WATU WASIOJULIKANA WAFANYA UHARIBIFU WA MAZAO YA WANAWAKE BUNGI, SHEHA ATOA UFAFANUZI

Na Abdul Sakaza, Bungi – Kusini Unguja.

Wakulima Wanawake kutoka Shehia ya Bungi, Mtaa wa Magurueni, wamewalalamikia watu wasiojulikana kuvamia mashamba yao na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao yao, yakiwemo migomba, mihogo na mazao mengine ya chakula.

Tukio hilo, ambalo limetokea mwezi uliopita  limezua taharuki kubwa katika jamii, huku wanawake wakiwa waathirika wakubwa wa  uharibifu huo na kusema kitendo hicho  kimewarudisha nyuma kimaendeleo na kuwaacha katika hali ya mshangao wa hali ya juu.

Akizungumza kwa uchungu mbele ya waandishi wa habari  na maafisa wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania Zanzibar TAMWA  Bi. Majida Abdalla mwenye umri wa 40  na mmoja wa waathirika wakuu wa tukio hilo, alisema uharibifu huo umefanywa kwa makusudi na bila huruma, jambo ambalo linavunja moyo wa wakulima wadogo hasa wanawake wanaojitafutia riziki kwa jasho lao. “Nilifika shambani asubuhi nikakuta migomba na mihogo yangu yote imekatwa na  mihogo imeng’olewa,  Nilishindwa kujizuia nililia kwa uchungu. Tumepoteza mazao tuliyoyatunza kwa muda mrefu, na hadi sasa hatujui ni nani aliyetenda haya,” alisema kwa huzuni Bi. Majida.

Naye Bi. Asha Juma, miaka 50 mkulima mwingine katika eneo hilo, alisema uharibifu huo si wa mara ya kwanza kutokea, kwani miezi michache iliyopita walishuhudia tukio kama hilo, lakini safari hii limekuwa kubwa zaidi na limeathiri mashamba ya wanawake wengi. “Kila siku tunaamka mapema kwenda kulima tukiwa na matumaini ya kupata chakula cha familia na kipato. Lakini sasa tumevurugwa. Inasikitisha kuona mazao ya migomba na mihogo yote ikikatwa bila sababu yoyote ya msingi,” alisema Bi. Asha.

Kwa mujibu wa wakulima hao, eneo walilolima ni sehemu ambayo kwa muda mrefu limekuwa likitumika na wananchi wa shehia hiyo kwa shughuli za kilimo cha chakula, lakini hivi karibuni kumekuwa na madai kwamba eneo hilo ni mali ya Chuo cha Kijeshi kilichopo Bungi.

WANAWAKE WALIOPATIWA MAFUNZO WATHIBITISHA HASARA ILIYOJITOKEZA

Bi. Mwanaidi Omar, mkulima mwingine aliyekumbwa na uharibifu huo, alisema wanawake wengi walijikusanya na kuanzisha mashamba ya pamoja baada ya kupata mafunzo ya kilimo mseto kupitia mradi wa Women Leadership in Adaptation (ZanzAdapt) unaotekelezwa na Taasisi ya Community Forest Pemba (CFP) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ). “Tulipewa miche ya migomba  kupitia mradi huo wa ZanzAdapt kutoka CFP, na mengine tulinunua wenyewe. Tuliamua kulima mashamba ya pamoja ili kujipatia kipato na kusaidiana kijamii. Lakini sasa jitihada zetu zote zimeharibika kutokana na tukio hili,” alisema kwa uchungu Bi. Mwanaidi huku akionyesha mazao yaliyoharibiwa.

Aidha, Mzee Ali Haruna, mkazi wa muda mrefu wa eneo hilo, alithibitisha kuwa eneo la kilimo lililoathirika ni sehemu ya ardhi inayomilikiwa na Chuo cha Kijeshi cha Bungi, ingawa wananchi wamekuwa wakilitumia kwa shughuli za kilimo kwa muda mrefu bila migogoro. “Ni kweli eneo hilo ni la chuo cha kijeshi, lakini wananchi wamekuwa wakilima hapo kwa muda mrefu. Pengine tatizo limetokea kutokana na ukosefu wa mawasiliano kati ya wananchi na uongozi wa chuo,” alisema Mzee Haruna.

Sheha wa Shehia ya Bungi, Bw. Vuai Ramadhani Vuai , amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tayari alifika eneo la tukio na kuona uharibifu uliotokea hasa ikiwemo migomba, mihogo na mazao mengine.“Ni kweli kumetokea uharibifu wa mazao katika eneo la Magurueni. Tumepokea malalamiko kutoka kwa wakulima, hasa wanawake. Nimezungumza na baadhi ya watu wanaotuhumiwa na kwa sasa tayari tumeshakaa kikao cha pamoja na muafaka tayari umeshapatiana ” alisema Sheha wa shehia ya Bungi.

Ameweka bayana kuwa eneo ambalo akinamama wamelima ni eneo tengefu la chuo hicho cha kujeshi na haliruhusiwi kwa shughuli za kilimo na huenda baadhi ya wananchi hawakuwa na taarifa sahihi juu ya mipaka yake.

Katika hatua nyengine sheha wa eneo hilo aliongeza kua hakutakua na fidia wala malipo ya uharibifu huo kwani eneo hilo ni eneo la chuo cha kijeshi “hakutakua na fidia bali pande zote mbili zinapaswa kusameheana kwasababu eneo sio la kilimo ” alisema Sheha.

Aidha, Sheha huyo ameahidi kwamba ofisi ya shehia itachukua hatua za haraka kuhakikisha suluhisho la kudumu linapatikana ili changamoto hii isije kujitokeza tena “Tutaandaa kikao cha pamoja kitakachowahusisha viongozi wa kijeshi, wananchi, na serikali ya shehia. Lengo ni kupata suluhisho la kudumu” alisema sheha.

Kwa upande mwingine, wanawake wa Bungi wametoa wito kwa serikali ya wilaya na taasisi zinazohusika na masuala ya ardhi na kilimo kuingilia kati mgogoro huo kwa haraka ili kulinda haki za wakulima wadogo.

Bi. Halima Salum, miaka 49 na mkulima kiongozi wa wanawake  Bungi, alisema uharibifu huo umeathiri zaidi wanawake wajane na wale wanaotegemea kilimo kama njia pekee ya kujikimu. “Kuna wajane, kuna wanawake waliotelekezwa na familia zao, wote hawa wanategemea kilimo cha migomba na mihogo ili wapate chakula na ada za watoto. Sasa wamebaki bila chochote. Serikali itusikilize, tusikandamizwe kwa kisingizio cha mipaka,” alisema Bi. Halima.

Aliongeza kuwa jamii ya wanawake wa Bungi imekuwa ikijitahidi kupambana na changamoto za kiuchumi kupitia kilimo, lakini matukio ya aina hii yanawakatisha tamaa na kuwakosesha imani kwa viongozi.

Mdau  wa mazingira na kilimo kutoka eneo la Kusini Unguja ambae alitaka kufichwa utambulisho wake wameitaka serikali kuhakikisha inawalinda wakulima wadogo dhidi ya migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara kati ya wananchi na taasisi za umma.

Mtaalamu huyo ameongeza   migogoro kama hii inahitaji usuluhishi wa haki na wa haraka kabla haijazua migawanyiko katika jamii. “Hatuwezi kuendeleza kilimo ikiwa wakulima hawana uhakika wa ardhi. Serikali inapaswa kuweka utaratibu wa wazi wa umiliki wa maeneo ili wananchi wasipoteze haki zao,” alisema

Kwa sasa, wakulima wa Magurueni wanasema bado wanaendelea kufuatilia hatima ya tukio hilo kupitia ofisi ya sheha “Tunataka suluhisho la kudumu. Kama eneo ni la kijeshi, basi tupewe sehemu nyengine ya kulima. Tusipigwe na njaa kwa sababu ya mgogoro wa ardhi,” alisema Bi. Majida kwa sauti ya uchungu.

Tukio la uharibifu wa mazao katika Shehia ya Bungi limeacha maumivu makubwa kwa wakulima, hasa wanawake wanaotegemea kilimo kama nguzo ya maisha yao,Wengi sasa wanaiomba serikali kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha haki inapatikana, migogoro ya ardhi inazuiliwa, na wanawake wakulima wanapatiwa nafasi ya kuendelea na shughuli zao kwa amani na uhakika wa kipato.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *