Na Abdul Sakaza , UNGUA UKUU – ZANZIBAR
Umasikini umeendelea kuwa sababu kubwa ya ukataji wa mikoko katika kijiji cha Unguja Ukuu, kilichopo wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Wakazi wengi wa kijiji hiki wanategemea mikoko kama chanzo cha kipato kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kata ya Unguja Ukuu Kaepwani ina wakazi 2,330, huku kata ya Unguja Ukuu Kaebona ikiwa na wakazi 1,788 lakini licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu, hali ya kiuchumi ya kijiji hichi bado ni changamoto, jambo linalochochea matumizi yasiyo endelevu ya mikoko.
Umasikini na Ukataji wa Mikoko
Kutokana na ukosefu wa fursa za ajira na vyanzo mbadala vya kipato, wakazi wengi wa Unguja Ukuu wamegeukia ukataji wa mikoko kama suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu kupitia maisha yao .
Miti hii hukatwa kwa ajili ya kuni na utengenezaji wa mkaa, ambayo huuzwa ili kupata fedha za kugharamia mahitaji ya kila siku kama vile chakula, madaftari ya shule kwa watoto wao, fomu za shule, na hata nguo za sikukuu. “Tunakata mikoko kwa sababu hatuna njia nyingine ya kupata kipato,Familia yangu inategemea kuni na mkaa ili tuweze kununua chakula na mahitaji ya shule kwa watoto,” anasema Bi Amina Suleiman, mkazi wa Unguja Ukuu.
Takwimu za kijiji zinaonyesha kuwa kipindi cha mwezi wa Ramadhani ndicho kinachoshuhudia ukataji mkubwa wa mikoko, kwani mahitaji ya kuni huongezeka kwa ajili ya maandalizi ya futari na daku hali Hii inazidisha uharibifu wa mazingira, huku maeneo mengi ambayo awali yalikuwa na mikoko minene sasa yakibaki wazi.
Utamaduni na Matumizi ya Mikoko Kama Nishati
Mbali na hali ngumu ya kiuchumi, utamaduni pia umechangia katika ukataji wa mikoko,Baadhi ya wanaume katika jamii ya Unguja Ukuu wanapendelea kuni za mikoko badala ya gesi kwa kupikia wakiamini kuwa chakula kinapopikwa kwa kuni kinakuwa na ladha bora zaidi.“Gesi siyo nzuri kwa baadhi ya vyakula vya asili kama muhogo na ndizi Kuni za mikoko zinatoa ladha tofauti,” anasema Juma Ameir, mmoja wa wakazi wa eneo hilo , Hali hii imeendeleza matumizi ya mikoko kama kuni, licha ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama gesi na majiko sanifu.
Athari kwa Mazingira na Jamii

Ukataji wa mikoko umeleta athari kubwa kwa mazingira ya Unguja Ukuu,Mikoko ni muhimu kwa kudhibiti mmomonyoko wa ardhi, kutoa makazi kwa viumbe wa baharini, na kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kupungua kwa misitu ya mikoko kumeathiri pia shughuli za uvuvi, kwani baadhi ya samaki wanategemea mikoko kama sehemu ya kuzaliana. “Mikoko inatusaidia kupunguza mawimbi makubwa na kulinda ufukwe, lakini sasa miti mingi imekatwa na athari zake zinaonekana,” anasema Mzee Haji Ali, mvuvi wa muda mrefu katika kijiji cha Unguja Ukuu.
Wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, jamii hii itaathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, hasa kuongezeka kwa kina cha bahari na upotevu wa viumbe wa baharini.
Mariam abrahman juma Ni afisa wa mazingira kutoka Taasisi ya Zanzibar Climate Change Alliance (ZACCA) ameielezea athari za mabadiliko ya tabianchi kama changamoto kubwa inayozidi kuathiri mazingira na maisha ya watu, hasa katika maeneo ya pwani ya Zanzibar na kuongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yameleta mabadiliko katika mifumo ya mvua, ambapo mvua zimekua hazina miongo maalumu pamoja na kuongezeka kwa joto duniani, hali inayochangia kuongezeka kwa maafa mbali mbali duniani na kwa kiasi kikubwa huchangiwa na ukataji wa mikoko
Jitihada za Kuhifadhi Mikoko

Katika juhudi za kupambana na uharibifu wa mikoko, mashirika mbalimbali yameanzisha miradi ya kutoa elimu kwa jamii na kutafuta njia mbadala za kipato, hivi karibuni kumeazishwa Mradi wa (ZanzAdapt ) umekuwa ukiwapatia wanakijiji wa Unguja Ukuu mafunzo kuhusu athari za ukataji wa mikoko na kuwahamasisha kutumia njia mbadala za kujipatia kipato kama ufugaji wa kaa nyuki na uvuvi endelevu.“Tunahimiza jamii kupanda mikoko na kuwekeza katika miradi mbadala ya kiuchumi ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa,” anasema Mbarouk Mussa Omar mkurugenzi wa Jumuiya ya Misitu Pemba (Community Forest Pemba, CFP)kupitia mradi wa ZanzAdapt
Kwa upande mwingine, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) kimekuwa kikihamasisha wanawake wa Unguja Ukuu kujitokeza kama viongozi wa harakati za kuhifadhi mikoko na kuchukuajukumu la kujitolea katika kuimarisha na kuirejesha mikoko iliyotoweka.“Wanawake wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira, kwa kuwa wao ndio watumiaji wakubwa wa kuni,Ikiwa watachukua nafasi za uongozi katika harakati hizi, tunaweza kuona mabadiliko chanya,” anasema dokta mzuri issa mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar wakati wa ufu guzi wa mradi huu.
Suluhu ya kuacha kukata mikoko Unguja Ukuu kwa sababu ya umasikini inaweza kuondoka ikiwa kutakua na mashirikiano na utoaji wa elimu kwa jamii hii na Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kuanzisha mifuko ya mikopo au msaada wa kifedha kwa familia za pwani ili kusaidia kupunguza utegemezi wa mikoko jambo ambalo litawapa wananchi njia mbadala za kipato na kupunguza shinikizo la kukata mikoko ili kupata fedha.
Kadhalika Kuanzisha mifumo ya Uwezeshaji wa Wanawake na Vijana Ikiwemo kuanzisha biashara za mazingira, kama vile utalii wa mikoko, ambavyo vitawawezesha kujipatia kipato pasipo kuathiri mazingira kwani mifumo hii inaweza kufundisha ustadi wa biashara, kilimo cha mikoko endelevu, na ufugaji wa samaki pamoja na kutolewa kwa mitungi ya gesi yakupikia ya kutosha pamoja na kutolewa elimu kuhusu utumiani wa nishati mabadala ya kupikia ili kuiweka mikoko katika hali ya usalama
