UCHIMBAJI WA MCHANGA OVYO UNAVYOCHOCHEA UHARIBIFU WA MAZINGIRA ENEO LA FUNGUREFU

Na Abdul Sakaza

Akiripoti Kutoka Kaskazini Unguja

Imeboreshwa Saa 9 Zilizopita

“Hili shamba alianza kulima mama yangu, baadae tulirithi na kulilima kwa zaidi ya miaka thelathini. Leo shamba letu halipo tena, limegeuzwa shimo tupu la mchanga.”

 Ni sauti iliyojaa huzuni nzito ya Mzee Ali Juma Shauri, miaka 60 Mkazi wa Pitanazako na mmiliki wa Shamba ambalo limeharibiwa vibaya na shuhuli za uchimbaji mchanga katika eneo la Fungurefu akieleza kwa uchungu namna alivyopoteza shamba la familia ambalo kwa miongo kadhaa lilikuwa tegemeo la maisha yao, alisema “kila anapofika eneo hilo, hukumbwa na majonzi makubwa baada ya kushuhudia ardhi iliyokuwa ikizalisha mazao sasa imebaki mashimo makubwa yasiyo na matumaini”

Uchimbaji wa mchanga kwa ajili ya shughuli mbali mbali za ujenzi umeendelea kuwa tatizo sugu katika eneo la Fungurefu, Shehia ya Mto wa Pwani, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo Uchunguzi unaonyesha wachimbaji wa mchanga wamevamia mashamba ya wakulima,maeneo ya uanikaji dagaa pamoja na maeneo mengine ya kijamii, hali iliyosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kuhatarisha maisha na usalama wa binaadam .

Kwa mujibu wa uchunguzi wa kina uliofanywa katika eneo hilo, imebainika kuwa uchimbaji wa mchanga haufanyiki tu katika maeneo ya wazi bali pia ndani ya mashamba ya kilimo, maeneo tengefu ya uanikaji dagaa na hata pembezoni mwa hifadhi ya mikoko.

Hali hii imesababisha uharibifu wa ardhi, kupotea kwa rutuba ya udongo na kudhoofika kwa uchumi wa wakulima wanaotegemea ardhi hiyo kama chanzo kikuu cha chakula na kipato.

MAONI YA WAKULIMA

Wakulima katika eneo la Fungurefu wanasema mashamba yao yameharibika kwa kiwango kikubwa kiasi cha kushindwa kutumika tena kwa shughuli za kilimo au makazi ya kijamii, kutokana na mashimo makubwa yaliyoachwa baada ya uchimbaji wa mchanga huo.

Juma Khamis Ali, miaka 48, mkazi wa Kivunge , anasema shamba lake limegeuzwa shimo kubwa lisilo salama, hali iliyoharibu kabisa uzalishaji wa chakula na uchumi wa familia yake na itachukua miaka mingi shamba lake kurejesheka tena kwa ajili ya kilimo“Nilikuwa nalima Viazi vitamu, Mpunga na Matikiti. Kupitia shamba hili niliwasomesha watoto wangu hadi chuo kikuu. Leo shamba halipo tena, watoto bado wapo chuoni, sijui nitapata wapi ada yao,” alisema mkulima Juma Khamis kwa masikitiko makubwa.

Nae, Asha Mussa Haji, miaka 42, mkazi wa Mkokotoni, anasema kupotea kwa ardhi ya kilimo ambayo imechimbwa mchanga Fungurefu kumemlazimu kutegemea vibarua visivyo na uhakika wa kipato “Hapa tulikuwa tunalima na kupata chakula cha familia. Sasa ardhi imeharibika, hata kulima haiwezekani. Maisha yamekuwa magumu sana, sasa ni muda wa kupanda mpunga shamba limegeuzwa shimo wapi nitalima,” alisema  Asha.

Mzee Abdalla Salum Omar, miaka 60, anasema ardhi aliyoirithi kutoka kwa wazazi wake sasa haina tena thamani ya uzalishaji na kuongeza kua shamba lake lilikua na mazao ya Muhogo na Viazi vitamu lakini lilichimbwa mchanga licha ya kutokomaa  kwa mazao hayo “Hii ardhi ilikuwa urithi wetu na tumekua tukitegemea. Leo imeharibiwa, haina maana tena,” alisema kwa huzuni mzee abdallah .

Amina Hamza Juma miaka 45 mkaazi wa Kivunge yeye hulima zao la   Mpunga kwa ajili ya chakula cha nyumbani tu na   kwa Mwaka Mmoja wa mavuno hupata vipolo kumi na tano (15)  vya kilo Hamsini (50) ambapo vipolo hivyo sawa na kilo Mia Saba Na Hamsini (750) ambapo kwa bei ya mchele wa mapembe  ambao unauzwa kilo moja elfu mbili (2,000) kilo Mia Saba Na Hamsini (750) sawa  na shilingi milioni moja na laki tano (1,500,000)  

Kwa upande wake mzee Juma Machu Nahoda miaka 50 mkaazi wa Mkwajuni yeye hulima Viazi vitamu na kwa mwaka mmoja wa mavuno hupata Vipolo Kumi Na Tatu (13) vya kilo Hamsini(50) ambapo kipolo kimoja huuza Shilingi Elfu Thelathini Na Tano (35,000 ) Vipolo Kumi Na Tatu (13) sawa na Shilingi Laki Nne Na Hamsini Na Tano Elfu (455,000)

                                           Jedwali: Uzalishaji Na Mapato Ya Wakulima

Jina la MkulimaMazaoIdadi ya VipoloJumla ya Kilo na vipoloBei kwa KipimoJumla ya Mapato (TZS)
Amina Hamza JumaMpunga15750 kg2,000 kwa kilo1,500,000
Juma Machu NahodaViazi vitamu1313 vipolo35,000 kwa kipolo455,000

Kulingana na takwimu hizo, ni wazi kuwa hata kilimo cha kiwango cha ngazi ya familia kina thamani kubwa kiuchumi,Mapato ya zaidi ya shilingi milioni moja kwa Mpunga na maelfu kwa Viazi vitamu kwa msimu mmoja yanaonesha mchango wa moja kwa moja wa ardhi katika ustawi wa familia hizi, Lakini iwapo uzalishaji huu utaathiriwa, athari zake hazitaishia kwa mkulima mmoja, bali zitaigusa familia na uchumi wa jamii kwa ujumla.

SABABU ZA VIJANA KUCHIMBA MCHANGA

Vijana wanaojihusisha na uchimbaji wa mchanga katika eneo la Fungurefu wanasema ukosefu wa ajira, umasikini na kukosekana kwa fursa mbadala za kiuchumi ndizo sababu kuu zinazowasukuma kuingia katika shughuli hiyo, licha ya kufahamu athari zake kwa mazingira na jamii.

Ali Hassan Said (sio jina lake halisi), miaka 26, anasema hana elimu ya juu wala mtaji wa kuanzisha shughuli nyingine za kiuchumi.“Nimehitimu elimu ya msingi tu. Sina kazi ya uhakika, sina mtaji wa biashara. Uchimbaji wa mchanga ndio unaonisaidia kupata pesa ya chakula na  kuendesha maisha yangu. Najua kuna hatari, lakini sina chaguo jingine,” alisema  Ali kwa sauti ya kujitetea.

Mussa Juma Bakari, miaka 29, anasema licha ya kazi hiyo kuwa na hofu ya kukamatwa na mamlaka, bado anaendelea kwa sababu humpatia kipato cha haraka ambacho kinaweza kukamilisha mahitaji yake “Kazi hii inatulipa haraka. Ukienda kwingine unaambiwa huna uzoefu au elimu. Hapa mchanga upo, wanunuzi wapo. Tunajua  hatari ila tutafanya  nini pia nimekamilisha mahari kwa sababu ya mchanga,” alisema Mussa.

Baadhi ya vijana ambao wanajishughulisha na uchimbaji wa mchanga wanadai kua baadhi ya maeneo ambayo yanachotwa mchanga yapo kihalali kwani husimamiwa na wamiliki wa maeneo(eka) husika, Salum Ali Machano,miaka 31, anasema wamiliki wa mashamba ndio wanaowaruhusu kuchimba mchanga kwa hofu ya maeneo yao kuchukuliwa na serikali ” wenye mashamba wanatuambia tuchimbe mchanga wao. Wanasema wakiacha tu, serikali itachukua eneo. Kwa hiyo wanauza mchanga ili wapate chochote kabla ya kupoteza ardhi yao,” alisema Salum.

