NA FAUZIA MUSSA
TAASISI ya ‘Together for Samia’ kwa kushirikiana na kundi la hamasa la ‘hatuna mbadala’, wameungana na Serikali kulaani vikali maudhui yaliyoenezwa katika mitandao ya kijamii Oktoba 4, 2025, yakionyesha watu wanaodaiwa kuwa wanajeshi wakihamasisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiingiza katika siasa kupitia mapinduzi.
Akizungumza baada ya vijana wa makundi hayo kutuma ujumbe wa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na kuhamasisha amani kupitia vijana wa makachu Forodhani, kiongozi wa Taasisi ya ‘Together for Samia’ Slim Salim Mohammed, aliwaomba vijana nchini kutokubali kutumiwa vibaya na wanasiasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kwa lengo la kuichafua amani iliyopo nchini.

Alisema ni jukumu la kila kijana kulinda amani na mshikamano wa Taifa, kwani bila amani hakuna shughuli za maendeleo zinazoweza kufanyika na kuwaomba watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza au kutumia maudhui ya uchochezi, kwani yanaweza kuhatarisha umoja na amani ya Taifa.“Tukio hili limekusudia kumpa moyo na ari Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aendelee na juhudi zake za kuwaletea maendeleo Watanzania. Vijana tunapaswa kuwa walinzi wa amani, si chachu ya vurugu,” alisema Slim.
Alibainisha kuwa wameamua kutumia vijana wa makachu kutokana na uwezo wao mkubwa wa kuifikia jamii kwa haraka kupitia mitandao ya kijamii, hivyo kusaidia kufikisha ujumbe chanya wa amani na mshikamano.

Kwa upande wake, mwakislishi wa kundi la hatuna mbadala, Nanaa Hassan, alisema wameungana na Together for Samia kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuwaletea Watanzania maendeleo, huku wakipinga vikali vitendo vya vijana wachache wanaotumika kudhalilisha au kubeza juhudi hizo.“Kama vijana, tunachukizwa na wale wanaokubali kutumiwa vibaya kutengeneza maudhui ya uchochezi. Badala yake, tutumie nguvu zetu kuelimisha, kuhamasisha na kuunga mkono juhudi za maendeleo,” alisema Nanaa.

Ameir Sleiman Rashid, kutoka kundi la Makachu Forodhani, alisema vijana wao wataendelea kutumia sanaa, michezo na ubunifu kueneza ujumbe wa amani na maendeleo, sio tu kipindi cha uchaguzi, bali hata katika maisha ya kila siku.Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania imeendelea kuwa mfano wa demokrasia ya amani barani Afrika, huku chaguzi zikiendeshwa kwa utulivu na wananchi wakiwachagua viongozi wao kupitia sanduku la kura.
