MTOTO WA MIAKA 14 ABAKWA NA KUPATA UJAUZITO KIDIMNI, MTUHUMIWA AKIMBILIA KUSIKOJULIKANA

Na Abdul sakaza


“Nilikuwa natamani nikue na kuwa mwalimu, lakini sasa niko hivi na sijui nifanye nini, Malengo yangu yamekatishwa na sijisikii kama nina mustakabali tena,” alisema kwa sauti ya huzuni Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 anayesoma darasa la saba Shule ya Msingi Kidimni (jina linahifadhiwa), na ambae amefanyiwa ukatili wa kingono na kupata ujauzito, hali iliyosababisha taharuki kubwa kwa familia, jamii na viongozi wa kijiji hicho cha kidimni kilichopo Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.


Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto huyo, tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa jioni alipokuwa akienda kujisaidia katika vyoo vya shule hiyo baada ya kumalizika kwa muda wa ziada wa masomo. Inadaiwa kuwa alikumbana na kijana mmoja (jina tunalihifadhi) ambaye alimshambulia na kumlazimisha kufanya naye kitendo cha ndoa bila ridhaa yake. Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa anadaiwa kukimbia kusikojulikana.


Mtoto huyo, akiwa na huzuni kubwa, alisema ‘naogopa hata kutoka njee’, Shuleni walinisema na mtaani pia wanasema ndio maana naamua kukaa ndani ” alisema kwa sauti ya chini kabisa.


Bibi wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 65 (jina tunalihifadhiwa) alisema familia yao bado haijapata muafaka wowote wa kufuatilia swala hilo kisheria na wako kwenye mateso makubwa kutokana na changamoto zinazoambatana na tukio hilo na amewaomba wanasheria na mamlaka kuwasaidia ili kupatikana haki ya mjukuu wao kwani wao hawana uwezo wa kuishuhulikia kesi hio .

kwa masikitiko Alieleza kuwa maisha ya mjukuu wake yamebadilika kwa kiasi kikubwa kwani sasa anaonekana mwenye huzuni na amepoteza furaha ya utoto aliyokuwa nayo awali. “Mjukuu wangu alikuwa na ndoto nyingi, lakini sasa hana tena hamasa ya kwenda shule wala ndoto za maisha. Amebaki mwenye wasiwasi kila wakati na mara nyingi hukaa kimya kana kwamba amechoka na dunia hii,” alisema bibi huyo kwa majonzi.


Alifafanua kuwa familia inapitia hali ngumu ya kimaisha kwani hawana chakula cha kutosha wala mahitaji muhimu ya kila siku. “Tunapitia matatizo makubwa ambayo yamesababishwa na maumivu ya kitendo alichofanyiwa mjukuu wangu na kimesabaisha mpaka Hata chakula cha kila siku ni shida sijui nimsaidiaje mjukuu wangu wakati anatakiwa kupata lishe bora na huduma za kiafya kwa sababu ya ujauzito huu,” aliongeza huku akisisitiza kuwa wanahitaji msaada wa haraka kutoka kwa jamii na serikali.

katika hatua nyengine bibi huyo na mjukuu wake wameziomba mamlaka husika kufatilia na kukamatwa kwa mtuhumiwa ili haki itendeke ili iwe funzo kwa watu wengine ambao wanania ya kuwaharibu watoto wengine.

Bw. Mathew Herman Cyprian na Bii Jina Mtumwa Mkombe ni wanaharakati wa masuala ya ukatili wa kijinsia eneo hilo wamesema kupitia ukatili wa mtoto huyo walichukua kila aina ya juhudi ili kuhakikisha kesi hii inaripotiwa polisi kwa hatua ya kwaza na kupatikana kwa haki lakini chakusikitisha mtuhumiwa wa kesi hii amekimbia kusiko julikana na wameziomba mamlaka husika kulifatia suala hili ili sheria ichukue mkondo wake .


Wameongeza kua sasa ipo haja ya mshikamano wa pamoja baina ya wazazi, jeshi la polisi, viongozi wa kijamii na wadau wa maendeleo katika kupambana na ongezeko la vitendo vya udhalilishaji. “Kesi kama hizi hazipaswi kuachiwa familia peke, Tunahitaji mshirikiano wa dhati ili watoto wetu walindwe ipasavyo,” walisisitiza.
Hii inaonyesha namna ambavyo matukio ya aina hii yanavyojitokeza kwa wingi katika jamii ya Zanzibar licha ya juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na serekali na wadau wengine wa maendeleo.


Kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Jumla ya matukio 107 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi wa Julai, 2025 ambapo waathirika walikuwa 107. Waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 88.8, wakifuatiwa na wanawake asilimia 11.3 na wanaume asilimia 0.9

Wilaya ya Magharibi ‘A’ imeripotiwa kuwa na matukio mengi ukilinganisha na Wilaya nyengine, matukio 26 sawa na asilimia 24.3 ikifuatia Wilaya ya Kati ambapo yameripotiwa matukio 16 (asilimia 15.0).

Wilaya ya Mkoani imeripotiwa kuwa na idadi ndogo ya matukio, tukio moja (1) sawa na asilimia 0.9. Wilaya ya Kati imeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya kubaka ikilinganishwa na Wilaya nyengine, ambapo jumla ya matukio ya kubaka 12 sawa na asilimia 21.1 kati ya matukio yote ya kubaka yaloripotiwa.

Ali Shehe Kombo ni Afisa Ustawi Wa Jamii Wilaya Ya Kati Mkoa Kusini Unguja amesema vitendo vya udhalilishaji katika wilaya hiyo vimekithiri licha ya kuwepo kwa juhudi mbali mbali za utoaji elimu kwani kwa mwezi huu wa nane zaidi ya kesi tatu zimeripotiwa katika ofisi yake.


Akizingumzia suala la mtoto huyo amesema amesikitishwa sana na ukatili aliyofanyiwa mtoto huyo asiejua nini ujauzito na amefahamisha kua taarifa za kitabibu kutoka kwa madaktari wa Hospitali ya Mnazi Mmoja zinaonyesha kwamba msichana huyo hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida kutokana na njia yake ya uzazi kuwa ndogo. “Madaktari wametushauri hatua mbadala za kitabibu zichukuliwe ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto atakayezaliwa unapatikana, Serikali na ofisi yetu tupo karibu kufuatilia hatua kwa hatua,” alisema afisa huyo.


Awali Mwalimu wa ushauri nasaha wa Shule ya Msingi Kidimni Bii Kaeni Issa Pandu ameweka bayana kua tukio hilo limekatisha ndoto za mwanafunzi ambaye alikuwa akionyesha uwezo mkubwa darasani. “Mwanafunzi huyu alikuwa na ufahamu wa hali ya juu, Mara nyingi alikuwa anashika nafasi ya kumi hadi kumi na tatu darasani, na tulitegemea afanye vizuri katika mtihani wa taifa wa darasa la saba. Kukatishwa malengo yake ni ubaya usiokubalika,” alisema mwalimu huyo.


Wakati huo huo, baadhi ya majirani wa eneo hilo wamelalamikia kuongezeka kwa matukio ya udhalilishaji wa watoto katika kijiji hicho na kuomba mamlaka zinazohusika kuchukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa “Watoto wetu wako hatarini. Kama hatutachukua hatua sasa, kizazi chetu kitapotea,” alisema mmoja wa wananchi aliyeomba jina lake lihifadhiwe.


Kesi hiyo imeripotiwa katika Kituo cha Polisi Dunga huku Tukio hili likiwa limeibua mjadala mpana juu ya usalama wa watoto shuleni na mtaani kwao.

3 thoughts on “MTOTO WA MIAKA 14 ABAKWA NA KUPATA UJAUZITO KIDIMNI, MTUHUMIWA AKIMBILIA KUSIKOJULIKANA

  1. Dah Allah atuhifadhi n familia zetu ila hil suala ni gumu maana amekatisha ndoto za Binti mdogo kabisa meenye malengo makubwa

    NAWAOMBA WANAO HUSIKA NA KESI ZA UDHLILISHAJI WAWKE JUHUDI KUBWA ZA KUWEZ KUMNASA MUHALIFU WA TUKIO KWA VYOVYOTE IWAVYO

  2. Kesi za udhalilishaji bado Zanzibar hazijapatiwa mu 40 ila laiti wangeuliwa au kuhasiwa basi haya yangeondoka la kwani nyie baadhi ya wanaume mmekua makatili sana hemu semeni na akili zenu

Leave a Reply to Siti kombo Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *