ZRA YAPELEKA HUDUMA MITAANI

Na. Muandishi Wetu

Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imeanzisha Kambi maalum za Huduma za Kodi zitakazofanyika katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa Wananchi.

Akizungumza jana wakati wa Kambi hiyo inayotambulika kwa jina la ZRA Mtaani Kwako iliyofanyika Chuini, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Wateja kutoka ZRA, ndugu Makame Khamis Mohd, alisema ZRA imeamua kuwasogezea huduma wananchi ili kupunguza muda wanaotumia kufuata huduma ofisini na kuwapa unafuu katika shughuli zao za kila siku.

Alifafanua kuwa, pamoja na kuwa ZRA imeweka ofisi katika kila Mkoa, bado imeona kuna umuhimu mkubwa wakuwakaribia na kuzisogeza huduma zao karibu na maeneo ya biashara na makaazi ili kurahisisha huduma hizo.Hivyo, aliwataka wananchi katika maeneo mbali mbali kuzitumia kikamilifu kambi hizo ili waweze kupata huduma kwa urahisi, kwa ukaribu na kwa wakati pasi na kuathiri harakati zao.

Alifafanunua kuwa huduma za Usajili wa biashara, elimu na Ushauri wa Kodi, Leseni za Udereva, Malipo ya Kodi sambamba na utaratibu wa kupata namba mpya za Vyombo vya Moto ni miongoni mwa huduma zinazotolewa katika Kambi hizo.

Baadhi ya wananchi waliotembelea kambi hiyo iliyofanyika Kituo cha Daladala Chuini Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, wameipongeza Serikali kwa kuwawekea utaratibu huo katika kutoa huduma na kuongeza kuwa utaleta ufanisi na urahisi kwa wananchi.

Yussuf Simon mkaazi wa Chuini ambaye ni miongoni mwa Wananchi waliofika katika Kambi hiyo na kupata huduma ameipongeza ZRA kwa kuwasogezea huduma na kubainisha kuwa imekuwa ni ya haraka na isiyopoteza muda ukilinganisha na kwenda ofisini.

Huduma ni ya haraka sana, tofauti na kwenda ofisini ambapo unatumia muda mrefu kusubiri kupata huduma, alisema.

Naye Suleiman Mohammed Ali kutoka Mbuzini, aliyefika katika Kambi hiyo kwa lengo la kupata namba mpya, aliwahimiza wamiliki wa vyombo vya moto ambao bado hawajafanya mabadiliko ya namba kuitumia fursa hiyo kwani utaratibu huo umewekwa kwa kwa mujibu wa sheria na taratibu halali za nchi.

Kutamatika kwa Kambi hii ya Siku sita (6) katika eneo la Kituo cha Mabasi Chuini, kunatoa fursa ya kupata huduma zinazotolewa na Kambi hiyo kwa Wananchi wa Mikoa mengine.

Kambi hiyo inatarajiwa kuendelea katika Mkoa wa Kaskazini na Kusini Unguja na hatimaye Kisiwani Pemba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *