Waumini wa dini ya kiislamu wametakiwa kujitolea kuwekeza katika mambo ya kheri ikiwemo kujenga misikiti, madrasa , sambamba na kuitumia katika kutatua changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika vijiji vyao.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al-hajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika ufunguzi wa Masjid TAIBAH Uliopo FUONI MAMBOSASA Wilaya ya Magharibi “ B” Unguja

Amesema kuwa kila mmoja kwa nafsi yake anapaswa kufanya mambo mema yatakayosaidia kufikia lengo la kuumbwa kwake hapa duniani ikiwemo kujenga msikiti, kuchimba visima, kujenga madrasa nayale yote ambayo ni sadakatuljaria kwa umma.
Alhajj Hemed amefahamisha kuwa katika jamii kumekuwa na changamoto mbali mbali hasa kwa upande wa vijana hivyo ni wajibu wa wamumini wa maeneo hayo na maeneo jirani kuutumia msikiti huo kufanyia ibada na kupeana elimu ambayo itawasaidi kufanya ibada kwa uhakika na kuandaa mazingira mazuri ya kesho akhera.

Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. MAHMOUD MUSSA WADI amewataka viongozi wa misikiti kuacha tofauti walizonazo katika suala zima la usimamizi wa misikiti pamoja na kushirikiana katika kufanya ibada jambo ambalo litapelekea kuvurithisha mambo mema vizazi vinavyokuja.
Akisoma risala ya ujenzi wa msikiti huo Mkurugenzi wa taasisi ya AL-NOOR CHARITABLE AGENCY FOR NEEDY ambayo ndio wafadhili wakuu wa msikiti huo Sheh NADIR MOH’D MAHFOUDH amesema kuwa taasisi yao imeshajenga misikiti 42 hadi sasa kwa lengo la kusaidia jamii kufanya ibada na kutoa elimu sehemu sahihi.

Sheikh Nafir amewataka waumini wa msikiti huo kuutumia katia suala zima la kufikisha elimu kwa vijana sambamba na kuisaidia serikali katika kuhubiri amani na utulivu kwa maslahi mapana ya nchi.Msikiti huo uliojengwa pamoja na madrasa unatarajiwa kuswaliwa na waumini zaidi ya elfu moja ( 1000) kwa wakati mmoja.
