Na mwandishi wetu
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesisitiza umuhimu wa kusimamia na kuimarisha ustawi wa jamii ili kujenga taifa lenye mshikamano, usawa na maendeleo endelevu kwa wananchi wake.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Ziwani Polisi, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame, alisema sekta hiyo ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii, hivyo kunahitaji usimamizi madhubuti.
Alieleza kuwa kazi ya ustawi wa jamii ni wito unaohitaji moyo wa kujitolea, uvumilivu na huruma kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia wananchi kwa ufanisi.

Waziri Makame alibainisha kuwa licha ya jitihada zinazofanywa, bado jamii inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo udhalilishaji, kutelekezwa kwa familia na mmomonyoko wa maadili.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuitaka jamii kubadili mienendo hasi na kushirikiana katika kulinda haki za watoto na makundi mengine yenye uhitaji maalum.
Mbali na hayo alisema tabia ya kutelekeza watoto husababisha madhara makubwa kwa maisha yao na kuathiri mustakabali wa taifa.
Alifafanua kuwa ustawi wa jamii ukisimamiwa vyema huchangia kujenga jamii yenye maadili, mshikamano na maendeleo.
Akizungumzia unyanyapaa, Waziri huyo alisema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kabisa hapa nchini.

Mbali na hayo Waziri huyo alipendekeza kuanzishwa kwa wiki maalum ya ustawi wa jamii ili kuwapa wananchi nafasi ya kueleza changamoto zao na kupata ufumbuzi kwa urahisi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Zawadi Amour Nassor, alisema serikali imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za kijamii.
Alieleza kuwa miundombinu ya huduma imeimarishwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Aidha, alisema serikali inaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo ili kuwainua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Hata hivyo alisema mipango maalum imewekwa kwa ajili ya kuwahudumia wazee na watoto ili kuhakikisha wanapata ulinzi na malezi stahiki.
Naibu huyo alisisitiza umuhimu wa jamii kuacha kutelekeza watoto na wazee pamoja na kuondokana na imani potofu zinazochochea unyanyapaa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdulla, alisema maofisa ustawi wa jamii wana jukumu kubwa linalohitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wananchi.
Akisoma risala ya maofisa ustawi wa jamii, Time Mkadam Kombo alieleza kuwa changamoto kuu ni ukosefu wa sera na sheria maalum pamoja na miundombinu duni, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta hiyo kwa maendeleo ya jamii.

Maadhimisho ya siku ya ustawi wa jamii duniani hufanyika kila mwaka jumanne ya tatu ya mwezi machi, yakiwa na kaulimbiu yam waka huu isemayo “kushirikiana kwa ajili ya mustakabali wa pamoja”.