Bakari Omar Khamis, miaka 27, anakiri kuwa katika baadhi ya maeneo, wamiliki wa mashamba ndio wahusika wakuu wa kuuza maeneo yao ila maeneo mengine wanachota bila ya uwepo wa wamiliki wa mashamba hayo “si kweli kua wachimbaji wote tunaiba mchanga, Wapo wenye mashamba wanauza kwa makusudi. Sisi tunafanya kazi kwa makubaliano nao ila wapo kweli wanaiba” alisema Bakari.

Hili linathibitishwa na Adam Juma Ali ambae sio jina lake halisi,yeye ni miongoni mwa wamiliki wa maeneo ambayo yanachimbwa mchanga katika eneo la Fungurefu ,anasema anauza mchanga ili kupata pesa za kujikwamua na umasikini na pia amesikia kua eneo la fungurefu linategemewa kuuzwa “sikutaka kuchimba mchanga ila hapa pakiuzwa sitopata chochote”  alisema Adam

MASHIMO YA MCHANGA NA ATHARI ZAKE

Katika hali isiyo ya kawaida ndani ya kipindi kifupi tu tayari mashimo hayo ya mchanga yameaza kuleta hofu kwa wakazi wa maeneo hayo ya Fungurefu na maeneo Jirani, Zainab Omar Said, miaka 38, mkazi wa eneo hilo, anasema mashimo yaliyoachwa wazi ni tishio kubwa hasa kwa watoto katika kipindi cha mvua za masika “Mashimo haya yanaachwa wazi bila uzio. Kipindi cha mvua hujaa maji na watoto wanaweza kudondoka bila kujua kina chake. Tunahofia maisha ya watoto wetu kila siku,” alisema Zainab kwa wasiwasi mkubwa.

Kulingana na picha satalaiti za Google Earth, inaonekana wazi kuwa takribani Miaka Mitatu iliyopita eneo hili lilikuwa na mashamba ya kijani, maeneo tambarare ya kilimo na sehemu maalum za uanikaji dagaa. Hakukuwa na mashimo makubwa wala dalili za uharibifu wa ardhi kama unaoonekana sasa. Hata hivyo, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa, ambapo maeneo makubwa sasa yamegeuka kuwa mashimo marefu na mapana, huku  yakiwa yameachwa wazi bila kuwekewa uzio.

Mashimo haya yamesababisha kupotea kwa ardhi yenye rutuba, kuharibu mifumo ya asili ya maji, na kuongeza hatari ya maafa hasa wakati wa mvua. Katika kipindi cha masika, mashimo haya hujaa maji na kubadilika kuwa mabwawa yasiyo na kingo salama, hali inayoongeza hatari ya watoto, mifugo na hata watu wazima kudondoka au kuzama bila msaada wa haraka.

Ahmed Salim Khatib, miaka 45, mkazi wa Mkokotoni, anasema jamii inaishi na wasiwasi  kuhusu  khatma ya eneo la Fungurefu linalochimbwa mchanga kwani hawafahamu  kama lipo kihalali au halipo kihalali, ”Kinachotushangaza ni kuona mamlaka ziko kimya wakati uharibifu unaendelea kila siku. Tunahitaji majibu ya wazi kutoka kwa taasisi zinazohusika,” alisema Ahmed.

Anaongeza“Haya mashimo si ya kawaida. Mengine yana kina kirefu sana. Mtoto akianguka huwezi kumpata kwa haraka. Hakuna alama, hakuna uzio, hakuna onyo,”

Mbali na athari za kimazingira, uchunguzi unaonesha kuwa uchimbaji wa mchanga umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ajira za utotoni katika eneo hilo. Vijana wadogo na watoto wameanza kuacha Shule na Madrasa ili kushiriki katika shughuli za uchimbaji mchanga kama njia ya kupata kipato.

Mwalimu mmoja kutoka Shule ya Mto wa Pwani, ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema zaidi ya watoto kumi na nne wameacha shule  na wengine kutokua na mahudhurio mazuri baada ya kujiingiza katika shughuli hizo.“baadhi ya wanafunzi tuliona mahudhurio yao ni duni, tulifatilia na tuligundua baadhi yao wako kwenye mashimo ya mchanga. Hii ni hatari kwa  maisha yao ya baadaye,” anasema mwalimu huyo kwa masikitiko.

Anaeleza kuwa hali hiyo imewaathiri kisaikolojia baadhi ya wanafunzi waliobaki shuleni.“Watoto wanaona wenzao wanapata pesa haraka kupitia mchanga, hivyo wanakosa motisha ya kusoma,” aliongeza.

Kwa ujumla, mashimo ya mchanga katika eneo la Fungurefu si tu ishara ya uharibifu wa mazingira bali pia ni chanzo cha hatari kiafya kutokana na maeneo haya kipindi cha mvua  yanaweza kua mazalia ya mmbu wa malaria na maambukizi ya tumbo la kuhara na kutapika (Kipindupindu) hali inayohitaji hatua za haraka na madhubuti kabla madhara hayo hayajajitokeza.

UCHIMBAJI MCHANGA UNAATHARI GANI KWA WAANIKAJI DAGAA FUNGUREFU

Kundi kubwa la waanikaji dagaa ambao wengi wao wanawake, wanasema maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa muda mrefu kama maeneo tengefu ya uanikaji dagaa  baadhi yamevamiwa na sasa yanachimbwa mchanga bila taarifa yoyote. Munira Hussein Alawi ni muanikaji dagaa Fungurefu, anasema. “Sisi tunalipa kodi kupitia halmashauri na hili eneo limetengwa kwa uanikaji dagaa. Laikini sasa limevamiwa na linaharibiwa kwa kuchimbwa mchanga. Hatujui nini kinaendelea.”

Sheha wa Shehia ya Mto wa Pwani, Moh’d Ali Ali, anakiri kuwepo kwa tatizo hili lakini anasema hana taarifa ya kufunguliwa kwa eneo hilo la uchimbaji wa mchanga. Anabainisha kuwa Serikali ya Shehia imekuwa ikijaribu kutoa elimu na kusitisha uchimbaji, lakini imekuwa changamoto kutokana na baadhi ya wamiliki kuuza mashamba yao kwa makusudi ili kuchimbwa mchanga.

Anasema:“Tumefanya kila juhudi kutoa elimu, lakini wamiliki wanauza mashamba yao na shughuli za uchimbaji zinaendelea bila udhibiti.”

Kando na hilo  Sleyum Saidi Khamis, Afisa Misitu Wilaya ya Kaskazini A,  anasema hadi sasa Miti ya matunda ipo hatarini kupotea na baadhi imeshaaza kuanguka “Si tu ardhi na mazingira vinaathirika, bali pia baadhi ya miti ya matunda kama Miembe na Minazi iliyokuwa imedumu kwa muda mrefu sasa iko hatarini kupotea. Hali hii inaweza kuathiri maisha ya jamii  kwa muda mrefu.”alisema Sleyum

Hassan Khatibu Majura ni mtaalamu wa mazingira Zanzibar anasema  sehemu ambazo zinachimbwa mchanga kiholela bila ya usimamizi na ambazo zipo  kinyume cha sheria ni rahisi sana kutokea uharibifu wa kimazingira kwani yamekosa uthibitisho wa kitaalamu “eneo kama Fungurefu linaweza kuleta madhara mengi ya kimazingira kwani limekosa kibali na usimamizi, wanaochimba mchanga wao hawajui namna ya uchimbaji mchanga kitaalamu lazima utarajie uharibufu” alisema Hassan Khatibu Majura mtaalamu wa mazingira.

Wananchi wanataka hatua za haraka zichukuliwe na uwajibikaji wa taasisi husika, pamoja na ushirikiano wa wananchi katika kulinda mashamba, ardhi, na maeneo ya uanikaji dagaa.

SHERIA NA KANUNI ZA RASILIMALI ASILIA NA MAZINGIRA ZINASEMAJE

Licha ya Zanzibar kutokuwa na sheria maalum ya uchimbaji wa mchanga , uchimbaji wa rasilimali hiyo unasimamiwa kupitia sheria na kanuni mbalimbali za rasilimali asilia na mazingira. Kisheria, mchanga unatambuliwa kama sehemu ya rasilimali asilia, hivyo matumizi na uchimbaji wake yako chini ya udhibiti wa Serikali. Kwa mujibu wa Sheria ya Uimiliki wa Kudumu wa Rasilimali Asilia ya mwaka 2017 (Natural Wealth and Resources – Permanent Sovereignty Act, 2017), Serikali ina mamlaka ya kusimamia, kudhibiti na kulinda matumizi ya rasilimali zisizo hai, ikiwemo mchanga, kwa maslahi ya taifa na kizazi cha sasa na kijacho.

Sheria na taratibu zilizopo zinaelekeza kuwa hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuchimba mchanga bila kupata kibali rasmi kutoka mamlaka husika, hususan wizara au idara zinazohusika na masuala ya ardhi na mazingira. Uchimbaji unaofanyika bila kibali huchukuliwa kuwa ni kinyume cha sheria. Serikali pia imeweka utaratibu wa kuainisha maeneo maalum yanayoruhusiwa kuchimbwa mchanga baada ya kufanyiwa tathmini ya kiusalama na kimazingira, huku ikipiga marufuku uchimbaji katika maeneo yasiyoidhinishwa, hususan yaliyo karibu na makazi ya watu na vyanzo vya maji.

Kwa mujibu wa taratibu hizo, mtu au taasisi inayohitaji mchanga kwa ajili ya shughuli za ujenzi hulazimika kulipia ada na ushuru unaotakiwa kupitia mifumo rasmi ya Serikali, mara nyingi kwa njia ya kielektroniki, ili kudhibiti biashara ya mchanga na kuzuia uchimbaji holela. Aidha, Serikali imesisitiza kuwa mchanga uchimbwe katika maeneo maalum yaliyotengwa kisheria, kama vile maeneo yanayotambuliwa kuwa salama kijiolojia, na si vinginevyo.

Uchimbaji wa mchanga pia unasimamiwa chini ya Sheria ya Mazingira ya Zanzibar ya mwaka 2015 (Zanzibar Environmental Management Act No. 3 of 2015), ambayo inalenga kudhibiti shughuli zote zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira. Sheria hiyo inazuia shughuli zinazoweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi, kuharibu vyanzo vya maji au kuhatarisha makazi ya watu bila kufuata taratibu za tathmini ya athari za kimazingira (EIA). Kwa mujibu wa sheria hiyo, mradi wowote unaoweza kuathiri mazingira hulazimika kuwa na mpango wa uhifadhi wa mazingira kabla ya kupewa kibali cha utekelezaji.

Sheria hizo pia zinaweka adhabu kali kwa watu au taasisi zinazojihusisha na uchimbaji wa mchanga bila kibali, ikiwemo kutaifishwa kwa vifaa, kutozwa faini na kuchukuliwa hatua za kisheria. Serikali na viongozi wa jamii wamekuwa wakisisitiza kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya wachimbaji haramu, wakieleza kuwa uchimbaji wa mchanga ovyo unaendelea kuchochea uharibifu wa mazingira, kuhatarisha maisha ya wananchi na kuathiri maendeleo endelevu, hali inayojitokeza pia katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kaskazini, ikiwemo Fungurefu.

SIRIKALI NAMNA INAVYOKOSA MAPATO

kupitia kanuni na sheria hizi ni wazi kua Serikali ya Zanzibar inakosa mapato lukuki kutokana na eneo hili la fungurefu  hii kuchimbwa mchanga kinyume cha sheria  kutoka kwa mamlaka husika

Bei ya mchanga shimoni Toyota Daina tripu Moja ni Shilingi Elfu Ishirini (20,000) na bei ya mchanga shimoni Mitsubishi Fuso tripu moja ni Shilingi Elfu Arobaini (40,000)

Kuazia saa nne na dakika ishirini asubuhi (4:20) hadi saa kumi na moja na dakika arobaini jioni (11: 40) Gari zote kwa ujumla ambazo ni  aina ya Toyota Daina kwasiku huchukua zaidi ya triipu mia tatu na kumi (310) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Milioni Sita Na Laki Mbili (6,200,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu (9,300) sawa na Shilingi Milioni Mia Moja Na Themanini Na Sita (186,000,000)

