WANANCHI KASKAZINI UNGUJA WAPATA MATUMAINI MAPYA KWA RC GALLOS NYIMBO

Na Abdul Sakaza
Akiripoti kutoka Mkokotoni

Imeboreshwa saa 3 zilizopita /News Follow Up.

Uongozi wa umma ni dhamana inayotekelezwa kwa misingi ya uwajibikaji, uwazi na kuendeleza maendeleo endelevu. Ndani ya mfumo wa utawala wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, makabidhiano ya ofisi kwa viongozi wa umma ni utaratibu muhimu unaolenga kuhakikisha huduma kwa wananchi zinaendelea bila kuathiriwa na mabadiliko ya kiuongozi.

 Hali hiyo imeshuhudiwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kufuatia hafla ya makabidhiano ya ofisi kati ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Mattar Zahor Masoud, na Mkuu mpya wa Mkoa, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kaskazini unguja iliyopo  Mkokotoni

Kwanini viongozi hukabidhiana ofisi

Makabidhiano ya ofisi kwa viongozi wa umma yanalenga kudumisha misingi ya utawala bora, kulinda kumbukumbu za taasisi na kuhakikisha mipango ya maendeleo inaendelea bila kukwama, Aidha, mchakato huu humwezesha kiongozi mpya kufahamu hali halisi ya ofisi, mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na mikakati ya kuzikabili.

Katika hafla hiyo, viongozi walisisitiza kuwa maendeleo ya mkoa hayawezi kusimama kwa sababu ya mabadiliko ya mtu mmoja, bali ni jukumu la pamoja linalohusisha serikali, watendaji na wananchi.

RC Mpya Aahidi Ushirikiano na Uwajibikaji

Mara baada ya kukabidhiwa ofisi, Mkuu mpya wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo, aliwataka watendaji wa serikali pamoja na wadau mbalimbali kushirikiana naye kikamilifu ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Ushirikiano ni msingi wa maendeleo,” alisema Mhe. Nyimbo.

Alisisitiza kuwa amani, utulivu, mshikamano na uwajibikaji ni nguzo kuu zitakazosaidia kufanikisha mipango ya maendeleo ya mkoa huo na Taifa kwa ujumla, huku akisisitiza nidhamu na uadilifu katika utendaji kazi.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, amesema anaondoka mkoani humo akiwa na faraja kubwa baada ya kuacha mkoa ukiwa katika hali ya amani na utulivu.

Mhe. Mattar alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake yalitokana na ushirikiano mzuri kati ya serikali na wananchi, na kuwaomba watendaji pamoja na wananchi kuendelea kumpa ushirikiano Mkuu wa Mkoa mpya ili kasi ya maendeleo isiende ikapungua.

Aidha, alitoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuimarisha maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja na Zanzibar kwa ujumla.

Matumaini ya Wananchi wa Kaskazini Unguja

Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wameeleza matumaini makubwa kwa uongozi mpya wa Mhe. Cassian Gallos Nyimbo, wakiamini utaendeleza mafanikio yaliyopo na kufungua fursa mpya za kiuchumi.

Ali Mohamed (46), mkazi wa Mkokotoni, amesema ana matumaini makubwa na uongozi wa RC mpya, akisisitiza kuwa fursa zilizopo mkoani humo zinapaswa kutumiwa kwa matumizi chanya ili kuharakisha maendeleo.

Naye Asha Hamadi (38), mkazi wa Mwazo Mghumu, amesema Mkoa wa Kaskazini Unguja una fursa kubwa katika sekta za utalii, kilimo, uvuvi na michezo, ambazo endapo zitatumiwa ipasavyo zinaweza kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wao, Mohammedi Ibrahim (35) pamoja na Juma Makame (55) kutoka Tumbatu, wamewataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia watu wote.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Tanzania ya mwaka 2022, Mkoa wa Kaskazini Unguja una jumla ya wakazi 257,290, kati yao wanaume ni 126,341 na wanawake ni 130,949. Mkoa huo una jumla ya kaya 33,257, idadi inayoonesha uwepo wa nguvu kazi kubwa na soko pana la shughuli za kijamii na kiuchumi.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja umeendelea kukua kwa kasi, ambapo idadi ya watu imeongezeka kutoka 187,455 mwaka 2012 hadi 257,290 mwaka 2022, sawa na ongezeko la watu 69,835 ndani ya kipindi cha miaka kumi.

Ukuaji huo wa idadi ya watu unaipa mkoa nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya Zanzibar kupitia sekta mbalimbali ikiwemo utalii, kilimo, uvuvi, biashara na michezo, endapo rasilimali zilizopo zitatumika kwa mipango madhubuti na uongozi makini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *