NA FAUZIA MUSSA
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imewataka vijana nchini hususan wanawake kuchangamkia fursa za masomo katika fani za anga, ikiwemo uongozi wa ndege, ili kuongeza idadi ya wataalamu wazalendo na kuhakikisha usalama endelevu wa anga la Tanzania.
Wito huo umetolewa na Muongoza Ndege Mwandamizi wa TCAA, Omar Mohammed Haji, katika maadhimisho ya siku ya waongoza Ndege Duniani hafla iliofanyika katika Ofisi za Mamlaka hiyo kituo cha Zanzibar, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya anga, bado kuna upungufu wa wataalamu wa kada hiyo nchini, hasa wanawake, jambo linalotoa nafasi kwa vijana wa kike kujitokeza kwa wingi kuisomea taaluma hiyo muhimu.
“Nitoe wito kwa jamii kuwekeza katika elimu ya anga. Tunahitaji wataalamu wengi zaidi, hasa wanawake, ambao wanapewa kipaumbele katika nafasi za ajira endapo watakuwa na vigezo vinavyohitajika,” alisema
Aliongeza kuwa TCAA itaendelea kusimamia na kudhibiti anga la Tanzania kuhakikisha ndege zote zinapaa na kutua kwa usalama bila kugongana, wala kukutana na vizuizi vingine angani au ardhini.“Tunajitahidi kuhakikisha usalama wa anga unadumishwa kwa kufuatilia mienendo ya ndege, kutoa taarifa za hali ya hewa, na kushirikiana na taasisi nyingine katika utafutaji na uokozi endapo ajali itatokea,” alifafanua.
Kwa upande wake, Mohammed Ali Mohammed, Meneja wa Usafiri wa Anga Tanzania, kituo cha Abeid Amani Karume, alisema ongezeko la ndege na matumizi ya teknolojia mpya kama drone limeongeza changamoto katika usimamizi wa anga, hivyo elimu kwa watumiaji wa anga ni muimu zaidi.“Leo anga yetu ile ile ambayo haiongezeki inatumiwa na ndege nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita. Tumeshuhudia ongezeko maradufu la ndege za kibiashara, matumizi ya drone, ujenzi wa minara ya mawasiliano na majengo marefu. Yote haya yanahitaji usimamizi wa karibu ili kuepusha hatari kwa anga zetu” alisema Mohammed.

Aliongeza kuwa Mamlaka itaendelea kutoa mafunzo kwa waongoza ndege na wadau wengine wa anga ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake katika kulinda usalama wa anga na mazingira.“Ndege zinapozunguka angani kwa muda mrefu hutoa moshi unaochangia uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, tunahimiza matumizi bora ya teknolojia rafiki kwa mazingira,” aliongeza
Katika kuadhimisha siku hiyo, TCAA Zanzibar ilitoa elimu kwa wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Lumumba, kuwahamasisha kuingia katika taaluma ya uongozi wa ndege na masuala mengine ya anga.
Omar Mohammed Haji, ambaye pia ni mwanachama wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TATCA), alisema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kazi za waongoza ndege katika usalama wa safari za anga.“Tunahitaji vijana wenye dhamira ya kweli. Uongozi wa ndege ni taaluma yenye uwajibikaji mkubwa na mchango wake ni muhimu katika uchumi wa taifa, hasa katika kukuza sekta ya utalii na biashara,” alisisitiza.

Mmoja wa wanafunzi waliopata elimu hiyo, Sumaiya Abdul Chacha, mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika Skuli ya Sekondari Lumumba, alisema ametiwa moyo kuona wanawake nao wanapewa nafasi katika taaluma za anga.
“Sikuwahi kujua kwamba wanawake wanaweza kuwa waongoza ndege. Leo nimepata hamasa kubwa kusomea fani hii,” alisema
Maadhimisho ya siku ya waongoza ndege Duniani huadhimishwa kila mwaka Oktoba 20, yakilenga kutambua mchango wa wataalamu wa uongozi wa ndege katika kuhakikisha usalama wa safari za anga duniani ambapo huduma za uongozi wa ndege zilianza mwaka 1920 jijini London, na tangu mwaka 1961 dunia imekuwa ikiadhimisha siku hii kutambua mchango wa taaluma hiyo katika usalama wa safari za anga.
