIEKA na ZAFELA, zimependekeza kuwepo kwa mifumo rasmi ya kupokea na kufuatilia malalamiko ya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya madiko, kuongezwa kwa kampeni za elimu ya haki za wanawake pamoja na kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo ya kazi hususan nyakati za usiku.
Taasisi hizo zinasema hatua hizo zinaweza kusaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji na kuwapa wanawake na wasichana nafasi ya kufanya kazi katika mazingira salama, yenye heshima na yanayolinda haki zao za msingi.
Mamlaka za Serikali kuptia Afisa Wa Ustawi Wa Jamii Wilaya Ya Kaskazini ‘B’ Fatma Adam Issa anakiri kuwepo changamoto hizo za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake nawatoto katika maeneo ya Mangapwani na Fungurefu jambo ambalo linarejesha nyuma ustawi wao na jamii kwa ujumla
Bii Fatma ameweka bayana kua wanawake wengi wanaofanya kazi za kuanika dagaa hutoka katika familia zenye kipato cha chini, jambo linalowafanya kushindwa kupinga vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa kutokana na ugumu wamaisha lakini huchukuajuhudi za makusudi kutoa elimu ya kujitambua katika maeneo hayo .

“Wanawake hawa wanahitaji kusaidiwa kiuchumi na kupewa elimu ya namna ya kujilinda pamoja na kuripoti vitendo vya ukatili,” alisema.
Ameongeza kua baadhi ya waathirika hupata madhara ya kisaikolojia yanayoathiri afya zao pamoja na mahusiano yao ya kijamii
“Ukatili wa kijinsia hauishii kwenye maumivu ya mwili pekee, unaacha athari kubwa za kiakili na kihisia, naiwaombe wazazi na walezi kutowaruhusu Watoto wao Kwenda katika maeneo hayo kwani ni wadogo sana” aliongeza.

Hali hiyo inaashiria kuwa licha ya mchango mkubwa wa wanawake katika kukuza uchumi wa bahari, bado wanakabiliwa na changamoto za usalama na ulinzi wa haki zao wakiwa maeneo ya kazi.
Vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vinavyoripotiwa katika maeneo ya Mangapwani na Fungurefu vinakinzana na matakwa ya sheria za Zanzibar na Tanzania zinazolinda haki za wanawake na watoto. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 zinatambua haki ya kila mtu kuishi kwa heshima, usawa na bila kubaguliwa. Aidha, Sheria ya Adhabu Na. 6 ya mwaka 2018 imeweka adhabu kali kwa makosa yanayohusiana na ubakaji, kulawiti, unyanyasaji wa kingono na vitendo vingine vinavyokiuka maadili ya jamii.
Vilevile, Sheria ya Mtoto Na. 6 ya mwaka 2011 ya Zanzibar inamtaka kila mtu kumlinda mtoto dhidi ya aina zote za ukatili, unyanyasaji, udhalilishaji na matumizi mabaya.
Hata hivyo, ushahidi uliokusanywa katika uchunguzi huu unaonesha kuwa licha ya kuwepo kwa sheria hizo, wanawake na wasichana wanaofanya kazi katika maeneo ya mwambao bado wanakumbana na vitendo vya matusi, vitisho na unyanyasaji wa kingono vinavyohatarisha usalama wao na kuvunja haki zao za msingi
Je, haya ya tadumu mpaka lini?Wakati dagaa wanaendelea kuwa chanzo cha kipato kwa mamia ya familia za pwani, wanawake wengi wanaolinda uchumi huo wanaendelea kubeba maumivu kimya kimya wakisubiri siku ambayo sauti zao zitasikika na haki zao kulindwa.
