KWANINI WIZI UMESABABISHA UMASIKINI CHAANI MCHEZA SHAURI NA CHANI MASINGINI

Na Juma Haji ,Abdul Sakaza,

Wakiripoti kutoka chaani kaskazini unguja .

Imeboreshwa saa 4 zilizopita

Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, sekta ya kilimo chaani  ndio chanzo kikuu cha uchumi wa maisha yao, Shehia ya Chaani Masingini ina wakazi takribani 5,143 (wanaume 2,499 na wanawake 2,644) huku shehia ya Mchenza Shauri ikiwa na wakazi 1,025 (wanaume 506 na wanawake 519).

Licha ya jitihada za wakulima na jamii kwa ujumla kuboresha uzalishaji wa mazao kama ndizi, nazi, kundi la mifugo na mazao ya mbogamboga, matukio ya wizi wa mazao yamekuwa yakiongezeka kwa kasi katika shehia hizi, na kuibua hofu, hasara ya kiuchumi na changamoto za kijamii. Wakazi na wakulima wa maeneo haya wanasema wizi unaendelea bila vikwazo vya kutosha, huku baadhi ya wahalifu wakifanya matukio yao bila hofu, jambo ambalo limevuruga shughuli za kilimo na kujenga mazingira ya hofu miongoni mwa wakulima na familia zao.

Katika mazingira haya, wakulima wengi wanaonyesha msongo wa mawazo na kuchanganyikiwa kwani wanapoteza mazao ambayo ni chanzo  kuu cha chakula na kipato jambo linalozidisha mzunguko wa umaskini na tatizo la usalama wa mali zao.

Kuwepo kwa wizi  Unaathari Gani Kwa Wakulima Wa Chaani

Rashidi Kunguni (38 ) mkazi wa Chaani Mcheza Shauri, amesema wizi wa mazao umekuwa tatizo sugu ambalo linawaathiri wakulima na wanapata  hasara kubwa. “Mwizi anaiba bila hofu, na mara nyingi wanaotenda matendo si rahisi  kufikishwa katika vyombo vya sheria. Wakulima wanapoteza kazi za miezi na hata miaka ya maandalizi ya kilimo, na hatimaye wanakosa mapato ya familia,” alieleza kwa msisitizo.

Bi Asha Juma (56)  mkulima wa migomba kutoka  Chani Masingini, aliieleza hali ilivyo kwa wakazi wenzake akisema kuwa matukio ya wizi yamekuwa sugu kiasi kwamba wengi wanapoteza mazao yao ya msingi kabla ya kufika sokoni au kabla ya mavuno. “Hii ni changamoto kubwa sana kwetu. Tunategemea mazao haya kwa chakula cha familia na pia kuuza ili kupata mahitaji ya msingi, lakini sasa tunapoteza bila kujua hatima ya juhudi zetu,” alisema Bi Asha kwa huzuni.

Wakulima mbali mbali  katika shehia hizo pia wametoa mfano wa jinsi wizi unavyoathiri ustawi wa familia zao kwa kupoteza mazao yao wazi wazi ,Bi Fatuma Salim (58) anasema kuwa wakati mwingine analazimika kutafuta njia mbadala za biashara ndogo ili kufidia hasara zilizotokana na wizi wa mazao yake ya nazi na mboga. “Tunapoteza mali zetu kwa wizi na hatuna uhakika wa kupata fidia, jambo linalotuletea msongo wa mawazo na kutoridhika kwa wengi wetu,” alisisitiza Bi Fatuma.

Pamoja na hasara za moja kwa moja, wananchi wanasema wizi wa mazao umechochea hali ya hofu na kutokuwa na amani ndani ya jamii, jambo ambalo limechangia mgawanyo miongoni mwa wakazi na kuibua migogoro ya kijamii.

Kwanini Wizi Unajitokeza Katika Jamii Hii Ya Chaani

Kulingana na Mbunge wa  International Peace Information(IPI)  Taasisi ya Kimataifa ya Kuhamasisha Amani upande wa Zanzibar Suleiman Bakari Silima, amesema vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya jamii wameshawishika  kushiriki katika matukio ya wizi kwa sababu ya kutaka maitaji ya haraka ikiwemo kutafuta fedha kwaajili ya kununua madawa ya kulevya huku wengine wanafanya matukio hayo ya wizi ili kupata fedha ambazo zinawasaidia Kwenda katika kumbi za starehe “Vijana wengi wanaamini kwamba wizi ni njia ya haraka ya kupata fedha na mahitaji ya kila siku. Hii ni dhana potofu inayochangia ongezeko la matukio ya uhalifu katika shehia zetu,” alisema Suleiman

Kadhalika Maoni kutoka kwa wakazi wa vijijini yanaonyesha kwamba baadhi ya vijana hufanya uhalifu wa wizi wa mazao kwa nia ya kupata fedha kwa haraka, bila kufikiria athari kwa familia na jamii kwa ujumla.

