LAZIMA SERIKALI IONGEZE USHIRIKISHWAJI WENYE TIJA KWA VIJANA ZANZIBAR

Na Abdul Sakaza, Unguja

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetakiwa kuweka mazingira bora yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika masuala ya demokrasia, utawala bora na uongozi ili waweze kuchangia maendeleo ya taifa.

Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Programu kutoka Pamoja Youth Initiative, Daudi Kasim, wakati wa kongamano la vijana na wadau mbalimbali lililofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kijangwani (Kariakoo) Mjini Unguja.

Daudi alisema kuwa ingawa vijana wamekuwa wakishirikishwa katika baadhi ya shughuli za maendeleo, bado ushiriki wao katika nafasi za maamuzi ni mdogo na hauendani na idadi yao katika jamii.

“Uhalisia unaonesha vijana wanashirikishwa, lakini bado kuna mwanya mkubwa unaoonyesha kuwa ushiriki wao katika maamuzi muhimu si wa kiwango kinachohitajika,” alisema Daudi.

Alieleza kuwa uwakilishi wa vijana wenye umri wa chini ya miaka 35 katika nafasi za maamuzi bado ni mdogo, hali inayohitaji kuwepo kwa mfumo au kanuni maalumu itakayohakikisha vijana wanapata nafasi zaidi za kushiriki katika uongozi na kufanya maamuzi.

Aidha, washiriki wa kongamano hilo wamewataka viongozi wa kisiasa pamoja na mamlaka mbalimbali kuacha kuwatumia vijana kwa maslahi ya muda mfupi na badala yake kuwapatia fursa zinazowajengea uwezo na kuwainua kiuchumi na kijamii.

.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mbaruku Maalum kutoka JUVIEKA alisema vijana wengi wamekuwa wakitumika zaidi wakati wa shughuli za kisiasa lakini baadaye wanasahaulika.

“Vijana wengi hutumiwa kwa makusudi hasa katika vipindi vya siasa, lakini baada ya hapo hudharauliwa na kuwekwa kando. Tunahitaji kuona vijana wakishirikishwa katika maamuzi yanayogusa maisha yao na mustakabali wa taifa,” alisema.

Aliongeza kuwa ipo haja ya kuwepo kwa mikakati thabiti itakayowapa vijana nafasi ya kushiriki katika kupanga na kuamua mustakabali wa nchi pamoja na maendeleo ya jamii wanazoishi.

Kongamano hilo la siku moja lililoandaliwa na Pamoja Youth Initiative liliwakutanisha vijana na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili nafasi ya vijana katika demokrasia, utawala bora na uongozi, huku washiriki wakisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wao katika ngazi zote za maamuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *