Na Abdul Sakaza,
Akiripoti Kutoka Bungi/Unguja Ukuu
Unguja Ukuu na Bungi, vijiji viwili vya pwani ya Kusini Unguja, vina historia ndefu ya kilimo, uvuvi na biashara ndogo ndogo za kijamii,Hata hivyo, changamoto za kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi na kupanda kwa gharama za maisha zimewalazimisha wanawake kuibua mbinu mpya za kujikwamua, Njia waliyoipata ni ile isiyotarajiwa na wengi usarifu wa achari za matunda na mboga mboga.
Achari hizi si tu zimekuwa ladha tamu mezani, bali pia zimegeuka kuwa daraja la kiuchumi linalowasaidia wanawake hawa kulipa ada za watoto wao, kugharamia huduma za afya na kupunguza utegemezi wa kipato cha wanaume pekee.
MWANZO WA SAFARI KUTOKA JIKO LA NYUMBANI HADI SOKO LA MJINI
Katika kikundi cha “Nguvu kazi kwa pamoja” Mwanzo wake ulikuwa mdogo,Wanawake wachache walikusanyia na kujaribu kutengeneza achari kwa kutumia maembe mabichi,mbirimbi,piipili na mchanganyiko mwengine,Walijaribu kwa kutumia chupa za plastiki zilizopatikana majumbani,Hata hivyo, ladha nzuri na mapendekezo kutoka kwa majirani yaliwapa ujasiri wa kuanza kuuza kwa wingi zaidi. “Tulianza kidogo tu, kila mmoja alitoa kilo mbili tatu za maembe. Tukazipika kwa mafuta na viungo, tukazitia kwenye chupa. Nilipopeleka sokoni jumbi , zikaisha haraka. Hapo nikajua huu ni mwanzo wa biashara mpya,” anasema Mosi Juma Denge Mwenyekiti wa kikundi cha nguvu kazi kwa pamoja kinachotengeneza achari Unguja Ukuu

Sasa bidhaa zao zimeongezeka , Wanaandaa achari ya maembe, mbirimbi , karoti, pilipili hoho na nyanya,Achari ya nyanya, maarufu kama tomato pickle, imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutokana na ladha yake tofauti na urahisi wa kutumia kama kitoweo. Mwazo tuliuza kwa chupa za kawaida ila mafuzo tulioyapata kupitia mradi wa woman leadership in adaption zanzadapt kutoka CFP yalitupa mabadliliko makubwa kwani sasa tunajua jinsi ya kuhifadhi bidhaa zetu kwenye chupa maalum ili zisiharibike haraka wala kupoteza ubora”Sasa tumekua wenye matumaini makubwa kuhusu ujasiriamali na ubunifu “alisema Mosi
MAFUNZO YALIYOLETA MABADILIKO
Siri ya mafanikio haya haikuishia tu kwa ubunifu wa wanawake hawa, Community Forests Pemba (CFP) kupitia mradi wa Zanzibar Women Leadership in Adaptation (ZanzAdapt) waliwaona wanawake hawa na kuwawezesha kupata mafunzo ya kisasa ya usarifu wa mazao.
Kupitia mafunzo hayo, walijifunza Usafi na usalama wa chakula ili kuhakikisha achari inakubalika sokoni,Mbinu za kuongeza thamani ya mazao kama vile kuongeza mchanganyiko wa nyanya na pilipili ili kudumu kwa muda mrefu,Ufundi wa vifungashio vinavyovutia zaidi wanunuzi, wakiwemo watalii,Masoko ya kidigitali kwa kutumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii.“Hapo awali tulikuwa tunatengeneza achari bila viwango. Wengine walitumia chupa zisizo salama, wengine walihifadhi vibaya. Lakini kupitia CFP, tumejifunza namna ya kuandaa achari kwa usafi, kwa vipimo na kwa vifungashio vizuri. Hii imetufanya tusimame kibiashara,”anafafanua doto Daniel kutoka Bungi.
Kwamujibu wa Lillian simule meneja masoko kimataifa anasema mradi huu umewawezesha wanawake kujikwamua na umasikini na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani mazao yao ambayo mwazo yaliharibika kutoka na athari za kimazingira saaa yana sarifiwa na kua bidhaa mpya Pia ameongeza kua wametoa mafuzo ya kuuza bidhaa kidijitali kupitia Mitandao ya Kijamii kama Facebook, WhatsApp, Instagram na Tiktok .

Kwa sasa, vikundi vya wanawake Unguja Ukuu na Bungi vimeunda ushirika mdogo,Wanakutana kila wiki kupanga kazi, kukusanya mazao kutoka mashamba na kuyasindika kwa pamoja. Mapato ya kila mwanakikundi yameongezeka kwa kiwango cha kuvutia na kila mwezi baadhi ya vikundi hulipana mshahara wa kila mwanakikundi elfu 50,Wapo waliokuwa hawana uwezo wa kumpeleka mtoto shule , sasa wanaweza kulipa ada na kununua sare nakuendesha maisha yao ya kila siku bila ya kutegemea kipato cha mwanamme. “Mimi nilikuwa natumia muda mwingi kuwaomba ndugu msaada wa pesa za matibabu. Lakini sasa ninaweza kujitegemea. Hata mume wangu anajivunia, kwa sababu pesa ninazopata kutoka kwenye uuzaji wa aachari zinasaidia familia,” anasema Fatma Khamis, mwanakikundi kutoka Unguja Ukuu.
Pamoja na hayo, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar TAMWA, pia kimekuwa bega kwa bega na wanawake hawa, ikiwajengea uwezo wa uongozi kupitia mafunzo ya jinsi ya kusimamia vikundi, kuendesha mikutano na kushiriki maamuzi ya kijamii,Kupitia kampeni zao za kijinsia, wanawake wa Unguja Ukuu na Bungi sasa wanatambulika kama viongozi wa vikundi na sio wafuasi tu, jambo ambalo limeongeza heshima yao ndani ya jamii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar, Dr Mzuri Issa anasema kuwekeza kwa wanawake ni sawa na kuwekeza kwa familia na jamii nzima. “Tunataka wanawake wasibakie nyuma. Wanawake wa Unguja Ukuu na Bungi wameonesha kuwa wanaweza kuongoza sio tu familia zao, bali pia kulinda rasilimali za taifa,” alisema.
UJASIRIAMALI UNAVYOKABILIANA NA MABADLILIKO YA TABIA NCHI
Wakati wa misimu ya mavuno, matunda na mboga nyingi zilikuwa zinaharibika shambani kutokana mabadiliko ya tabia nchi na ukosefu wa masoko,Sasa wanawake wanayachuma mapema na kuyasindika kuwa achari kabla hayajaoza.

Kwa njia hiyo, wanapunguza upotevu wa chakula na taka za mazao shambani,Zaidi ya hayo, CFP imeunganisha mafunzo haya na elimu ya uhifadhi wa mikoko na rasilimali za pwani,Wanawake wanahimizwa kuendeleza biashara zinazohusiana na mazingira bila kuharibu misitu au bahari.
Licha ya mafanikio haya, changamoto bado ni nyingi ikiwemo Mitaji midogo , wanawake wengi hutegemea mikopo midogo ya vikoba ambayo haitoshi kuzalisha kwa kiwango kikubwa.
Vifaa vya kuhifadhia ukosefu wa jokofu na vifaa vya kuziba chupa kwa ubora wa kimataifa,Pia Uhaba wa vifungashio bora mara nyingi hulazimika kutumia chupa zilizotumika, jambo linalopunguza mvuto kwa wanunuzi wa kimataifa.
Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, Ali ameir ujasiriamali wa aina hii ni mfano bora wa jinsi wanawake vijijini wanavyoweza kuongoza mapambano ya kiuchumi na kijamii. “Mradi wa CFP kupitia ZanzAdapt siyo tu unawajengea wanawake kipato, bali unawapa nafasi ya uongozi. Wanawake hawa sasa wanahusiana moja kwa moja na maamuzi ya kijiji kuhusu matumizi ya ardhi na rasilimali,” alisema afisa huyo.

Wanawake wa Unguja Ukuu na Bungi wanasema wana ndoto kubwa ya kuona achari zao zikifika masoko ya Afrika Mashariki na hata Ulaya, Wanaamini kwamba iwapo serikali na wadau binafsi watawaunga mkono kwa mitaji na masoko, bidhaa zao zitakuwa moja ya nembo za Zanzibar. “Tunataka siku moja mtu akitaja Zanzibar, asifikirie tu viungo vya karafuu, bali pia afikirie achari zetu. Hii ndiyo dira yetu,” anasema kwa matumaini Mwanahamisi Suleiman.
Kile kilichoanza kama jaribio la kupika achari jikoni kimegeuka kuwa mapinduzi ya kiuchumi kwa wanawake wa Unguja Ukuu na Bungi,Kupitia msaada wa Community Forests Pemba (CFP) chini ya mradi wa ZanzAdapt, wanawake hawa si tu wamejijengea uwezo wa kifedha, bali pia wamepewa nafasi ya kushiriki katika kulinda mazingira na kuongoza mabadiliko ya kijamii.
