RC . MATTAR ATOA WITO WA AMANI NA AJIRA KWA VIJANA KASKAZINI UNGUJA

Na Abdul Sakaza .

Mkoa Wa Kaskazini Unguja.

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mattar Zahor Masoud, amewataka vijana wa mkoa huo kuchagua viongozi bora katika uchaguzi mkuu ujao huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Akizungumza katika kongamano la vijana lililofanyika Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, aliwataka vijana kuwa mabalozi wa amani na kukemea vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.

“Amani ya nchi yetu ipo mikononi mwa vijana,Tuendelee kuwa walinzi wa amani kwa kutoa taarifa pale tunapobaini dalili za vurugu. Uchaguzi ni haki yetu, lakini ni lazima tufanye hivyo kwa utulivu na busara,” alisema Mattar.

Aidha, alieleza kuwa serikali ya mkoa inatambua changamoto ya ajira, hasa katika sekta ya utalii, na kwamba ofisi yake imeandaa mikakati ya kuhakikisha vijana wananufaika na fursa zilizopo katika sekta hiyo akisisitiza kuwa ajira za mahoteli haziendani na uvunjaji wa mila na silka za Mzanzibari kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, aliwahimiza vijana kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi na kutumia mabaraza ya vijana kama njia ya kujenga sauti ya pamoja yenye nguvu ya ushawishi.

Naye Mkurugenzi wa Jumuiya ya Vijana na Elimu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ (JUVIEKA), Mbarouk Maalum Mohammed, alitoa shukrani kwa uongozi wa mkoa, shirika la ActionAid, na washirika wengine kwa kufanikisha kongamano hilo na kuwezesha jukwaa la majadiliano kwa mustakabali wa vijana.

Washiriki wa kongamano hilo walipongeza JUVIEKA kwa kuwezesha majadiliano ya kina kuhusu masuala ya vijana, wakisisitiza haja ya jamii kuondokana na mtazamo hasi kuhusu ajira katika mahoteli.

Walisema kazi hizo ni halali, zenye heshima, na zinaweza kufanywa kwa kuzingatia maadili ya Kizanzibari.

Kongamano hilo lililowashirikisha vijana zaidi ya 100 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja wakiwakilisha mabaraza ya vijana, taasisi, na mashirika mbalimbali limeandaliwa na shirika la ActionAid kwa kushirikiana na Taasisi ya JUVIEKA.

Mada ya Ushiriki wa Vijana kwenye Uchaguzi na Kudumisha Amani pamoja na Changamoto za Wanawake na Vijana katika Sekta ya Utalii ziliwasilishwa na kujadiliwa katika kongamano hilo lililobeba ujumbe “Vijana Tunaweza – Tutashiriki Kuchagua na Kuchaguliwa.” mabaraza ya vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *