
Mkoa Wa Kaskazini Unguja
Na Abdul Sakaza,
Wiki ya Unyonyeshaji Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi 7 ambapo nchi zaidi ya 120 ikiwemo Tanzania – Zanzibar zinaungana kwa pamoja kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani inayolenga kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kunyonyesha, huku ikihimiza serikali na mashirika ya afya kuunga mkono wanawake katika kuhakikisha watoto wanapata maziwa ya mama kwa wakati na kwa ukamilifu.
Hata hivyo, katika jamii nyingi, hususan visiwani Zanzibar, suala la mama kunyonyesha maeneo ya umma limekuwa jambo lenye kuibua mitazamo tofauti, huku wanawake wengi wakijikuta wakihisi aibu na hata wengine wakihisi kunyonyesha hadharani ni kuonyesha sehemu nyeti ya mwili wao .
Hali hii imeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika juhudi za kuhakikisha watoto wanapata maziwa ya mama kwa muda unaostahili, hususan ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa na kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kuongezewa maji au vyakula vingine.
WANAWAKE WAKIRI KUKOSA UJASIRI KUNYONYESHA SEHEMU ZA UMMA

Katika mahojiano maalum yaliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini “B” Panga Tupu, wanawake kadhaa walikiri kuwa aibu ya namna hii huwafanya wasiwe tayari kunyonyesha watoto wao wakiwa maeneo ya umma kama sokoni, stendi,magari ya umma na hata katika taasisi mbali mbali.
Bi Fatma Ali, mama wa mtoto wa miezi mitatu na Mkaazi wa Bumbwini anasema, “Siku moja nilikuwa kwenye daladala na mtoto akalia kwa njaa, lakini sikumnyonyesha mpaka nilipofika nyumbani Nilikua naona aibu watu wataniona sijiheshimu.”
Kauli kama hiyo inashabihiana na aliyosema mama mwingine ambaye hakutaka jina lake kutajwa anasema, “Hata ofisini, siwezi kumnyonyesha mwanangu,Watu wanaweza kuniangalia vibaya, na si kila mmoja anaelewa umuhimu wa maziwa ya mama.”
Wataalamu wa afya wanakiri kuwa aibu ya kunyonyesha ni moja ya changamoto kubwa zinazowakumba wanawake, hasa maeneo ya vijijini ,Thuwaiba Ibrahim Haji muuguzi wa afya ya mama na mtoto hospital ya wilaya kaskazini “A” Kivunge, anasema jamii inahitaji kuelimishwa zaidi kuhusu unyonyeshaji.
“Unapomwambia mama anyonyeshe ndani ya saa moja baada ya kujifungua halafu anapokua kliniki anaona aibu kunyonyesha, au katika maeneo ya umma anahaki ya kunyonyesha lakini hii ni changamoto kwao Tunahitaji jamii ielewe kuwa kunyonyesha si aibu, bali ni haki ya mtoto,” alisema muuguzi huyo.
Mitazamo ya kijamii kwamba mama anayenyonyesha hadharani “hajiheshimu” au “anajianika” imeendelea kuwafanya wanawake wengi wa Zanzibar, hasa Kaskazini Unguja, kuzuia tendo hilo hata pale linapohitajika haraka.
Wapo baadhi ya wanaume na hata wanawake wenzao wanaowakejeli au kuwapigia vijembe akinamama wanaojaribu kunyonyesha hadharani, hali inayoongeza msongo wa mawazo kwa mama na kumwacha mtoto bila kunyonya wakati anapokua eneo la wazi

Kunyonyesha ni mchakato wa kiasili na wa kiafya unaotambulika na kupendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na wataalamu wa afya kote duniani. Maziwa ya mama yana virutubisho vyote muhimu na kinga ya mwili kwa mtoto, hasa katika miezi ya mwanzo.
Wataalamu wanasema kuwa kuchelewa kunyonyesha au kumpa mtoto maziwa ya kopo badala ya maziwa ya mama huongeza hatari ya maambukizi, utapiamlo na matatizo ya ukuaji.
Shirika la Afya Duniani WHO na Shirika La umoja wa Mataifa la kuhudumia wayoto UNICEF zilitoa ripoti ya pamoja na kuweka malengo ya kunyonyesha watoto bila kuwapa kitu kingine chochote kwa miezi sita wafikie asilimia 50 ifikapo mwaka 2025 ,Lakini takwimu zilizotolewa wiki hii ya unyonyeshaji zinaonesha ni asilimia 44 pekee ya watoto wachanga wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza ya maisha .WHO na UNICEF pia inakadiria kuwa maisha ya watoto 820,000 wa chini ya miaka 5 yangeokolewa kila mwaka endapo watoto wote wangenyonyeshwa ipasavyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Save the Children, watoto zaidi ya milioni 2.7 hufariki kila mwaka duniani kutokana na matatizo yanayotokana na utapiamlo ambao mara nyingi huanzia katika kutonyonyeshwa maziwa ya mama kwa njia sahihi

Waziri wa Afya Zanzibar, Nasor Ahmed Mazrui anasema wanashirikiana ipasavyo na mashirika afya ya kimataifa kama vile WHO, UNICEF na SAVE THE CHILDREN ili kutoa miongozo kwa mama wanaonyonyesha ili kufikia malengo ya kimataifa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar .
Wazir Mazri amesema ” Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hutoa likizo ya miezi mitatu kwa wafanyakazi wake pale wanapojifungua ili kuwanyonyesha vyema watoto wao jambo ambalo linapaswa kuigwa na Taasisi binafsi” alisema mazrui
NAFASI YA DINI KATIKA UNYONYESHAJI
Katika Uislamu, suala la unyonyeshaji lina nafasi kubwa na limeelekezwa moja kwa moja ndani ya Qur’an,Kitabu hichi kitakatifu kinabainisha kuwa mama anatakiwa amnyonyeshe mtoto wake kwa muda wa miaka miwili kamili, kwa yule anayetaka kukamilisha kipindi kamili cha unyonyeshaji.
Aya ya Surah Al-Baqara (2:233) inasema: “Na wale wanaoamua kunyonyesha, basi mama wawanyonyeshe watoto wao kwa miaka miwili kamili. (Hili ni kwa) anayetaka kukamilisha muda wa kunyonyesha…”
Aidha, Qur’an inaweka bayana kuwa baba anatakiwa kubeba jukumu la kumgharamia mama anayenyonyesha, jambo linaloonyesha mshikamano wa kifamilia katika malezi bora ya mtoto.
Kwa upande wa Ukristo, unyonyeshaji umeonyeshwa kuwa ni tendo la huruma na upendo wa asili kati ya mama na mtoto, Ingawa Biblia haitoi muda mahususi wa kunyonyesha, inaashiria umuhimu wa tendo hilo katika maisha ya mwanadamu.
Katika kitabu cha Isaya 49:15, Mungu anatoa mfano wa mama na mwanawe ili kueleza kiwango cha huruma: “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, asimhurumie mwana wa tumbo lake?” Mfano huu unadhihirisha kuwa kwa mtazamo wa kidini, mtoto anayenyonya hakuwa tu sehemu ya mwili wa mama bali pia hufungamana na hisia na huruma za kina jambo linaloonyesha thamani ya kunyonyesha kama jukumu la kiroho na kijamii.

Kulingana na hali hii Ni wakati sasa jamii za Zanzibar zikaweka wazi kuwa kunyonyesha hadharani si jambo la aibu wala fedheha,Familia, viongozi wa dini, wazazi wa kiume, na jamii kwa ujumla wanapaswa kusaidia kubadilisha mtazamo huu potofu.
Hii ni pamoja na kuanzisha “Maeneo Rafiki kwa Unyonyeshaji” katika ofisi, masoko, vituo vya afya na maeneo ya wazi ambapo wanawake wanaweza kunyonyesha bila hofu .
Wiki ya Unyonyeshaji Duniani iwe chachu ya mabadiliko si kwa maneno tu, bali kwa vitendo kwani Tunapoadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani 1–7 Agosti ni kukuza kulinda na kusaidia unyonyeshaji kwa nguvu na mshikamano ambapo Mwaka huu 2025 kaulimbiu “Toa Kipaumbele kwa Unyonyeshaji, Tengeneza Mifumo ya Msaada Endelevu”

Kazi nzuri sana
asante sana kaka