Na. Muandishi Wetu
Jumuiya ya Wawekezaji katika Sekta ya Utalii (ZATI) imetakiwa kushirikiana na Mamlaka za Ukusanyaji wa Mapato Nchini ili kuhakikisha wafanyabiashara wote wanaolaza wageni wanasajiliwa na kulipa Kodi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ofisi ya Zanzibar ndugu Saleh Haji Pandu wakati akifungua Semina ya Marekebisho ya Sheria za Kodi kwa mwaka 2025/2026 kwa Uongozi na Wanachama wa ZATI, katika Ukumbi wa Mikutano wa TRA, Mayugwani Mjini Zanzibar.
Kamishna Saleh alisema katika Sekta ya Utalii zipo biashara nyingi zinazofanyika kwa njia ya Mtandao ikijumuisha wanaolaza wageni kwa mfumo wa “Air BnB” na kusisitiza kuwa hawa wote wanapaswa kusajiliwa na kulipa Kodi kama wengine ili kuhakikisha kila anayefanya biashara anasajiliwa na kulipa Kodi, pamoja na kuweka mfumo sawa wa ulipaji kodi, Kamishna Saleh aliitaka ZATI kutoa mashirikiano ya dhati kwa kwa TRA na ZRA ili kuhakikisha wasiolipakodi wanalipa na biashara ya utalii inastawi nchini.
Ndugu Saleh aliongeza kuwa, marekebisho ya Sheria za Kodi kwa mwaka 2025/2026 yamelenga kuipa uwezo Serikali kuwasaidia Wafanyabiashara katika kustawisha biashara zao sambamba na kuendana na mwenendo wa mfubo wa biashara Duniani.

Akiwasilisha marekebisho hayo kwa upande wa Sheria zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi ndugu Makame Khamis Moh’d aliwataka wafanyabiashara wenye madeni kuchangamkia fursa ya msamaha wa Adhabu na Riba iliyotolewa na Serikali ili waweze kujipangaupya katika biashara zao.
Alisema pamoja na marekebisho mengine, ZRA katika mwaka huu wa fedha itaanza rasmi kusajili vyombo vya moto vinavyotumia Umeme ili navyo viweze kutambulika rasmi katika mfumo wa usajili wa vyombo vya Moto.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha marekebisho ya Sheria za Kodi zinazosimamiwa na TRA kwa mwaka 2025/2026, Mkuu wa Kitengo cha Elimu na Mawasiliano kutoka kutoka taasisi hiyo ndugu Shuwekha Salum Khalfan aliwataka Washiriki kuyapokea marekebisho hayo na kuyafanyia kazi kwani tayari utekelezaji wake umeanza.

Nao Washiriki wa Semina hiyo walizishukuru Mamlaka za Kodi nchini kwa kuona umuhimu wa kuwaita na kuwapa taarifa za marekebisho yaliyopo na wakafafanua kuwa yatawasaidia katika majukumu yao ya kibiashara na Kikodi.

ZRA tunashukuru kwa elimu hiyo maanake kina bishara nyingi za mtandaoni ambazo zinafanywa na watu wanaingiza mamilioni ya fedha hakika Hilo ni jambo jema