TUZO ZA UANDISHI WA HABARI ZA TABIANCHI COMMUNITY FORESTS ZIMEZINDULIWA LEO NA TAMWA ZNZ, CFP NA CFI.

Na Abdul  Sakaza

Akiripoti Kutoka Tunguu -Mkoa Wa Kusini Unguja

Imeboreshwa Saa 9 Zilizopita

ZANZIBAR – Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na Community Forests Pemba (CFP) na Community Forests International (CFI), kimezindua rasmi Tuzo za Uandishi wa Habari za Tabianchi za Community Forests, zikiwa na lengo la kuonyesha mchango na uongozi wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo  katika ufunguzi wa tuzo hizo  ukumbi wa TAMWA ZNZ Tunguu, Mkurugenzi wa Community Forests Pemba, Mbarouk Mussa Omar, amesema kuwa tuzo hizo zinalenga kutambua mchango wa waandishi wa habari na vyombo vya habari Zanzibar vinavyoandika, kurusha na kusambaza habari zinazoonyesha mchango wa wanawake na uongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hususan katika eneo la mikoko, kilimo mseto kinachostahimili tabianchi na kukuza usawa wa kijinsia.

Mbarouk amesema kuwa kupitia tuzo hizo, TAMWA ZNZ, CFP na CFI zinalenga kukuza uandishi wa habari unaoonyesha uongozi wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kutambua mchango wa waandishi wa habari mahiri wanaoandika habari zinazohusu wanawake na uongozi. Aidha ameweka bayana kua  tuzo hizo zinahamasisha uandishi wa habari unaozingatia usawa wa kijinsia, ushahidi wa kisayansi na hadithi za mabadiliko chanya kutoka ngazi ya jamii.

Kwa upande wake, Mkuu  Mawasiliano Kitengo cha Habari TAMWA ZNZ, Sophia Ngalapi, amesema licha ya wanawake kuwa mstari wa mbele katika shughuli za kilimo-misitu, uhifadhi wa mikoko na mbinu nyingine za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mchango na uongozi wao bado hauonekani vya kutosha katika vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.

Sophia amesisitiza kuwa uwakilishi mdogo wa wanawake katika simulizi za vyombo vya habari haupunguzi tu nafasi yao ya kushiriki na kuongoza, bali hupunguza mwonekano wa mikakati bora ya jamii katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, utafiti uliofanywa na mradi wa ZanzAdapt mwanzoni mwa mwaka jana unaonesha kuwa sehemu ndogo tu ya habari zilizochambuliwa kutoka vyombo mbalimbali ilijumuisha sauti za wanawake, huku ni sehemu ndogo zaidi zilizoonyesha wanawake kama viongozi katika masuala ya tabianchi.

Mradi wa ZanzAdapt, unaotekelezwa na Community Forests International na Community Forests Pemba kwa ushirikiano na TAMWA Zanzibar, unalenga kuziba pengo hili kwa kuhamasisha uandishi wa habari unaozingatia usawa wa kijinsia na kuonyesha uongozi wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Tuzo hizi zitalenga makundi makuu ya vyombo vya Habari ikiwemo magazeti, vipindi vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii, na kazi zote lazima ziwe zikionyesha masuala ya mabadiliko ya tabianchi Zanzibar pamoja na sauti na uongozi wa wanawake.

Aidha, kutakuwa na tuzo maalumu zinazotambua chombo cha habari kilichoonyesha uwajibikaji zaidi katika masuala ya wanawake na uongozi, tuzo ya mwandishi wa habari kijana, tuzo ya uandishi wa habari wa mitandao ya kijamii yenye mashabiki wengi zaidi na tuzo kwa habari iliyoonyesha kwa kina nafasi ya wanawake na uongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Vigezo vya tathmini ni pamoja na kuonyesha sauti na uongozi wa wanawake, usawa wa kijinsia, ubora wa picha na sauti, ubunifu, uchunguzi bora, ufasaha wa lugha, ushawishi kwa jamii na uwasilishaji wa habari. Kipindi cha redio na televisheni kisizidi dakika thelathini na picha na sauti ziwe katika ubora unaostahiki.

Dirisha la kupokea kazi limefunguliwa na litadumu kwa muda wa wiki tatu, ambapo kazi lazima ziwe zilizochapishwa au kurushwa hewani kuanzia mwanzo wa mwaka jana hadi mwishoni mwa mwaka jana. Waandishi wanatakiwa kuwasilisha kazi mbili kila mmoja kupitia kiungo cha mtandao au moja kwa moja katika ofisi za TAMWA ZNZ Unguja na Pemba.

Hafla ya utoaji wa tuzo inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa tatu, ikihusisha waandishi wa habari, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari, taasisi za kiserikali, zisizo za kiserikali na wadau wa kimataifa.

TAMWA ZNZ, CFP na CFI wanasema tuzo hizi ni jukwaa muhimu la kuonyesha nguvu ya uandishi wa habari katika kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kimazingira, huku zikizingatia usawa wa kijinsia na uongozi wa wanawake.

Kwa maelezo zaidi, wasiliana na: info@tamwaznz.or.tz & ngalapi@tamwaznz.or.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *