Kauli ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuhusu kuwapa askari risasi 120 kabla ya uchaguzi mkuu imezua hofu na ukosoaji mkubwa. Upinzani na wananchi waonya vitisho hivyo vinaweza kudhoofisha amani, demokrasia na haki.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekosolewa vikali kufuatia kauli yake kuhusu maandalizi ya kuwapa askari polisi na wanajeshi risasi 120 kila mmoja kwa ajili ya kukabiliana na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwakani. Kauli hiyo imeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi kuhusu usalama, demokrasia na haki za binadamu.
Museveni alitoa matamshi hayo wakati akijibu swali la mwanahabari katika moja ya vikao vya jioni vya kampeni zake. Swali hilo lilihusu mwito wa mara kwa mara wa mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi, anayejulikana kama Bobi Wine, anayewahimiza wapigakura kubaki kwenye vituo vya kupigia kura ili kuhakikisha kura zao haziibiwi.
Akijibu, rais Museveni ambaye ni mgombea wa chama tawala cha NRM, alisema kuwa askari wa usalama wako tayari kukabiliana na vurugu zozote, akitaja idadi ya risasi walizonazo kama ishara ya nguvu ya dola.
“Nimekuwa nikimsikia Kyagulanyi akisema askari ni wachache na wanaoweza kufanya vurugu ni wengi. Msimsikilize, kwa sababu kila askari ana risasi 120. Mkisema wanaofanya vurugu ni wengi, walingenisheni na idadi ya risasi za askari,” alisema Museveni.
Kauli hiyo imeibua hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi wengi, huku baadhi wakisema matamshi hayo yanaweza kuwakatisha tamaa raia kujitokeza kupiga kura. Wengine wameeleza kuwa amani na uthabiti wa taifa haviwezi kudumishwa kwa vitisho vya silaha.
