ZAECA YAWATAKA WANAWAKE WAGOMBEA KURIPOTI VITENDO VYA RUSHA MAPEMA

NA MARYAM NASSOR

MAMLAKA ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) imewataka wanawake wanaogombea nafasi mbali mbali za uongozi kutoa taarifa mapema za vitendo vya rushwa kwani kuna sheria inayomlinda shahidi na mtoa taarifa.

Akizungumza katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa Habari Afisa Elimu na kinga kutoka ZAECA, Yussuf Juma huko katika Afisi za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) Tunguu Unguja.

Amesema, sheria ya ZAECA namba 5 ya mwaka 1992, kifungu cha 98 kinamlinda mtoa taarifa na kifungu cha 99 kinamlinda shahidi, hivyo ikiwa shahidi utapata ulinzi lakini pia ukiwa mtoa taarifa sheria inakulinda.

Amesema , Rushwa ndio kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa , hivyo ni vizuri jamii kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa mapema kabla tukio halijafanyika.

Amesema kuwa, silaha imara dhidi ya rushwa ni kila mtu kujitambua na kujua thamani yake kwa kufuata sheria na kutokuwa tegemezi“ Kesi nyingi tunazozipata huwa zimeshatokea aidha mtu kaahidiwa ajira kakubali kutoa rushwa hatowi taarifa mpaka atakapokosa hiyo ahadi ndipo anakuja kwetu katika hatua za mwisho kabisa” amesema Yussuf.Amesema kuwa, vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi vinatokea lakini taarifa hazifiki kwao “rushwa ya ngono ipo lakini haizungumzwi kwa sababu watu wanaichukulia kama Jambo la kawaida “ amesema .

Aidha amewataka viongozi wanaogombea nafasi mbali mbali za uongozi kufuata sheria na taratibu za nchi na za uchaguzi ili wasiwe wao ndio visababishi vya rushwa. “ Sababu kubwa za kutokea kwa rushwa ni kuvunja sheria na taratibu kwani mtu ili agombee lazima awe na sifa za kugombea “ amasema.

Nae, Mwezeshaji wa mafunzo hayo Asha Abdi Makame amewataka waandishi wa Habari kuwawezesha wanawake kujiamini ili kushiriki na kugombea nafasi za uongozi.Amesema kuwa, kazi kubwa ya waandishi wa Habari ni kuibua na kutetea haki za wanawake, hivyo ni vizuri kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa wanawake kugombea nafasi za uongozi.“ Jamii bado haina uwelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa wanawake kuwa viongozi, hivyo ni vyema waandishi wa habari kuandika Makala na Habari za wanawake waliofanya vizuri kwenye uongozi ili waonekanae “ ameshauri .

Nao baadhi ya waandishi walibahatika mafunzo hayo, Maryam Naasor amewashauri waandishi wachanga waliopata mafunzo hayo, kujitoa zaidi ili kufanikiwa katika kazi zao.Amewataka waandishi hao , kushirikiana na waandishi wengine ambao wapo katika mradi huo ili kupata urahisi wa kazi zao.Awali mafunzo hayo, yalifunguliwa na Afisa program wa mafunzo hayo ya waandishi wa Habari wachanga (Young Media Fellows) Tatu Ali ambapo aliwataka waandishi wa mradi huo kuendelea kuandika Habari za wanawake na uongozi hasa kipindi kinachoelekea cha uchaguzi.

Mafunzo hayo ya siku moja , yamewashirikisha waandishi wa Habari 14 wa unguja kutoka vyombo mbali mbali vya Habari nchini ikiwa ni muendelezo wa mradi wa YMF kutoka TAMWA ZNZ.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *