Mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Maalum ya Uchumi na Fedha Mkoa wa Kaskazini Unguja kupitia chama cha ACT Wazalendo, Haji Mwadini Makame, ametangaza rasmi kurejea katika Chama cha Wananchi (CUF), ambacho alikihama mwaka 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwadini alisema amefikia uamuzi huo kwa hiari yake binafsi bila kushinikizwa na mtu yeyote, akisisitiza kuwa amerudi nyumbani ili kushirikiana na wanachama wenzake kuimarisha chama na demokrasia nchini.“Hii ni haki yangu ya kisiasa. Mwanadamu anaweza kuingia katika chama anachokiamini na akiona dira yake haipo tena, ana uhuru wa kuhamia sehemu nyengine. Nimeamua kurejea CUF ili kushirikiana na viongozi na wanachama wenzangu kukirejesha kwenye hadhi yake ya zamani,” alisema Mwadini.
Alibainisha kuwa chama cha CUF bado kina nafasi kubwa ya kufanikisha mabadiliko ya kweli endapo wanachama na viongozi wake watashirikiana kwa dhati.
Haji Mwadini alianza safari yake ya kisiasa mwaka 1994 ndani ya CUF, ambapo alihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo Mjumbe wa Kamati ya Uongozi Jimbo la Nungwi na Katibu wa Vijana.
Mwaka 2010 aligombea nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Nungwi na kushinda kupitia CUF, ambapo pia aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati (2010–2015).
Baada ya hapo alihamia Jimbo la Kijini lakini uchaguzi ulifutwa Kutokana na migogoro ya kiuongozi ndani ya CUF mwaka 2017, Mwadini alijiunga na ACT Wazalendo ambapo aliendelea kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo Mjumbe wa Kamati ya Mkoa na Katibu wa Kamati Maalum ya Fedha na Uchumi, kabla ya kutangaza kurejea CUF mwaka huu.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZNZ.
