TEZ YAELEKEZA MAOFISA ELIMU KUKUTANA NA WALIMU KUIMARISHA TAALUMA ZA WANAFUNZI

NA FAUZIA MUSSA

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Zanzibar (TEZ), Abdalla Mohamed Mussa, amewataka maofisa elimu wa wilaya kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na walimu wa masomo pamoja na wakuu wa taaluma ili kujadili maendeleo ya wanafunzi na ustawi wa kitaaluma wa skuli zilizomo katika maeneo yao.

Akizungumza wakati akimuwakilisha Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Mwanakhamis Adam Ameir katika ufunguzi wa mafunzo kwa wakuu wa taaluma wa skuli za Wilaya ya Magharibi ‘B’, Abdalla alisema kuwa kuwa wakuu wa taaluma ni kiungo muhimu katika mnyororo wa elimu na wana nafasi katika kuhakikisha elimu na ufaulu wa wanafunzi unaimarika.“Wakuu wa taaluma wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia walimu wenzao kwa kuwapatia mbinu na maarifa ya ufundishaji ili kuinua viwango vya ufaulu wa wanafunzi wetu,” alisema Mussa.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imedhamiria kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kwa kuongeza idadi ya waliopata ufaulu wa daraja la kwanza na kuondoa kabisa Divisheni Zero, hivyo ni muhimu kwa walimu kushirikiana kupanga mikakati madhubuti kufanikisha malengo hayo.

Aidha, alihimiza walimu kutumia mbinu za kisasa za ufundishaji zilizowekwa kwenye mtaala wa umahiri, akieleza kuwa njia hizo zina mchango mkubwa katika kumwezesha mwanafunzi kuelewa kwa kina na kuachana na mtazamo wa kusoma kwa nadharia pekee.“Walimu wanapaswa kutumia njia shirikishi, zenye ubunifu na zinazoendana na mazingira halisi ya mwanafunzi ili kuwezesha uelewa wa kina wa masomo,” aliongeza.

Kwa upande wake, ofisa elimu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Abdalla Mohamed, alisema mafunzo hayo yamelenga kuweka mikakati imara itakayosaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa, na kuwataka wadau mbalimbali wa elimu kuunga mkono juhudi hizo. “Ushirikiano wa pamoja kati ya walimu, viongozi na wadau wa elimu ni msingi imara wa kuleta mafanikio ya kweli kwa wanafunzi wetu,” alisisitiza ofisa huyo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu ya Wilaya hiyo, Hussein Iddi Ramadhan, alisema mafunzo hayo ni matokeo ya kikao cha tathmini ya ufaulu wa wanafunzi kilichofanyika baada ya mitihani ya ndani (MOK), ambapo walibaini changamoto zinazowakabili wanafunzi na kuamua kuunda kikosi kazi maalum kitakachosaidia kuimarisha ufaulu wao.“Tumeona kuna umuhimu wa kuwa na mikakati thabiti ya kuimarisha taaluma, na kwa pamoja tutaweza kufanikisha azma ya kuwafanya wanafunzi wetu wafanye vizuri zaidi katika mitihani yao,” alisema Mwenyekiti Hussein.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *