KUHAKIKISHA USAWA KWA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

Na Salum Ameir

ZANZIBAR – Wadau mbalimbali wameeleza wasiwasi kuhusu uwakilishi mdogo wa watu wenye ulemavu katika Baraza la Wawakilishi, wakizitaka vyama vya siasa na taasisi za serikali kuunda mazingira jumuishi zaidi kisiasa.

Wito huu umetolewa kufuatia kuongezeka kwa malalamiko kwamba mifumo iliyopo kwa sasa inashindwa kuwaruhusu wananchi wenye ulemavu kuchagua au kugombea nafasi za wawakilishi wao.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina jumla ya watu 1,889,773, ambapo 215,434 (sawa na asilimia 11.4) ni watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, kati ya wajumbe 76 wa Baraza la Wawakilishi, viti vitatu pekee ndio vinashikiliwa na watu wenye ulemavu: viti viwili maalum (Mwantatu Mbaraka Khamis na Aza Januar Joseph kutoka jumuiya za CCM) na kimoja cha mteule wa Rais, Anna Athanas Paul.

Huenda mabadiliko chanya zaidi yakaonekana baada ya uchaguzi ujao wa Oktoba, iwapo mwelekeo wa kisiasa utaruhusu uwakilishi mkubwa zaidi wa watu wenye ulemavu.

Salma Saadat, Mwenyekiti wa JUWAUZA (Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar), amesisitiza haja ya ushirikiano kati ya vyama na jamii. Ameeleza kuwa ingawa jamii inaweza kuwa tayari kuwapigia kura watu wenye ulemavu, mara nyingi vyama vya siasa hushindwa kuwaunga mkono wagombea hao, na hivyo kuunda kikwazo kwa fursa zao za uongozi.

Wakati huohuo, Ussi Khamis Debe, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu, amekiri kuwa kumekuwa na maendeleo, lakini amesisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanyika.Amevitaka vyama vya siasa kuunda mazingira jumuishi yatakayowawezesha wagombea wenye ulemavu kushindana kwenye majimbo ya kawaida, si tu kutegemea viti maalum.

Hata hivyo, licha ya historia ndefu ya mashirika yanayotetea haki za watu wenye ulemavu Zanzibar, Adil Mohamed Ali, Mratibu wa Chama cha Wasioona Zanzibar (ZANAB), amesema bado mashirika haya hayajaunda sauti ya pamoja yenye nguvu ya kushawishi sera na sheria. Amewataka washirikiane zaidi ili kuwasilisha mapendekezo yenye nguvu yatakayoweza kusukuma mageuzi ya kimfumo.

Aidha, Wakili Bakar Hamad ametaja nafasi ya vyombo vya habari na teknolojia katika kuziba mapengo, akipendekeza kuwa redio, televisheni, na mitandao ya kijamii vitumike kukuza sauti za wagombea wenye ulemavu na kuwapa majukwaa ya kuunganishwa na wapiga kura bila kukumbana na dharau za kijamii.

Katika hatua nyengine Sada Hamad Ali kutoka Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar ameongeza kuwa ujumuishaji wa kweli pia unatakiwa kuzingatia usawa wa kijinsia. Amesisitiza kuwa wanaume na wanawake wenye ulemavu wana haki sawa ya kupata fursa za uongozi na kuwakilishwa, na kwamba madai yao yawasilishwe waziwazi katika medani ya kisiasa.Baada ya takwimu na mashinikizo yote haya, sauti za watu binafsi ndizo kumbusho kuu la kinachohatarishwa.

Nawaz Ahmed (si jina lake halisi), mtetezi mwenye ualbino, ameonyesha hisia zake za kuchoshwa na hali ilivyo sasa.”Tunataka tuwachague wawakilishi wetu wenyewe ili tuweze kuwawajibisha ,Hatuwezi kumuwajibisha mtu ambaye hatujamchagua; atahudumia yule aliyemchagua” alisema Nawaz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *