ZFDA YAZUIA VIRUTUBISHO VYENYE MADHARA KWA WATUMIAJI

NA FAUZIA MUSSA

WAKALA wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imepiga marufuku uingizaji wa bidhaa za virutubisho vyenye mchanganyiko wa dawa za hospitali, kutokana na madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi holela ya bidhaa hizo bila ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari na wataalamu wa afya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii huko Ofisini kwake Mkurungezi Mtendaji wa ZFDA Dk. Burhani Othman Simai, alisema kuwa dawa hizo zimekuwa zikiingizwa nchini kinyume cha sheria na zimebainika kuwa na madhara kwa afya ya binaadamu.

Alieleza kuwa ZFDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walifanikiwa kukamata shehena ya virutubisho hivyo takriban ya tani 2.5 katika matukio tofauti ndani ya kipindi cha miezi miwili zililzoingizwa kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa hali inayoonesha ongezeko kubwa la matumizi ya bidhaa hizo miongoni mwa wananchi.“Watumiaji wengi hawazingatii maelekezo ya kitaalamu na hawajui madhara makubwa wanayoweza kuyapata, hasa wanapotumia virutubisho hivi bila usimamizi wa daktari,” alisema Dk. Burhani.

Alisema virutubisho hivyo vinadaiwa kuongeza hamu ya tendo la ndoa na kukuza maumbile ya sehemu za siri, na mara nyingi huchanganywa na asali au chocolate ili kuwavutia watumiaji. Dk. Burhan alivianisha virutubisho hivyo kuwa ni pamoja na royal honey, M plus, Etuma na gold Q7 chocolate ambazo huchanganywa na dawa asili pamoja na dawa za hospitali, jambo linaloongeza hatari ya madhara.

ZFDA imebainisha madhara makubwa yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya bidhaa hizo, ikiwa ni pamoja na kupata Kifafa, mshtuko wa moyo, Kifo cha ghafla hasa kwa wagonjwa wa VVU wanaotumia dawa za ARV na Kushindwa kushiriki tendo la ndoa baada ya kuacha matumizi ya virutubisho hivyo.

Alisema Changamoto nyingine za kiafya zinaweza kuwa kupungua kwa uoni, na usikivu.

Kutokana na hatari hizo, ZFDA imepiga marufuku uingizaji na uuzaji wa virutubisho visivyosajiliwa, na imeahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaokiuka agizo hilo. “Tunatoa wito kwa wananchi wanaotumia virutubisho hivyo kuacha mara moja na kutoa taarifa kwa mamlaka pale wanapobaini uwepo wa bidhaa hizo katika maeneo yasio rasmi,” alisema

Aidha ZFDA imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa bidhaa zisizosajiliwa haziingii tena nchini na kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi salama ya Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *