KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 61 YA ELIMU BILA MALIPO YAFANYIKA ZANZIBAR

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa, amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu bila vikwazo vya kifedha kwa lengo la kuimarisha mfumo wa elimu bure nchini.

Akizungumza katika Ukumbi wa Polisi Ziwani wakati wa Kongamano la Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 61 ya Elimu Bila Malipo, Waziri Lela alisema siku hiyo ni ya kihistoria kwani inakumbusha hatua kubwa iliyoongozwa na Hayati Mzee Abeid Amani Karume mnamo tarehe 23 Septemba 1964 alipotangaza rasmi elimu bila malipo na kuondoa ubaguzi katika upatikanaji wa elimu.“Kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kulikuwa na shule chache mno na fursa ya kupata elimu ilikuwa ndogo. Kulikuwepo shule moja tu ya maandalizi yenye wanafunzi 60, shule 62 za msingi na shule tano za sekondari. Leo hii, tunashuhudia Mapinduzi makubwa ya kielimu,” alisema Waziri Lela.

Aliongeza kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha na hivyo ni jukumu la walimu pamoja na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanakwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya kielimu.

Waziri alifahamisha kuwa tangu Mapinduzi hadi sasa, Zanzibar imefanikiwa kujenga zaidi ya skuli 1,554 za maandalizi, msingi na sekondari, ikiwemo shule mpya za ghorofa katika kila wilaya.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 518 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule mpya za maandalizi, msingi na sekondari, ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora.

Waziri Lela pia ameitaka Wizara ya Elimu kuweka kozi za muda mfupi kwa walimu ili kuongeza ufanisi na uwezo wa kufundisha kwa kuendana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia.

Akizungumzia sekta ya michezo, Waziri Lela aliitaka Idara ya Michezo kusimamia mila, silka na desturi ili kuwajengea wazazi imani ya kuwaruhusu watoto kushiriki michezo, akisisitiza kuwa michezo ni sehemu ya elimu na maendeleo ya mtoto.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khamis Abdulla Said, alisema Serikali ipo katika mageuzi makubwa ya elimu yanayojumuisha sanaa na utamaduni, ikiwemo mpango wa kujenga academia za michezo Unguja na Pemba ili kukuza vipaji vya vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *