NA FAUZIA MUSSA
KATIBU wa Chama cha Kisukari Zanzibar (DAZ), Omar Abdallah, amewahimiza wanafunzi kuepuka matumizi ya bidhaa zinazodhuru afya kama vile tumbaku, pombe na vyakula vyenye sukari nyingi Ili kujikinga na maradhi sugu kama kisukari.
Akitoa elimu ya maradhi hayo kwa wanafunzi wa skuli ya Glorious, Omar aliwahimiza kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo lishe bora, kufanya mazoezi ya mara kwa mara Ili kujikinga na maradhi yasioyakuambukiza kwa ujumla.
Omar aliwaeleza Wanafunzi hao kwa kina jinsi tumbaku inavyoweza kusababisha maradhi sugu ikiwemo saratani, maradhi ya moyo, matatizo ya mapafu, na zaidi ya yote kuchangia kwa kiasi kikubwa na kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya pili kwa mtumiaji.
Kwa Upande wake Mwenyekiti WA DAZ Haji Abdalla ( Golo), alieleza kuwa hatua hiyo imelenga kuongeza uelewa Kwa Vijana juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku na uhusiano wake na maradhi ya kisukari pamoja na athari zake kwa afya ya binadamu.
Alibainisha kuwa matumizi ya tumbaku siyo tu yanaharibu afya kwa ujumla, bali pia yanaongeza uwezekano wa kupata kisukari cha aina ya pili, ambacho kinazidi kuongezeka kwa kasi miongoni mwa vijana.
Alifahamisha kuwa DAZ itaendelea kuungana na Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi si tu katika kutoa elimu maskulini na katika maeneo ya jamii lakini pia kuwafikia kwaajili ya uchunguzi wa awali ili kubaini wagonjwa wapya na kuchukuliwa hatua Jambo ambalo litachangia kukabiliana na ongezeko la maradhi yasioyakuambukiza Nchini.
Wanafunzi washiriki walionekana kuwa na hamasa kubwa ya kujifunza huku wakiuliza maswali mbalimbali kuhusiana na mada hiyo, jambo lililoonesha mwitikio chanya na kiu ya maarifa kuhusu masuala ya afya.
Nao walimu wa Skuli hiyo, waliushukuru uongozi wa DAZ kwa jitihada zao za kuelimisha jamii, hususan wanafunzi, wakisisitiza kuwa elimu kama hiyo ni ya msingi katika kujenga kizazi chenye afya bora.
Mwalimu Hamza alikipongeza Chama cha Kisukari Zanzibar kwa kuandaa tukio hilo muhimu na kuchagua skuli yao kuwa sehemu ya kampeni ya uhamasishaji.
Tunafarijika sana kuona taasisi kama hii inajitokeza moja kwa moja maskulini kutoa elimu ya afya. Wanafunzi wetu wamejifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia kuishi maisha yenye afya njema na maamuzi sahihi.
Takribani Wanafunzi 240 wa kidatu cha Kwanza na pili wa Skuli hiyo walipatiwa elimu hiyo skulini hapo wakitarajiwa kuwa mabalozi wazuri katika jamii inayowazunguka
