NA FAUZIA MUSSA
SERIKALI ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) imeeleza dhamira yake ya kutekeleza mikakati madhubuti kwa lengo la kuinua maendeleo ya chuo hicho na ustawi wa wanafunzi kwa ujumla.
Akizungumza na gazeti la Zanzibar leo katika Ofisi ya Serikali ya Wanafunzi iliyopo Tunguu, Wilaya ya Kati, Rais wa Serikali hiyo, Asia Ramadhan Khamis alisema kuwa mipango iliyowekwa inalenga kutoa mchango chanya katika sekta za elimu, maendeleo, uongozi na ushiriki wa kimataifa.”Serikali yetu imejipanga kwa mikakati imara itakayochangia kuwajengea wanafunzi uwezo wa kiujuzi na kuwaandaa kwa ushindani wa kitaifa na kimataifa,” alisema Asia.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuanzisha programu za semina, warsha na mijadala zitakazowawezesha wanafunzi kukuza ujuzi katika nyanja za uongozi, ujasiriamali, pamoja na matumizi ya Sayansi na Teknolojia.
Aidha, Serikali hiyo imejipanga kuanzisha miradi midogo ya kijamii na kiuchumi ndani ya skuli mbalimbali za SUZA, ikiwemo uanzishwaji wa klabu za ubunifu, ujasiriamali, michezo na sanaa Ili kuwawezesha wanafunzi kiuchumi, kijamii na kuwaandaa kwa maisha ya baada ya chuo.
Katika kuendeleza vipaji na kuimarisha jina la chuo, Asia alieleza kuwa wanaandaa utaratibu wa kushirikisha wanafunzi katika mashindano ya kitaaluma, michezo na ubunifu ndani na nje ya nchi, ili kuongeza fursa kwa vijana na kulikuza jina la SUZA kimataifa.

Serikali hiyo pia imedhamiria kuimarisha ushirikishwaji wa wanafunzi katika maamuzi kupitia vikao rasmi, majukwaa ya maoni na miradi ya pamoja, jambo litakalosaidia kukuza nidhamu, maadili na mshikamano ndani ya chuo.
Sambamba na hayo alitoa wito kwa viongozi, walimu na wanafunzi kushikamana kwa pamoja katika kuhakikisha mafanikio ya SUZA yanafikiwa kwa faida ya taasisi hiyo na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
