WATUHUMIWA 17 WA WIZI WA PIKIPIKI WAKAMATWA NA POLISI ZANZIBAR

Na Fatma Rajab

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watuhumiwa 17 wanaodaiwa kuhusika na makosa ya wizi wa vyombo vya moto vilivyoibwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kuuzwa ndani na nje ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kinachofanyika kila mwezi ofisini kwake Madema mkoa wa Mjini Magharibi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib Richard Thadeo Mchomvu ameeleza kuwa mnamo tarehe 24 Septemba 2025, Jeshi hilo lilianzisha operesheni maalum iliyolenga kuwakamata wezi wa pikipiki pamoja na wahalifu wengine wanaohusishwa na makosa mbalimbali ya jinai.

Kupitia operesheni hiyo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 17 na kupata pikipiki 23, injini moja ya Vespa na bodi ya Vespa ambazo ziliibwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo,Pikipiki zilizopatikana ni aina ya TVS 19, Click 2 na Vespa 2.

Kamanda wa Polisi amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakiiba pikipiki na kisha kuziuza kwa bei nafuu kati ya shilingi laki moja hadi laki nane kwa watu wanaopokea vyombo hivyo vya wizi.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini mtandao mzima wa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kihalifu na kuhakikisha wote wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.‘’ Tunendelea na uchunguzi ili kuwakamata watuhumiwa wengine waliotoroka au kuhusika kwa namna yoyote katika matukio haya,” alisema Kamanda Mchomvu.

Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na wanunuaji wa pikipiki za wizi akiwemo Suleiman Ramadhani Mwinyi maarufu Eddo mwenye umri wa miaka 27 mkazi wa Magogoni, Thabit Mohd Zuberi maarufu Thabi mwenye miaka 19 mkazi wa Chuini, Sharifu Juma Hamadi maarufu Mwarabu mwenye miaka 31 mkazi wa Chunga Fuoni, Juma Mohd Chuma mwenye miaka 33 mkazi wa Amani Fresh, na Abdul-Rahman Mussa mwenye miaka 25 mkazi wa Kwa Mchina Mwisho.

Kwa upande wa wezi wa pikipiki waliokamatwa ni pamoja na Abrahamani Juma Shaibu maarufu Man Mdogo mwenye miaka 20, Alkram Haji Ali maarufu Kasongo mwenye miaka 19, Abubakari Mussa Kifani maarufu Abuu mwenye miaka 22, Khamisi Juma Hassan mwenye miaka 21, Nasri Suleiman Abdalah mwenye miaka 20, Hassan Said Hassan maarufu Kaba mwenye miaka 30, Said Masoud Omary maarufu Fela mwenye miaka 31, Juma Khamisi Juma maarufu Kiboring mwenye miaka 31, Mohd Khamisi Juma mwenye miaka 24 na Abdilah Khamisi Othman maarufu Folani mwenye miaka 23.

Wengine wawili waliokamatwa ambao wanajihusisha na wizi pamoja na ununuzi wa pikipiki hizo za wizi ni Khamis Abdalah Juma maarufu Bata Boy mwenye miaka 23 na Abrahman Yussuph Mmadi maarufu Kipanya mwenye miaka 20.

Jeshi la Polisi limezitaja baadhi ya pikipiki zilizopatikana kuwa ni Click mbili zenye rangi nyeupe, Vespa mbili zenye rangi nyeusi na choklate, pamoja na pikipiki 19 aina ya TVS zenye namba mbalimbali za usajili ikiwemo Z.513 KW, Z.931 PS, Z.443 NM, Z.899 PY, Z.546 NJ na nyengine ambazo hazina namba za usajili.

Aidha Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa mapema pale wanapohisi kuwepo kwa vitendo vya uhalifu katika maeneo yao ili kusaidia kudhibiti wimbi la wizi wa vyombo vya moto na makosa mengine ya kijinai.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *