NA FAUZIA MUSSA
KITUO cha Msaada wa Kisheria Zanzibar (ZLSC) kimesema kitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi, hususan wale wanaojishughulisha na kilimo cha mwani visiwani Zanzibar.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wa shehia ya Kikungwi, Wilaya ya Kati Unguja, Mkurugenzi wa ZLSC, Felista Mauya, alisema wanawake wakulima wa mwani wanastahili kuungwa mkono katika juhudi zao za kujitafutia kipato ili kuboresha maisha yao na familia zao.
“Wanawake hawa si tu kuwa wanahitaji msaada wa kisheria, bali pia wanapaswa kupewa elimu ya fedha, kuunganishwa na masoko ya uhakika, kupatiwa vifaa vya kisasa vya kilimo, na mafunzo ya usindikaji wa mazao yao ili kuongeza thamani na tija katika shughuli zao,” alisema Mauya.

Alieleza kuwa mwani ni zao lenye faida kubwa kiuchumi endapo litachakatwa na kugeuzwa kuwa bidhaa mbalimbali zenye soko ndani na nje ya nchi, tofauti na kuuza zao hilo katika hali yake ya asili kama inavyofanyika sasa kwa wakulima hao.”Wapo wanaonunua mwani kutoka kwa wakulima wetu, lakini wao huenda wakaliongezea thamani kwa kutengeneza sabuni, mafuta, au bidhaa za urembo na kuuza kwa bei ya juu. Huu ni ushahidi kuwa wanawake hawa wana fursa ya kuongeza mapato yao kama watawezeshwa,” alisisitiza.
Mapema Mauya alieeleza kuwa ZLSC itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada wa kisheria, lakini pia kuangazia namna ya kujumuisha masuala ya kijamii na kiuchumi hasa kwa makundi maalum kama wanawake na wenye ulemavu ili kuhakikisha wanapata haki na fursa sawa za maendeleo.

Kwa upande wao, wakulima wa mwani katika shehia ya Kikungwi waliiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuwaangalia kwa jicho la huruma kutokana na mazingira magumu ya kazi yao na mapato yasiyoendana na juhudi wanazoweka.
Bahati Issa Suleiman, Katibu wa Kamati ya Uvuvi Kikungwi, aliiomba Serikali kuweka bei elekezi ya mwani ili kuwasaidia wakulima kupata kipato chenye tija.”Zao hili linahitaji kazi kubwa kuanzia kuvuna, kuchakata hadi kukausha. Hata hivyo, hatupati bei inayotufaa. Tunahitaji Serikali iingilie kati na kuweka bei elekezi itakayolinda maslahi ya wakulima,” alisema Bahati.
Wakulima hao pia walieleza kuwa bado kuna changamoto ya soko la bidhaa zinazozalishwa nchini, kwani wananchi wengi hupendelea bidhaa kutoka nje, jambo linalopunguza thamani ya bidhaa za wazalendo na kulazimisha wakulima kuuza mwani ghafi.”Tunaomba wananchi wabadilike, wawe wazalendo kwa kununua bidhaa za hapa hapa nyumbani. Tukiweza kuchakata mwani na kupata bidhaa kama sabuni, mafuta ya ngozi au bidhaa za afya, wenzetu watusapoti kwa kununua,” alisema mmoja wa wakulima hao.
