UMOJA WA MATAIFA KUJADILI SULUHISHO LA MATAIFA MAWILI KATIKA MZOZO WA ISRAEL NA PALESTINA

Ufaransa na Saudi Arabia zitaongoza mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujaribu kufufua matumaini ya suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Palestina

Nchi hizo mbili zina matumaini ya kuutumia mkutano huo maalum wa mwaka huu wa viongozi wa dunia kuzungumzia vita katika Ukanda wa Gaza kama njia ya kuonyesha uharaka wa jambo hilo, baada ya matumaini hayo kukwama kwa muda mrefu. 

Mkutano huo wa Jumatatu unafanyika mjini New York, Marekani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, katika wakati ambapo shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel likiongezeka kutokana na vita vya Gaza. Juhudi zinazofanywa na Ufaransa na Saudi Arabia ni pamoja na kuwepo mfumo mpya kwa taifa huru la Palestina kwenye maeneo ambayo Israel iliyanyakua katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967, na hatua ya nchi kadhaa za Magharibi kuungana katika kulitambua taifa huru la Palestina, kama njia pekee ya kuutatua mgogoro uliodumu kwa miongo mingi.

Nchi kadhaa kutangaza kuitambua Palestina kama taifa huru

Katika mkutano huo, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron anatarajiwa kutangaza hatua ya Ufaransa kuitambua rasmi Palestina kama taifa huru. Nchi nyingine kadhaa za Magharibi, ikiwemo Uingereza, Canada, Ubelgiji, Malta na Australia, zinatarajiwa pia kuchukua hatua hiyo, huku zikiungana na takribani nchi 150 ambazo tayari zimelitambua taifa huru la Palestina.

Hata hivyo, juhudi hizo tayari zinakabiliwa na vikwazo vikubwa kuanzia kwa Marekani na Israel. Marekani imewazuia maafisa wa Palestina kuhudhuria Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, baada ya kuwanyima visa. Aidha, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ametishia kuchukua hatua za upande mmoja katika kujibu hatua hiyo, ikiwemo uwezekano wa kunyakua sehemu za Ukingo wa Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Varsen Aghabekian Shahin amesema hatua ya nchi hizo kulitambua taifa huru la Palestina, inaleta karibu zaidi uhuru na mamlaka ya Wapalestina. ”Hili pia linapeleka ujumbe wa wazi wa matumaini kwa watu wa Palestina wanaokabiliwa na kitisho kilichopo. Siku zote Israeli inadai inakabiliwa na kitisho. Leo hii ni Wapalestina ndiyo wanakabiliwa na kitisho, na tunapaswa kupaza sauti zetu kuzungumzia kitishio hiki,” alifafanua Shahin.

Rais wa Palestina Mahmud Abbas ambaye hatohudhuria mkutano huo baada ya kunyimwa visa na Marekani, ameipongeza pia hatua hiyo, akisema ni ”muhimu katika kuelekea kupatikana kwa amani ya haki na ya kudumu”.

Uingereza kuelezea madhila wanayokumbana nayo raia wa Gaza

Wakati huo huo, Uingereza imesema itautumia Mkutano wa kilele wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kushinikiza kuungwa mkono kimataifa mfumo wa amani katika Mashariki ya Kati, kutokana na hatua yake ya kulitambua taifa la Palestina. Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer Jumapili alitangaza kuitambua Palestina kama dola huru, akisema alinuiwa kufufua matumaini ya amani kwa Wapalestina na Waisraeli.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper amesema atautumia mkutano huo kuelezea madhila wanayokumbana nayo raia wa Ukanda wa Gaza ulioharibiwa kwa vita, na kutafuta kuimarisha makubaliano ya kimataifa kuhusu njia ya amani katika Mashariki ya Kati.

(AFP, AP, DPA, Reuters)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *