Na Abdul Sazaka
Imeboreshwa saa 3 zilizopita
Wakati umma wa Kiislamu visiwani Zanzibar ukijiandaa kwa sherehe za Eid El-Fitri, ambayo huambatana na furaha, mikusanyiko ya kijamii na shughuli mbalimbali za kifamilia, kumekuwa na wito kwa jamii kuchukua tahadhari zaidi ili kuhakikisha usalama wa watoto unalindwa ipasavyo, kufuatia kuongezeka kwa matukio ya udhalilishaji hasa katika kipindi cha sikukuu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Machi 19, 2026, TAMWA-ZNZ imeeleza wazi kuwa “kipindi cha sikukuu huambatana na mikusanyiko na shughuli mbalimbali za kijamii ambazo bila uangalizi wa karibu, zinaweza kuwaweka watoto katika hatari ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.” Kauli hii inaakisi hali halisi inayojitokeza katika jamii ambapo furaha ya sikukuu huambatana na changamoto za usalama, hasa kwa watoto.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa karibu kila mwaka wakati wa sherehe za Eid El-Fitri au Eid El-Adh-ha, huripotiwa matukio mbalimbali ya udhalilishaji dhidi ya watoto katika maeneo tofauti ya Zanzibar. Matukio hayo yanajumuisha “kupotea kwa watoto, kubakwa, kulawitiwa, kutoroshwa na matukio ya mengine ya aina hiyo,” hali ambayo imeendelea kuleta hofu kwa wazazi na walezi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwezi Januari 2026 ulirekodi jumla ya matukio 113 ya udhalilishaji, ambapo matukio 91 sawa na asilimia 80.5 yalihusisha watoto. Ikilinganishwa na Januari 2025 ambapo matukio 103 yaliripotiwa na 87 kati yake (asilimia 84.5) yalihusisha watoto, inaonekana kuwa tatizo hili linaendelea kuwepo kwa kiwango kikubwa licha ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa.
TAMWA-ZNZ imefafanua kuwa takwimu hizi “zinaashiria kuwa vitendo vya udhalilishaji vimeshamiri na kutokana na uzoefu wa miaka ya nyuma huongezeka zaidi wakati huu wa sikukuu kutokana na watoto kuachiwa kutembea huru kwa wakati mrefu nje na ndani ya viwanja vya kusherehekea.”
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimesisitiza kuwa ni jukumu la pamoja kuhakikisha watoto wanalindwa ipasavyo. Katika kusisitiza hilo, TAMWA-ZNZ imesema “ni jukumu la pamoja kuhakikisha watoto hawatoki peke yao kwenda sikukuuni, hivyo wazazi na walezi wanahimizwa kuwasimamia watoto wao kwa karibu, kuongozana nao na kuhakikisha wanawarejea nyumbani salama.”
Aidha, chama hicho kimeonya juu ya tabia ya kuwaachia watoto jukumu la kuwasimamia wenzao, kikieleza kuwa “ni muhimu kuepuka kuwapa watoto jukumu la kuwasimamia au kuwaongoza watoto wenzao, kwani nao bado wanahitaji uangalizi na ulinzi wa watu wazima.” Hii inaonyesha wazi kuwa watoto hawawezi kubeba jukumu la ulinzi kwa wenzao bila msaada wa watu wazima.
Katika kuimarisha juhudi za ulinzi, TAMWA-ZNZ imeitaka jamii kuwa makini katika kufuatilia mienendo isiyo ya kawaida na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika na imeliomba Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika kipindi chote cha sikukuu.
Chama hicho pia kimehimiza wazazi kuzungumza na watoto wao kuhusu masuala ya usalama, kikieleza kuwa “TAMWA – Zanzibar inatoa wito kwa wazazi kuzungumza na watoto wao kuhusu usalama wao, kuwajengea ujasiri wa kuripoti matukio yoyote ya vitisho au unyanyasaji, na kuhakikisha wanakuwa katika uangalizi wa watu wanaoaminika wakati wote.”
Maoni ya Wazazi na Walezi
Baadhi ya wazazi na walezi wameunga mkono wito huo wa TAMWA-ZNZ, wakieleza kuwa ni muhimu kwa kila mzazi kuwajibika kikamilifu katika kulinda watoto wake wakati wa sikukuu.
Bi. Zainab Suleiman, mkazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema kuwa anazingatia sana ushauri wa wataalamu kuhusu ulinzi wa watoto.
“Kweli kabisa kama TAMWA walivyosema, ‘watoto hawatakiwi kutoka peke yao kwenda sikukuni’. Mimi huhakikisha naandamana nao kila wanapotaka kwenda sehemu za sherehe,” alisema.
Naye Bi. Asha Mohammed kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi alisisitiza umuhimu wa kuwapa watoto elimu ya kujilinda.
“Hili la ‘kuwajengea ujasiri wa kuripoti matukio yoyote ya vitisho au unyanyasaji’ ni muhimu sana. Watoto wakielimishwa wanakuwa na uwezo wa kujilinda,” alieleza.
Kwa upande wake Bi. Halima Juma wa Wilaya ya Kati alisema jamii inapaswa kushirikiana kwa karibu.
“Ni kweli kabisa kuwa ‘mhalifu hatoki mbali’. Wakati mwingine ni watu tunaowaamini, hivyo lazima tuwe macho,” alisisitiza.
Kwa upande wa wanaume, Bw. Salum Ali kutoka Mkoa wa Kusini Unguja alisema kuwa jukumu la kulinda watoto si la wanawake pekee.
“Sisi wanaume pia tuna wajibu mkubwa. Kama TAMWA walivyosema, huu ni ‘wajibu wa pamoja’, hivyo hatupaswi kuwaacha akina mama pekee wabebe jukumu hili,” alisema.