Kadhalika Gari zote kwa ujumla ambazo ni  aina ya Mitsubishi Fuso kwasiku huchukua zaidi ya triipu Hamsini (50) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Milioni Mbili (2,000,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu Elfu Moja Namia Tano (1,500) Sawa Na Shilingi Milioni Sitini (60,000,000)

                     Jedwali La Uchambuzi Wa Mapato Ya Mchanga Fungurefu (Muda Wa Mchana)

Aina ya GariBei kwa Tripu (TSH)Tripu kwa SikuMapato kwa Siku (TSH)Tripu kwa MweziMapato kwa Mwezi (TSH)Mapato kwa Mwaka (TSH)Serikali KuuSerikali ya Kijiji
Toyota Dyna20,0003106,200,0009,300186,000,0002,232,000,00000
Mitsubishi Fuso40,000502,000,0001,50060,000,000720,000,00000
JUMLA3608,200,00010,800246,000,0002,952,000,00000

Pia tumeangalia wakati wa usiku Kuazia saa moja na dakika kumi usiku (1:10) hadi saa tano na dakika kumi usiku (5:10) Gari aina ya Toyota Daina kwa muda huu huchukua zaidi ya triipu kumi na saba (17) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Laki Tatu na Elfu Arobaini (340,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu (510) sawa na Shilingi Milioni kumi na laki mbili (10,200,000)

 Kuazia saa moja na dakika kumi usiku (1:10) hadi saa tano na dakika kumi usiku (5:10) Gari aina ya aina ya Mitsubishi Fuso huchukua zaidi ya triipu nne (4) ambazo tripu hizo ni sawa na Shilingi Elfu Themanini (80,000) ambapo kwa Mwezi huchukua tripu mia moja na ishirini (120) Sawa Na Shilingi Milioni mbili na laki nne  (2,400,000)

      Jedwali La Uchambuzi Wa Mapato Ya Mchanga Fungurefu (Muda Wa Usiku)

MaelezoBei kwa TripTrip kwa Usiku MmojaTrip kwa MweziMapato kwa Usiku MmojaMapato kwa MweziMapato kwa MwakaSerikali KuuSerikali ya Kijiji
Toyota Dyna20,00017510340,00010,200,000122,400,00000
Mitsubishi Fuso40,000412080,0002,400,00028,800,00000

Lakini Kulingana takuwimu hizi Serikali inakosa mamilioni ya fedha pamoja na Serikali ya kijiji ambazo fedha hizo zingesaidia kujenga na hata kukarabati miundombinu na huduma   za kijamii kama vile Barabara,Elimu ,Hospitali na Masoko .

 MAMLAKA ZA SERIKALI ZINASEMAJE?

Afisa Mmoja Kutoka Wizara Ya Maji, Nishati Na Madini Zanzibar amesema kwa sharti la kutotajwa jina kua eneo linalochimbwa mchanga  Fungurefu halipo kihalali na kwa muda mrefu limekua na utata na amekiri Serikali imekua ikipoteza mapato mengi kutokana na uchimbaji mchanga unao fanyika kwa njia ya haramu na magendo.

Waziri mwenye dhamana wa Wizara ya Maji, Nishati Na Madini Mh. Nadir Abdullatif hivi karibuni amefanya ziara katika maeneo yanayochimba mchanga na vifusi Mkoa Wa Kaskazini Unguja na kubaini shughuli za uchimbaji mchanga na vifusi kwa njia ya magendo huku akitoa  onyo kali kwa wale wote wanaochimba mchanga kinyume cha sheria na bila ya kibali kutoka serikalini  kuacha maramoja na badala yake kukata vibali ili kulipa kodi serikalini

Mh. Nadir amsema wataendelea kufanya doria kwa wale wote wanaochimba mchanga kinyume na sheria na amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wale wote wanaojishuhulisha na uchimbaji haramu wa mchanga.

Mkuu wa Mkoa Wa Kaskazini Unguja  mhe.Cassian Gallos Nyimbo amesema kapitia doria hiyo zaidi ya eka 1000 zimeharibiwa vibaya na uchimbaji mchanga kinyume cha sheria katika mkoa huo na kuongeza kua hali hairidhishi hata kidogo na ametoa onyo kwa wale wote wanaofanya shuhuli hizo bila ya kibali kuacha maramoja “ naomba nitoe indhari watu wanaojishirikisha kuchimba mchanga  bila ya vibali katika mkoa huu waache mara moja kwa sababu mimi sitokubali kama nikiwa Mku Wa Mkoa  huu wa Kaskazini Unguja  tutawakamata,tutawashtaki,tutataifisha magari na mali zao  ” alisema kwa msisitizo .

Kando na hilo Mh. Nyimbo ameweka bayana kua wale wenye maeneo ambayo yako vizuri katika shughuli za uchimbaji mchanga  kufika katika Wizara husika ili kupata utaratibu na kupewa kibali cha uchimbaji mchanga kisheria .

Katibu Mkuu Wa Wizara Ya Maji, Nishati Na Madini , Ndugu Joseph Kilangi, ameapa kuwafatilia wale wote wanaohujumu Uchumi wa serikali kwa kuchimba mchanga kiholela na kinyume cha sheria kua watawachukulia hatua kali za kisheria

Ameongeza kua kuchimba mchanga kiholela bila mpangilio wa Serikali kunasababisha uharibifu mkubwa na ukizingatia Zanzibar ni kisiwa ambacho kinatakiwa kulindwa ili vizazi vinavyokuja viweze kunufaika na aridhi yao

Uchunguzi wa Habari hii umebaini kua  katika Mkoa Wa Kaskazini Unguja tayari mashimo ya mchanga ya namna hii yameshawahi kuleta athari marakadhaa mwaka 2023 Watoto wanne wamepoteza maisha baada ya kuingia na kuzama katika mashimo ya mchanga Muwanda wakiwemo Watoto watatu wa familia moja, Fatma Hamza Juma Mika 13 ,Amina Hamza Juma Mika 10 ,Miraji Hamza Juma miaka 7, na Khairat Yussuf Hassan miaka 7, na majeruhi alikua Aisha Yussuf Hassan miaka 9 ambapo Tukio hili lilikua baya sana kushuhudiwa huku  liliacha wakati mgumu na hasira kwa baadhi ya wananchi.

Ili kunusuru mazingira,jamii ya Fungurefu na maeneo Jirani inahitajika nguvu ya pamoja kati ya serikali, jamii, na wachimbaji wenyewe kutambua kuwa ardhi inayoharibiwa  leo ndio tegemeo pekee la kesho yetu na ikiwa hali hii itaachiwa iendelee bila udhibiti wa dhati, eneo la Fungurefu litakabiliwa na hatari ya kugeuka jangwa lisilo na tija (wasteland), Kupotea kwa ardhi tayari ni ishara ya kwanza ya njaa ya baadae kwani mashamba yanayozalisha chakula yanatoweka.  

Aidha, bila uzio wala onyo, mashimo haya yataendelea kuwa “mabwawa ya mauti” kwa watoto, huku kukiwa na uwezekano wa mlipuko wa magonjwa kama malaria na kipindupindu wakati wa mvua za masika.

Kadhalika ni muhimu  kuazishwa  kwa Mpango wa kitaalamu wa Kurejesha Mashimo (Rehabilitation) kati ya Jamii na sirikali ili kufukia mashimo hayo (land reclamation) Huu unaweza kujumuisha upandaji wa miti inayostahimili mazingira hayo ili kurudisha rutuba na uimara wa udongo.

Kwa vijana ni muhimu kuazishwa kwa Programu za Ajira Badala ya kutegemea uchimbaji haramu, Serikali na taasisi binafsi zianzishe programu za mafunzo ya ufundi na mitaji midogo ili kuwapa fursa mbadala za kiuchumi zinazozingatia maendeleo endelevu.

 Lakini Bila hatua za makusudi kuchukuliwa sasa, swali la “khatma ya mashimo ya mchanga  Fungurefu ipo kwa nani?” litabaki kuwa kilio kisicho na jibu mbele ya mashimo yasiyo na mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *