NA FAUZIA MUSSA
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Mkadam Khamis Mkadam, amewataka watumiaji wote wa barabara kuongeza umakini na kuzingatia sheria za usalama barabarani hasa katika kipindi hiki kinachoelekea sikukuu ya Idd El-Fitr, ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
Wito huo aliutoa alipokuwa akitoa nasaha kwa waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria futari iliyoandaliwa na kampuni ya Amani Central Agency iliyofanyika Fuoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mkadam alisema kuwa mara nyingi kipindi cha kuelekea sikukuu hushuhudiwa ongezeko la ajali za barabarani kutokana na kuongezeka kwa safari za wananchi wanaokwenda na kurudi katika maeneo mbalimbali kutafuta mahitaji na kusherehekea siku hiyo.“Barabara zetu zimekuwa na hatari zaidi hasa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu, ambapo watu wengi husafiri kwenda na kurudi katika maeneo tofauti. Ni muhimu kila mtumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama ili kulinda maisha,” alisema Mkadam.
Alifahamisha kuwa uzembe wa madereva pamoja na kutotii kanuni za usalama barabarani ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia ajali nyingi zinazotokea nchini.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya barabara na kupunguza ajali zinazochukua maisha ya watu na kuwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.“Madereva wengi hasa wa bodaboda hawana leseni halali za udereva. Tunawasihi wajifunze udereva rasmi na kufuata taratibu zote ikiwemo kujiunga na kampuni za bima, kwani hatua hizo husaidia kuongeza usalama barabarani,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Amani Central Agency, Juma Awadhi Khatib, alisema kuwa lengo la kuandaa futari hiyo ni kuimarisha mshikamano, upendo na ushirikiano miongoni mwa wananchi pamoja na wadau mbalimbali katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.“Tumekutana hapa leo si tu kwa ajili ya kufutari pamoja, bali pia kuendeleza mshikamano na kujenga mahusiano mema katika jamii yetu,” alisema Khatib.
Aidha aliwashukuru viongozi wa nchi kwa kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano ambao unaiwezesha jamii kufanya shughuli zake kwa utulivu.
Naye Maulid Mohammed, akitoa shukrani kwa niaba ya uongozi wa Amani Central Agency, aliwashukuru wageni wote waliohudhuria futari hiyo na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa makini wanapotumia barabara hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu.“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunatumia barabara kwa uangalifu ili kulinda maisha yetu na ya wengine,” alisema.