 Hii inaonyesha taswira mbaya  ambapo wakulima wanapoteza matumaini ya kujenga maisha endelevu kupitia kilimo wanachokiona kama chaguo thabiti cha kujikwamua kiuchumi,Changamoto hii pia inaonesha umuhimu wa kuelewa mizizi ya matatizo ya kijamii yanayohusiana na ukosefu wa ajira, upungufu wa fursa za ujasiriamali kwa vijana na changamoto za kijamii zinazochangia uhalifu wa mazao.

Ukosefu Wa Ulizi Shirikishi Na Athari Zake Katika Jamii

Moja ya sababu kubwa inayochangia kuongezeka kwa wizi wa mazao katika shehia hizi ni ukosefu wa ulizi shirikishi wenye ufanisi katika kuzuia matukio ya wizi,Askari shehia walio na jukumu la kuongoza kamati za ulizi na doria mara nyingi hawashiriki kikamilifu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa rasilimali, mafunzo duni na upungufu wa ushirikiano na vyombo vya ulinzi rasmi.

Rashidi kunguni  ameeleza kuwa hali hii inazidisha kuendelea kwa wizi kwani wahalifu hufanya matukio yao bila hofu ya kuwakabiliwa na ulizi madhubuti. “Askari shehia wanastahili kuwa mbele ya doria na ulizi, lakini wakati mwingine hawapo katika vikao vya kupanga mikakati ya usalama kwa sababu ya ukosefu wa ushirikiano na vyombo vya ulinzi,” alisema kunguni .

Ukosefu wa doria, mikakati ya pamoja kati ya askari shehia na wananchi kumesababisha uhaba wa taarifa za mapema kuhusu matukio ya wizi, na hivyo kuwapa wahalifu nafasi ya kufanya uhalifu bila kukabiliwa na adhabu kali.

Mustafa Ahmada Ali Sheha wa Chaani Masingini amekiri kuwepo kwa matukio ya wizi kwenye shehia yake yanayofanywa na vijana  ambayo yanachochewa na utumiaji wa madawa ya kulevya jambo ambalo linaharubu haiba ya shehia yao .

Ameweka bayana kwasasa wameandaa mikakati ya kufufua kamati za ulishi shirikishi ili kudhibiti matukio kama hayo na kuwataka wanajamii kujiunga katika kamati hizo ili kukabiliana na matukio ya wizi katika jamii yao  “Tumekuwa tukifanya mikutano ya jamii, kutoa elimu juu ya madhara ya wizi na umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya ulinzi, lakini wanajmii ni wagumu kuhudhuria vikao  na hili linachangia kutofikia malengo yeyote ” alisema Mustafa.

Wakulima kama Ali Hassan kutoka Chaani Mcheza Shauri wameeleza kuwa wanataka ushirikiano mkubwa kati ya askari shehia na wananchi, wakisema kwamba ulizi unaoongozwa na jamii unaweza kuwa chombo chenye nguvu zaidi katika kukabiliana na wizi. “Tunahitaji uwepo wa askari shehia wenye uaminifu na waliopata mafunzo ya ulizi shirikishi ili kuongoza juhudi za usalama kwa ufanisi zaidi,” alisema Ali.

Maoni ya wakazi yanaonyesha matumaini kwamba kwa kushirikiana kikamilifu na vyombo vya ulinzi, kuweka doria shirikishi na kutoa elimu endelevu kwa vijana, matukio ya wizi yataanza kupungua. Bi Asha Juma alisema, “Tuna matumaini kwamba jamii na vyombo vya ulinzi vitashirikiana, na kwamba vijana wataelewa umuhimu wa kutumia nguvu zao kwa shughuli za maendeleo badala ya uhalifu.”

Ingawa wizi wa mazao unaendelea kuwa changamoto katika shehia za Chaani Mcheza Shauri na Chaani Masingini na kuathiri ustawi wa wakulima na jamii kwa ujumla, maoni ya wakazi na viongozi yanaonyesha kuwa kuna mwanga wa matumaini endapo itakuwepo ushirikiano imara kati ya jamii na askari shehia

Ushirikiano huu unaweza kuchochea sera za ulizi shirikishi, kutoa fursa za elimu na ajira kwa vijana, na kuimarisha amani na usalama wa mali katika maeneo haya,Hii ni hatua muhimu kuelekea kuendeleza kilimo na shughuli za kiuchumi kwa njia endelevu, na kusaidia wakulima kupata ustawi wa maisha bila hofu ya kupoteza mazao yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *