NI LAZIMA HAKI ZA BINADAMU ZIHESHIMIWE, ZILINDWE NA KUTEKELEZWA KABLA, WAKATI NA BAADA YA UCHAGUZI.

NA FAUZIA MUSSA

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mwinyichande Khatib Mwinyichande, amesema Ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unakuwa huru, haki na wa amani, ni lazima haki za binadamu ziheshimiwe, zilindwe na kutekelezwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu haki za binadamu na wajibu wao wakati wa uchaguzi, yaliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Manispaa, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Kamishna Mwinyichande alisisitiza kuwa waandishi wana jukumu kubwa la kuhabarisha na kuelimisha jamii kwa weledi mkubwa wakati wote wa mchakato huo.”waandishi wa habari wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora, na kuepuka kusambaza taarifa za upotoshaji au zenye kuibua taharuki,” alisema Kamishna huyo.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuwa wao ni kiungo muhimu katika kueneza taarifa sahihi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa THBUB, Juma Msafiri Karibona, alisema tume hiyo imepanga kutoa elimu ya haki za binadamu kwa waandishi wa habari katika mikoa yote ya Zanzibar ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma. “Waandishi wa habari ni walinzi wa amani. Mafunzo haya yanalenga kuimarisha uwezo wao kuhakikisha taarifa wanazotoa hazikiuki haki za binadamu wala kuchochea migogoro,” alisema Karibona.

Tunu Myenda, Ofisa Uchunguzi kutoka THBUB – Tawi la Dar es Salaam, akiwasilisha mada kuhusu haki za kushiriki uchaguzi, alisema kila raia mwenye sifa ana haki ya kuchagua, kuchaguliwa na kushiriki uchaguzi bila vizuizi visivyo halali.”Wananchi wana haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu wagombea, vyama vyao na taratibu za uchaguzi. Waandishi wa habari wana wajibu wa kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia kwa usahihi,” alisema.

Aliongeza kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuonyesha usawa katika kuripoti shughuli za vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi, kuheshimu utu na usiri wa watu, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa makundi yote yenye sifa ya kupiga kura.”Wakikiuka maadili, waandishi wanaweza kusababisha taharuki, migogoro, uvunjifu wa amani na hata kuathiri uaminifu wao binafsi na wa vyombo vyao vya habari,” alionya Myenda.

Mbwana Mbwana, Mkurugenzi Msaidizi wa THBUB, alisema tume itaendelea kutoa elimu kwa wananchi, kufuatilia mwenendo wa uchaguzi na kufanya uchunguzi katika kila hatua kuhakikisha haki za binadamu hazikiukwi.”Tunaendelea kuangalia mwenendo wa kampeni kuhakikisha makundi yote, ikiwemo watu wenye ulemavu, yanashiriki ipasavyo,” alisisitiza.

Waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo waliishukuru THBUB kwa kuwawezesha kupata elimu hiyo muhimu na kuahidi kuwa mabalozi wa haki za binadamu katika kipindi chote cha uchaguzi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *