Na Fauzia Mussa
Akiripoti Kutika Mkoa Wa Kaskazini Unguja
ZAIDI ya shilingi milioni nne zimetumika kujenga daraja katika Kijiji cha Garibovu, shehia ya kwa Gube, Jimbo la Mahonda, hatua itakayorahisisha usafiri na usafirishaji kwa zaidi ya wananchi 300 wa kijiji hicho.
Kivuko hicho kinatarajiwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo, hususan wakati wa msimu wa mvua, ambapo mawasiliano yalikuwa yakikatika mara kwa mara kutokana na mafuriko na matope.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda, Mboja Ramadhan Mshenga, alisema ataendelea kushughulikia changamoto za wananchi wake hatua kwa hatua, kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Mboja ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi alibainisha kuwa wakazi wengi wa kijiji cha Garibovu ni wakulima, hivyo kukamilika kwa daraja hilo kutawarahisishia kusafirisha mazao yao kwa wakati kwenda sokoni, kuongeza kipato, pamoja na kuwawezesha kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii katika vijiji jirani bila vikwazo.
“Kama viongozi wa majimbo, tuna wajibu wa kuisaidia Serikali kutatua changamoto ndogondogo zilizo ndani ya uwezo wetu, ili Serikali Kuu ipate nafasi ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Mboja.
Alifafanua kuwa hadi sasa ametumia shilingi milioni nne na laki tatu fedha zake binafsi, na kubainisha kuwa ujenzi huo umefikia asilimia 70 na utaanza kutumika rasmi mara baada ya kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari, mwaka huu.
Aidha, Mboja aliwataka wakazi wa eneo hilo kuendelea kuunga mkono juhudi za viongozi wao kwa kuthamini miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya kijiji na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Kwa Gube, Tatu Zahor Haji, alisema kabla ya kuanza kwa ujenzi huo, wananchi walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kuvuka kwenda upande wa pili, hususan wakati wa mvua kubwa, hali iliyokuwa ikisababisha mawasiliano kukatika kabisa kati ya kijiji hicho na vijiji jirani.
Alieleza kuwa katika kipindi hicho, majanga na maafa mbalimbali yalikuwa yakitokea, ikiwemo vyombo vya usafiri kushindwa kupita na hata kifo kikiwa kimewahi kutokea kutokana na mazingira hatarishi ya eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kwa Gube, Khamis Makame, alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, mijini na vijijini.

Alisema daraja hilo litawasaidia pia watoto wa kijiji hicho wanaosoma Skuli za Kitope na Kazole, hususan katika kipindi cha mvua, kwa kuhakikisha wanavuka salama bila kuhatarisha maisha yao.
Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, wananchi wanaomba Serikali na viongozi wao kuendelea kuwasaidia kwa kurekebisha barabara ya ndani kwa kiwango cha lami, ili kurahisisha zaidi mawasiliano na kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo kwa ujumla.
Kwa upande wake, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Ngwali Ishaka Ngwali, alisema ujenzi wa daraja hilo ni mkombozi mkubwa kwao, akieleza kuwa awali maji yalikuwa yakituama na kusababisha matope mazito yaliyokuwa yakizuia kabisa wananchi kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Kuna kipindi kijana alizama kwenye dimbwi la matope na kupoteza maisha. Hali hiyo ilikuwa ya hatari sana,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati wa mvua kubwa, kina mama walilazimika kuwabeba watoto wao kuvuka, wakiwa wamekunja nguo zao, hali iliyokuwa ikiathiri ustawi na taswira ya kijamii ya eneo hilo, huku wenye vyombo vya usafiri vya magurudumu mawili wakilazimika kuvibeba kutokana na matope mazito.
Daraja hilo linatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo katika Kijiji cha Garibovu kwa kuimarisha usafiri, kuongeza usalama na kuchangia kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo kwa ujumla.
