NA OMKR
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema ni wajibu wa viongozi wa dini kulingania haki, utulivu na amani, ili kuiwezesha nchi kusonga mbele kimaendeleo.
Akizungunza baada ya kukutana na Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Mhashamu Augustine Shao, katika Ofisi za Kanisa la Roman Catholic St. Joseph, Minara Miwili, Mjini Unguja, Othman alisema viongozi wa dini wana dhima kubwa ya kuhakikisha haki inatendeka, kwani sauti yao inasikika zaidi.

Katika mkutano huo, Othman pia alikabidhi Ripoti Maalum ya Hali ya Kisiasa Nchini na kueleza nafasi ya ACT-Wazalendo katika mchakato wa kuhimiza amani ya kudumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, alisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila haki na amani.”Kamati za amani zisitumike tu baada ya matatizo kutokea, bali zisimamie sasa kwa kuonya mapema kuhusu mambo yanayoweza kuvuruga amani,” alisema Jussa.
