ZBS YATANGAZA TUZO ZA UMAHIRI

NA FAUZIA MUSSA

TAASISI ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeandaa mashindano ya tuzo za umahiri 2026, yanayolenga kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma bora zilizothibitishwa kwa viwango vya kitaifa na kikanda.

Mashindano hayo yanahusisha biashara ndogo na ndogo sana (MSE – Micro and Small Enterprises) na biashara za kati na kubwa (MLE -Medium and Large Enterprises) ambapo mwisho wa kuwasilisha maombi ni Aprili 6, 2026 saa 3:30 asubuhi.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ya mwongozo wa ushiriki Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Ubora (ZBS) Suleiman Abdalla aliwataka wafanyabiashara wenye nia kuzingatia muda wa kuwasilisha maombi yao kwani maombi yatakayochelewa hayatapokelewa.

Suleiman aliyataja makundi ya tuzo hizo kuwa ni pamoja na kampuni bora ya mwaka, bidhaa bora ya mwaka, mtoa huduma bora wa mwaka (Kampuni Binafsi), msafirishaji bora wa mwaka wa bidhaa za jumla pamoja na tuzo ya mtu binafsi aliyechangia kwa kiwango kikubwa masuala ya viwango vya kitaifa, uhakikishaji wa ubora, uthibitishaji na vipimo (SQAM) na kubainisha kuwa washiriki wanaweza kuwania zaidi ya kundi moja kulingana na sifa na vigezo vilivyowekwa.

Aidha alifahamisha kuwa washiriki wanatakiwa kuwasilisha maombi yao kwa kuoanisha mafanikio yao na vigezo vya kila kipengele wanachowania, wakitumia vielelezo kama picha, chati na takwimu zitakazowezesha majaji kutathmini kwa urahisi mchango wao katika jamii kupitia ajira na mnyororo wa thamani.

” kampuni au Taasisi zinaweza kushiriki kundi zaidi ya moja. Maombi yatakayokubaliwa ni yatakayotumwa kupitia anuani zilizotajwa.” Alisisitiza
Pamoja na hayo alibainisha kuwa ili kushiriki ni lazima kampuni na taasisi ziwe zimesajiliwa Zanzibar na kuwa na nyaraka halali ikiwemo usajili wa biashara (BPRA), namba ya mlipa kodi (TIN) pamoja na leseni ya biashara.

Alibainisha kuwa washindi watatangazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na watapata fursa ya kushiriki katika tuzo za kitaifa, kikanda na kimataifa zikiwemo za Tanzania Bureau of Standards (TBS), SADC na EAC.
Mbali na kutunukiwa tuzo na vyeti vya ithibati, alieleza kuwa mshindi wa kila kipengele atazawadiwa Shilingi milioni moja za Kitanzania.

“Maombi yanapaswa kuwasilishwa katika ofisi za Taasisi ya Viwango Zanzibar, Maruhubi, Zanzibar au kupitia anuani ya barua pepe: qualityawards@zbs.go.tz.” alisema Suleiman

Akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari Meneja Uhusiano na Masoko ZBS, Aisha Abdulkheir Mohammed alisema kwa mara ya kwanza wameanzisha túzo hizo na kuwa ziitakua endelevu ili kuimarisha utamaduni wa ubora nchini, kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani katika soko la kikanda na kimataifa, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi unaotegemea viwango na ubunifu.

” Hapa tunawalenga wanaozalisha au kuziongezea thamani bidhaa za Zanzibar na kusafirisha nje ya nchi.” Alisema Aisha

Aidha aliwataka wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo inayolenga kuibua ari ya ushindani wa kibiashara unaozingatia ubora, sambamba na kutambua mchango wa wazalishaji, watoa huduma na wajasiriamali wanaotekeleza mifumo ya viwango, vipimo na uthibitishaji katika shughuli zao.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo inatarajiwa kufanyika Mei 20, 2026 katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *