MGONGOMBE WA ACT WAZALENDO KILOSA AAZIMIA KUBORESHA AFYA ZA WANANCHI.

Na Mwandishi wetu

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kilosa kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Hassan Mbaruku, ameahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha anasimamia ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika kata ambazo bado hazijafikiwa na huduma hizo muhimu wilayani Kilosa.

Ametoa kauli hiyo Oktoba 4, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya soko la mjini, Kata ya Mbumi, ambapo alisisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kwa ukaribu, jambo ambalo litapunguza gharama na muda wa kufuata huduma mbali.

Sambamba na hilo, Mbaruku ameahidi kuanzisha viwanja vya michezo katika kila kata ya jimbo hilo, akieleza kuwa michezo ni ajira kwa vijana na pia huimarisha afya. Aidha, ameeleza mpango wake wa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuanzisha maeneo maalumu ya kuzalisha nyasi endelevu kwa ajili ya mifugo.

Nae Naibu Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amewasihi wananchi wa Kilosa kuwachagua viongozi bora wenye maono ya kuleta maendeleo, akisema kiongozi bora ni yule anayeacha alama ya mafanikio katika jamii aliyoihudumia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *