NA FAUZIA MUSSA
Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) na Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala Zanzibar wametoa wito kwa watengenezaji na watoa huduma wa tiba hizo kusajili bidhaa na huduma zao ili kulinda afya za wananchi.
Akizungumza kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya tiba asili Barani Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA, Dk. Burhani Othman Simai aliwaasa wananchi dhidi ya matumizi holela ya dawa asilia na virutubisho vya lishe ambavyo havijasajiliwa wala kuthibitishwa usalama wake kiafya.
Alisema baadhi ya bidhaa zinazodaiwa kuwa tiba asili, zinachanganywa na kemikali hatari, zenye uwezo wa kusababisha madhara makubwa, ikiwemo saratani.“Bidhaa hizi si tiba asili halisi. Ni mchanganyiko wa kemikali zisizodhibitiwa zinazotishia afya ya watumiaji.”Alieleza kuwa ZFDA itaendelea kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kuziondoa bidhaa hizo sokoni na kuziteketeza ambapo zitabainika kutokukidhi vigezo.
Aidha, Dk. Simai aliwataka wananchi kuhakikisha wananunua bidhaa hizo katika maduka yaliyothibitishwa kama vile famasi, OTC, au maduka ya tiba asili yaliyo sajiliwa.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Zanzibar, Mohammed Mshenga Makame, alikemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuchanganya dawa za asili na kemikali nyingine zinazopunguza ubora na usalama wake.“Tiba hizi zinaweza kusaidia, lakini zikitumiwa vibaya huleta madhara. Usajili ni lazima siyo hiari.” alisema Makame alisema hadi sasa, kesi sita zimefikishwa mahakamani mwaka 2024 kwa matumizi mabaya ya dawa za tiba asili, ambapo mbili tayari zipo kwenye hatua ya kutoa hukumu.
Aidha, aliwataka wananchi kutotumia dawa yoyote wanayoletewa, hata kama imetoka kwenye nyumba ya ibada, pasipo kujiridhisha kuhusu usalama wakeSiku ya Tiba Asili Barani Afrika huadhimishwa kila tarehe 31 Agosti, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni:“Tiba Asili, Tafiti na Maendeleo.” ikilenga kuhimiza tafiti za kitaalamu na matumizi salama ya dawa asilia.
