ZIMWI LINALOIHUJUMU SERIKALI MAMILIONI YA FEDHA KASKAZINI UNGUJA

Na Abdul Sakaza

Akiripoti Kutoka Kaskazini Unguja
Imeboreshwa Saa 3  Zilizopita

Wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiendelea na jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ili kugharamia huduma za kijamii, ujenzi wa miundombinu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hali ni tofauti katika eneo la Fungurefu, lililopo Shehia ya Mto wa Pwani, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Eneo hili limegeuka kuwa kitovu cha biashara haramu ya uchimbaji mchanga, hali inayosababisha upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali na hata serekali ya Kijiji hali ambayo inaweza kuzorotesha juhudi za maendeleo ya taifa.

Uchunguzi wa kina uliofanywa kwa muda wa takriban miezi mitano, ukihusisha ukusanyaji wa takwimu za mzunguko wa magari, bei ya  mchanga na uchunguzi wa moja kwa moja wa shughuli zinazofanyika, umebaini kuwepo kwa mtandao wa uchimbaji mchanga usio na vibali rasmi. Shughuli hizi zinafanyika mchana na usiku, bila ya ufuatiliaji wa karibu kutoka mamlaka husika, hali inayofanya eneo hilo kufanana na “shimo la upotevu” wa mamilioni ya fedha kila dakika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa, Magari yanayohusika zaidi katika usafirishaji wa mchanga ni aina ya Toyota Dyna na Mitsubishi Fuso,Magari haya hufanya safari nyingi kwa siku, yakichukua mchanga moja kwa moja kutoka mashimoni na kuusafirisha kwenda maeneo mbali mbali yanayohusika, Kutokana na uchimbaji huu kuwa wa magendo na kukosa vibali halali, hakuna ushuru, ada wala kodi yoyote inayolipwa Serikalini au kwa Serikali ya Kijiji.

Bei ya mchanga shimoni kwa gari aina ya Toyota Dyna ni shilingi elfu ishirini (20,000) kwa tripu moja, huku Mitsubishi Fuso ikiuzwa kwa shilingi elfu arobaini (40,000) kwa tripu moja. Ingawa bei hizi zinaweza kuonekana kuwa za kawaida kwa wanunuzi shimoni lakini kwa mtazamo wa mapato ya Serikali, zinawakilisha kiwango kikubwa cha fedha kinachopotea nje ya mfumo rasmi wa ukusanyaji wa mapato.

MCHANGANUO WA MAPATO YANAYOPOTEA (FINANCIAL LEAKAGE)

Kuazia saa nne na dakika ishirini asubuhi (4:20) hadi saa kumi na moja na dakika arobaini jioni (11: 40) Gari zote kwa ujumla ambazo ni  aina ya Toyota Daina kwasiku huchukua zaidi ya triipu mia tatu na kumi (310) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Milioni Sita Na Laki Mbili (6,200,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu (9,300) sawa na Shilingi Milioni Mia Moja Na Themanini Na Sita (186,000,000)

Kadhalika Gari zote kwa ujumla ambazo ni  aina ya Mitsubishi Fuso kwasiku huchukua zaidi ya triipu Hamsini (50) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Milioni Mbili (2,000,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu Elfu Moja Namia Tano (1,500) Sawa Na Shilingi Milioni Sitini (60,000,000)

        Jedwali La Uchambuzi Wa Mapato Ya Mchanga Fungurefu (Muda Wa Mchana)

Aina ya GariBei kwa Tripu (TSH)Tripu kwa SikuMapato kwa Siku (TSH)Tripu kwa MweziMapato kwa Mwezi (TSH)Mapato kwa Mwaka (TSH)Serikali KuuSerikali ya Kijiji
Toyota Dyna20,0003106,200,0009,300186,000,0002,232,000,00000
Mitsubishi Fuso40,000502,000,0001,50060,000,000720,000,00000
JUMLA3608,200,00010,800246,000,0002,952,000,00000

Pia tumeangalia wakati wa usiku Kuazia saa moja na dakika kumi usiku (1:10) hadi saa tano na dakika kumi usiku (5:10) Gari aina ya Toyota Daina kwa muda huu huchukua zaidi ya triipu kumi na saba (17) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Laki Tatu na Elfu Arobaini (340,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu (510) sawa na Shilingi Milioni kumi na laki mbili (10,200,000)

 Kuazia saa moja na dakika kumi usiku (1:10) hadi saa tano na dakika kumi usiku (5:10) Gari aina ya aina ya Mitsubishi Fuso huchukua zaidi ya triipu nne (4) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Elfu Themanini (80,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu mia moja na ishirini (120) Sawa Na Shilingi Milioni mbili na laki nne  (2,400,000)

  Jedwali La Uchambuzi Wa Mapato Ya Mchanga Fungurefu (Muda Wa Usiku)

MaelezoBei kwa TripTrip kwa Usiku MmojaTrip kwa MweziMapato kwa Usiku MmojaMapato kwa MweziMapato kwa MwakaSerikali KuuSerikali ya Kijiji
Toyota Dyna20,00017510340,00010,200,000122,400,00000
Mitsubishi Fuso40,000412080,0002,400,00028,800,00000

Kwa kujumlisha mapato ya mchana na usiku, zaidi ya shilingi milioni 258,600,000 huzalishwa kwa mwezi kupitia biashara hii haramu ya mchanga katika eneo la Fungurefu. Kwa mwaka, kiwango hiki ni shilingi bilioni 3.1 fedha ambazo zingeliweza kujenga au kukarabati  vituo vya afya ikiwemo vifaa tiba na madawa ,Madarasa, Barabara za vijijini au hata kusaidia miradi ya maji safi na salama katika jamii.

Swali linalobaki ni nani anasimamia shughuli hizi? Je, ni uzembe wa kiutendaji, ukosefu wa rasilimali za ufuatiliaji, au kuna mtandao mpana unaonufaika na biashara hii ya magendo? Bila majibu ya wazi na hatua za haraka, Serikali itaendelea kupoteza mapato muhimu huku mazingira yakiharibiwa kwa kasi kubwa.

Wataalamu wa uchumi wanasema kuwa katika kipindi ambacho Serikali inaongeza juhudi za kupanua wigo wa kodi na kuhimiza ulipaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa, ni muhimu pia kuziba mianya mikubwa ya upotevu wa mapato kama huu. Mapato yanayopotea katika eneo moja pekee yanaweza kuwa sawa na bajeti ya maendeleo ya sekta fulani katika Wilaya moja au Mkoa .

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia wizara na taasisi zake husika, inapaswa kufanya ukaguzi wa haraka na wa kina katika eneo la Fungurefu na maeneo mengine yanayodaiwa kuwa na shughuli kama hizi. Utoaji wa vibali, ufuatiliaji wa uzalishaji na ukusanyaji wa ushuru vinapaswa kuimarishwa kwa kutumia mifumo ya kidijitali ili kuzuia mianya ya upotevu.

Kwa sasa, Fungurefu imebaki kuwa mfano halisi wa jinsi rasilimali zinavyoweza kugeuka kuwa “zimwi” linaloihujumu Serikali kwa kunyonya mamilioni ya fedha kila mwezi,Bila hatua za makusudi, zimwi hili litaendelea kukua, na gharama yake italipwa na wananchi kupitia kukosekana kwa huduma bora za kijamii na maendeleo endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *