WAANDISHI WAASWA KUZINGATIA MAADILI YA UTANGAZAJI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU.

NA FAUZIA MUSSA

TUME ya Utangazaji Zanzibar (TUZ) imewataka waandishi wa habari na vyombo vya utangazaji kuzingatia maadili ya taaluma yao kuelekea uchaguzi mkuu ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na amani na utulivu.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Suleiman Ame Khamis, akifungua semina kuhusu maadili ya utangazaji kwa waandishi wa habari, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni mjini unguja, alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu la kutoa habari kwa umma, lakini kwa njia inayozingatia sheria na weledi wa taaluma.“Kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maadili ya utangazaji, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, ili kulinda amani ya nchi yetu,” alisema.

Alieleza kuwa tayari vyama vya siasa vimeanza kutambulisha wagombea wao na kampeni zinatarajiwa kuanza hivi karibuni, hivyo waandishi wanapaswa kuepuka kushiriki katika upotoshaji au kutumiwa kueneza propaganda za chuki.“Nchi nyingi zilizoshuhudia machafuko ya kisiasa, vyombo vya habari vilihusika kwa namna moja au nyingine. Nawasihi msikubali kutumiwa kama majukwaa ya uchochezi,” aliongeza.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Hiji Dadi Shajak, alisisitiza kuwa waandishi wa habari ni watu muhimu hasa katika kipindi cha uchaguzi, lakini hawapaswi kutumia nafasi hiyo kuvuruga amani.“Mafunzo haya yamekusudiwa kuwakumbusha wajibu na maadili ya uandishi hasa katika kipindi hiki nyeti. Taarifa za uchaguzi lazima ziwe sahihi na zisichochee mgawanyiko,” alisema.

Mapema alieleza kuwa Tume imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika kuimarisha usalama wa habari na kuhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa wakati wote zinazingatia sheria na miongozo ya maadili ya utangazaji.

Akitoa mada kuhusu kanuni za huduma za utangazaji wakati wa uchaguzi, Ofisa Sheria kutoka Tume ya Utangazaji, Khadija Mabrouk Hassan, alibainisha kuwa vyombo vya habari vinapaswa kutoa taarifa zisizo na uchochezi, ubaguzi au kashfa, bali virejee katika sera na ilani za vyama bila upendeleo wowote.“Taarifa zisiwe za kichochezi wala kuonyesha upendeleo. Na ni Tume ya Uchaguzi pekee yenye mamlaka ya kutangaza matokeo rasmi,” alisisitiza.

Alieleza kuwa watoa huduma za maudhui hawaruhusiwi kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi na wasimamizi wa uchaguzi, kutoa taarifa zozote za kupotosha au kuchochea vurugu na kutoa maoni binafsi yanayohusu uchaguzi wakati wanatangaza.

Aliwakumbusha waandishi kuwa ni marufuku kutoa maoni binafsi katika habari za uchaguzi, na kwamba wale wenye mgongano wa kimaslahi hawaruhusiwi kushiriki katika kuhariri au kutangaza kipindi chote cha uchaguzi.Kwa mujibu wa Khadija, mwandishi atakayekiuka kanuni hizo anaweza kutozwa faini ya shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi 12, au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Aidha, alikumbusha kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuwasilisha mpango kazi wa vipindi watakavyotoa kuelekea uchaguzi kwa tume ili kuepuka uvunjifu wa sheria.Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, akitoa mada ya mwongozo wa utangazaji wakati wa machafuko na majanga yanayoweza kutokea kipindi cha uchaguzi alieleza kuwa ingawa vurugu hazitarajiwi kutokea lakini waandishi wanapaswa kuwa tayari kukabiliana na hali yoyote.

Alikumbusha kuwa historia inaonyesha jinsi vyombo vya habari vilivyohusishwa moja kwa moja na machafuko makubwa katika baadhi ya nchi.“Katika uchaguzi wa Nigeria mwaka 2007, watu zaidi ya 1000 walipoteza maisha na wengine 600,000 walikosa makazi, huku waandishi wakitajwa kuchangia hali hiyo kupitia habari zenye kuchochea,” alisema.

Kisaka alisema waandishi wanapaswa kutumia taaluma zao kulinda amani, kuepuka kuripoti taarifa zisizohakikiwa, na kutotangaza habari za moja kwa moja wakati wa machafuko bila uangalizi wa wahariri wakuu.“Taarifa zisizohakikiwa ni chanzo cha migogoro. Uongo, uvumi na upotoshaji ndio chimbuko la vurugu nyingi,” aliongeza.

Alisema vyombo vya habari vina wajibu wa kukemea na kurudia kulaani vitendo vyovyote vya chuki au uchochezi, na kuelekeza nguvu kwenye taarifa zenye kusaidia jamii badala ya kulaumu.

Washiriki wa mafunzo hayo walisema yamekuja kwa wakati muafaka na yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi katika kipindi hiki muhimu kwa mustakabali wa taifa.”Habari zetu lazima zijenge, si kubomoa,” alisema mmoja wa washiriki.

Semina hiyo ya siku moja imendaliwa na Tume ya Utangazaji Zanzibar (TUZ)kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)Semina hiyo ikiwahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya serikali, binafsi na wazalishaji wa maudhui mtandaoni kutoka Unguja, huku ikielezwa kuwa mafunzo kama hayo pia yatafanyika kisiwani Pemba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *